Umoja wa Mataifa umeingia
ushirikiano na FURSA ili kuongeza uelewa wa malengo ya maendeleo endelevu kwa
vijana zaidi ya 10,000 katika mikoa mitatu ya Dodoma, Dar es Salaam pamoja na
Kigoma.
Fursa, ambayo imekuwa ikifanyika
kwa miaka mitatu iliyopita, imejikita katika kuwajengea uwezo vijana wa
kuzitambua fursa katika maeneo yao wanayoishi lakini pia namna ya kutengeneza
miradi na biashara kupitia fursa hizo.
Ushirikiano wa Fursa na Umoja wa
Mataifa utalenga kuwafikia vijana wanaohudhuria semina za Fursa kuelewa namna Malengo
ya Dunia yanavyohusiana na maisha yao ya kila siku na wajibu wa kila kijana
katika kushiriki kuyakamilisha.
Akizungumza wakati wa kuzindua
semina za Fursa mkoani Dodoma, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez alisema semina za Fursa zimeweza kubadilisha
maisha ya vijana wengi na hivyo ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa katika
kufikia vijana utatoa nafasi ya vijana kuyaelewa Malengo ya Dunia.
‘Vijana wengi wana ari ya kushiriki
katika kufanikisha Malengo ya Dunia, ndio maana Umoja wa Mataifa umeamua
kushirikiana na Fursa ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanayafahamu malengo
haya lakini pia wanashiriki katika kuyatekeleza’ alisema Alvaro.
Kwa
upande wake, Mwanzilishi wa Fursa, Ruge Mutahaba amesema kwa zaidi ya miaka
mitatu sasa Fursa imefanikiwa kuwafikia zaidi ya vijana milioni 5, na kuwapa
mbinu na maarifa ya kuweza kutumia fursa katika maeneo yao.
‘Tunaushukuru
Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Fursa kuwafikia vijana katika mikoa ya
Dodoma, Dar es Salaam na Kigoma, ili sio tu wapate nafasi ya kupata mafunzo ya
Fursa na biashara balipia mafunzo juu ya Malengo ya Dunia’ alisema Ruge.
No comments:
Post a Comment