Habari za Punde

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                                         30.11.2016
---
RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Kenya na kuahidi kurejeshwa utamaduni wa safari za meli kati ya Zanzibar na Mombasa kwa kutumia meli yake mpya ya MV Mapinduzi II.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa  Kenya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Chirau Ali Mwakwere.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Mwakwere kuwa mbali ya ujirani wa mipaka kati ya Zanzibar na Kenya pande mbili hizo pia, zina udugu wa asili  ambao ulikuza uhusiano wa kiuchumi na kiutamaduni, hivyo ipo haja ya kuuendeleza.

Aidha, Dk. Shein amelipokea mikono miwili ombi la Balozi huyo la kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa baharini kwa kuanzisha safari za meli kati ya Zanzibar na Mombasa, jambo ambalo Rais alisema kuwa limo katika mipango ya kutekelezwa.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kurejesha safari za meli zilizokuwepo hapo siku za nyuma baina ya Mombasa na visiwa vya Zanzibar na si muda mrefu safari hizo zitaanza huku akieleza kuwa safari za Tanga, Mtwara, Dar-es-Salaam na hata Comoro nazo zitajumuishwa.

Mbali na hilo, Dk. Shein aliunga mkono wazo la Balozi Mwakwere la kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kati ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Zanzibar na vyuo vikuu vya nchini Kenya na kueleza kuwa hatua hiyo itazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo sambamba na kuinua sekta ya elimu.

Dk. Shein alimueleza Balozi Mwakwere kuwa kumekuwa na uhusiano wa kidugu na wa kihistoria kati ya Tanzania na Kenya hatua ambaye imeipelekea kuwepo kwa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko mjini Mombasa.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa nchi mbili hizo zimekuwa na historia ya kusaidiana pale nchi moja wapo inapopata matatizo, hivyo ana imani kubwa utamaduni huo utaendelezwa kwa manufaa ya pamoja.

Nae Balozi wa Kenya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chirau Ali Mwakwere alimueleza Dk. Shein kuwa Kenya inajivunia uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi kuukuza na kuuendeleza.

Katika kuendeleza na kuukuza uhusiano na ushirikiano huo, Balozi Mwakwere alitoa ombi maalum kwa Dk. Shein kurejeshwa utamaduni uliokuwepo hapo siku za nyuma za kuwemo usafiri wa baharini kati ya Zanzibar na Mombasa.

Aidha, Balozi Mwakwere alimueleza Dk. Shein haja ya kuwepo kwa uhusiano na ushirikiano wa kubadilishana uzoefu na utaalamu  wa wanafunzi kati ya vyuo vikuu vya Zanzibar na vile vya kenya ili vijana waweze kuutambua na kuukuza uhusiano uliopo.

Balozi Mwakwere alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa amani, utulivu na maendeleo na kuahidi kuwa Kenya chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyata  itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake hizo.

Alisema kuwa kwa vile Kenya hasa maeneo yake ya ukanda wa pwani tamaduni, silka na desturi zake zimeshabihiana na Zanzibar ni vyema uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo ukaimarishwa zaidi hasa katika sekta ya biashara na utalii.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Kenya imechukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha maeneo ya ukanda wote wa Pwani ya nchi hiyo unaendelea kutunza utamaduni, silka na desturi zao za asili.

Sambamba na hayo, Balozi Mwakwere alipongeza hatua za kuendelea kuyalinda na kuyatunza Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo yaliondosha unyonge na kuleta utu na demokrasia na kuifanya Zanzibar iweze kujisimamia mambo yake wenyewe.

Balozi Mwakwere alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na watu wake kwa kuendelea kuilinda na kuitunza lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa lugha maarufu ndani na nje ya Bara la Afrika na kusema kuwa wananchi wa Kenya wamekuwa wakikizungumza na kukipenda Kiswahili cha Zanzibar ambacho ndicho cha asili.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.