Habari za Punde

Makarani washauriwa: Msizifanyie biashara hukumu za majaji, mahakimu

Na Haji Nassor, Pemba
MAKARANI wa mahakama nchini, wametakiwa kuacha tabia ya kuchungulia maamuzi yanayofanywa na mahakimu au majaji na kisha kuwafuata na watuhumiwa, kwa lengo la kujipatia fedha, wakiwaeleza kuwa, wanaweza kuwasaidi kushinda kesi zao.
Baadhi ya makarani hao, wametajwa kuwa, kutokana na ukaribu wao na mahakimu au majaji hao, wamekuwa wakijifanya wema kwa kuwapa taarifa watuhumiwa, kwamba wanaweza kuwasaidia, iwapo watawapatia kiasi cha fedha.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar, Khamis Juma Maalimu, alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa wa Idaza za mahakama kisiwani Pemba.
Alisema wapo baadhi yao na wameshapokea malalamiko, kwamba huwadai vitu watuhumiwa au walalamikaji, wakijifanya wametumwa na mahakimu na majaji, kwamba kesi zao zimeshaelekea vibaya na bila ya kutoa chochote zinaweza kuwageuka.
Alisema wapo wanaofanya hivyo hata bila ya mahakimu hao kuwa na taarifa juu ya jambo hilo, na kuwapaka matope mahakimu na majaji.
“Jamani suala la maadili lazima tuwe makini sana, na hasa nyinyi baadhi ya makarani, ukaribu wenu na mahakimu na majaji, wakati mwengine mnautumia vibaya’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine Naibu huyo Waziri, amewataka mahakimu wa mahakama za kadhi Zanzibar, kufanya kila juhudi na kutumia ujuzi na elimu zao, ili kuzinusuru ndoa na hatimae watoto kukosa matunzo.
Alisema ijapokuwa wanaofika mahakamani hapo wengi wao hutaka talaka, lakini ni vyema wakatumia taaluma zao, ili kuzinusuru ndoa hizo, kwa lengo la kuwapa watoto matunzo.
“Ongezeko la takala lipo na linaendelea, lakini nyinyi mahakimu wa mahakama zetu hizi za Kadhi, angalieni sana kwanza msivunje ndoa, bora sulhu ipite, maana waathirika wa migogoro ya ndoa ni watoto wetu’’,alifafanua.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kubingwa Mashaka Simba, alisema sasa serikali inajipanga ili kukamilisha sera ya mfuko wa bima ya afya Zanzibar, kwa ajili ya watumishi wake.
Alisema kila uchao gharama za matibabu zinaongezeka, na ndio maana sasa sera inakuja na sheria yake itaandaliwa, ili kuwapunguzia mzigo wa matibabu wafanyakazi.
“Jambo zuri sana kuwa na mfuko wa bima ya afya, na sasa sera iko njiani kukamilika, na sasa kazi iliopo kwenu wafanyakazi ni kuukubali na kuunga mkono mfuko huo’’,alifafanua.
Awali Hakimu wa mahaka ya wilaya Wete Taki Abdalla Habibu, aliiomba wizara hiyo, kuangalia uwezekano wa kuanza kwa mfuko wa bima ya afya kwa watumishi wa umma, hasa kutokana na uwepo wa mishahara midogo .
Akisoma ripoti ya kazi, Mrajis wa Jimbo Mahakamu Kuu Pemba Hussein Makame Hussein, alisema bado Idara ya mahakama inakabiliwa na changamoto ya ukachakuvu wa majengo.
“Muhueshimiwa hili jengo la mahakama ya Chakechake liko safi, lakini bado Wete, Mkoani na hata Konde, hali hairidhishi sana’’,alifafanua.

Awali ujumbe huo ukiongozwa na Naibu Waziri, Naibu Katibu  mkuu, Afisa Mdhamini na mahakimu wa mkoa, ulitembelea jengo lililofanyiwa mtengenezo makubwa la Chakechake, Konde na Wete.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.