Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Atia Saini Kitabu cha Maombolezi ya Rais wa Cuda Dar leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisaini kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Cuba Bwana Fidel Castro kwenye ubalozi wa Cuba Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam.
Kushoto yas Balozi Seif aliyesimama ni Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez.
Balozi Seif akitia saini kitabu hicho akishuhudiwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar  Mh. Harus Said Suleiman pamoja na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga.
Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kushoto akimfariji Balozi wa Cuba Nchini Tanzania wa kwanza kutoka kushoto mara baada ya kutia saini Kitabu cha maombolezo ya Kifo cha Rais Mstaafu wa Cuba Bwana Fidel Castro.
Kushoto ya Balozi Seif ni na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar  Mh. Harus Said Suleiman , Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga pamoja na Mratibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ  Dar es salaam Nd. Issa Mlingoti Ali.
Balozi wa Cuba Bwana Jorge Luis Lopez akiagwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar  Mh. Harus Said Suleiman baada ya kumalizika kwa kazi ya utiaji saini.
Balozi wa Cuba Bwana Jorge Luis Lopez akiagwa na Naibu Waziri wa  baada ya kumalizika kwa kazi ya utiaji saini.Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga(Picha na Hassan Issa OMPR)

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametia saini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Marehemu Fidel Alejandro Castro Ruz  kilichotokea Tarehe 25 Novemba 2016 katika Mji wa Biran Nchini Cuba.

Utiaji saini huo wa Kitabu cha Maombolezo ameufanya katika Makaazi ya Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Nchini Tanzania uliopo Bara bara ya Ali Bin Said Mtaa wa Namanga Jijini Dar es salaam.

Balozi Seif  ameiwakilisha Serikali ya Mainduzi ya Zanzibar katika utiaji saini huo akiambatana na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar  Mh. Harus Said Suleiman , Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga pamoja na Mratibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ  Dar es salaam Nd. Issa Mlingoti Ali.

Marehemu Fidel Alejandro Castro Ruz  aliyefikia umri wa Miaka 90 alifanikiwa kuiongoza Jamuhuri ya Cuba akiwa na umri wa Miaka`32 kuanzia mwaka 1959 baada ya vugu vugu la kampeni ya kuuondosha Madarakani utawala wa Batista mwaka 1958 akisaidiwa na Kaka Yake Raul Castro pamoja na mwana harakati wa kupigania ukombozi wa wanyonge Kamanda Guavara.

Akimfariji Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Bwana  Jorge  Luis Loez baada ya saini hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Kifo cha Jemedari huyo wa Taifa la Cuba hakikuacha pengo kwa nchi hiyo lakini pia kimeigusa Tanzania kutokana na Mataifa hayo kufanana katika harakati zao za kupigania Uhuru kutoka makucha ya Kikoloni.

Balozi Seif alisema Jamuhuri ya Cuba ni kaka wa Tanzania katika njia ya kusaidia maendeleo na nyanja za uchumi zilizopata ufanisi mkubwa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Wataalamu wa Nchi hiyo kuwawezesha Kitaaluma wananchi Wazalendo wa Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Balozi huyo wa Cuba Nchini Tanzania amewataka Wananchi wa Taifa hilo lilioko katika Bahari ya Carribean kukubali kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi cha kuondokewa na Kipenzi Rais wao Mstaafu Kamanda Fidel Castro.

Akitoa shukrani zake  Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez alisema Cuba itaendele kuwa mshirika mkubwa wa Tanzania katika azma yake ya kuona wananchi waliowengi wa ngazi ya chini wa Mataifa hayo wanafaidika na Uhuru walioupata kutoka katika makucha ya wakoloni.

Balozi Lopez alisema Cuba na Tanzania zimeshirikiana kwa muda mrefu uliobakia kuwa Historia kwa sasa hasa katika sekta za Afya, Kilimo, Viwanda na masomo ya Elimu ya Juu, ushirikiano uliowekwa msingi wake  na Waasisi wa Nchi hizo Mbili Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na Bwana Fidel Castro. 

Marehemu Fidel Castro alizaliwa Mnamo Tarehe 13 Agosti mwaka 1926 ndani ya familia ya watoto Sita akiwa watatu  wa Mzee Angel aliyekuwa mfanyakazi wa mashamba ya miwa akiwa na asili ya Taifa la Hispania.

Marehemu Fidel Castro katika utoto wake alionyesha kipawa chake wakati alipoanza kupata elimu iliyomuwezesha kuonekana mwenye akili kubwa katika masomo yake Darasani tokea maandalizi,msingi, sekondari hadi chuo Kikuu.

Alipohitimu  masomo yake katika Chuo Kikuu cha  El  Colegio de Belen Mjini Havana Nchini Cuba Marehemu Fidel Castro aliamua kujiunga katika  harakati za Kisiasa zilizompelekea kukumbwa na misuko suko kadhaa  iliyomsababishia kuikimbia Cuba katika miaka ya 40.

Alirejea  Nchini Cuba Disemba 2 mwaka 1956  akiambatana na zaidi ya askari 80 wakiwa na silaha kwa ajili ya mapambano lakini nguvu za Kijeshi za Batista zilisababisha kushindwa kwa jeshi hilo na hatimae Castro, Raul, Guavara na baadhi ya askari wao waliamua kukimbilia katika milima ya Sierra Maestra.

Miaka miwili baadaye Marehemu Castrol alijiimarisha tena kijeshi kwa lengo la kupambana kwa mara nyengine na Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Batista ambapo mwanzoni mwa mwaka 1958 akaanza kampeni ya kujipenyeza tena Nchini Cuba.

Mbinu za kuimarisha majimbo sambamba  na kuyashawishi makampuni ya Kilimo na Viwanda kumkubali  zilimuwezesha Castrol na washirika wake kuongeza nguvu zilizoisambatarisha Serikali ya Batista iliyokosa nguvu za kiutawala na hatimae  Jeshi la Castrol likafanikiwa kuidhibiti Cuba Kijeshi.

Mwezi Januari mwaka 1959  Batista aliamua kukimbilia Jamuhuri ya Dominica baada ya Serikali yake kushindwa nguvu na Kikosi cha Castrol akisaidiwa na Kaka yake Raul na Mwanaharakati za kupigania uhuru wa wanyonge Kamanda Enersto Guavara.

Bwana Fidel Castro alilazimika kukasimu madaraka kwa  kumteuwa Kaka yake Raul Castro mnamo Tarehe 31 Julai 2006 kukaimu nafasi hiyo  baada ya  afya yake kutomruhusu kuendelea kushika wadhifa wa Urais wa Cuba.

Tarehe 24 Febuari mwaka 2008 Bwana Raul akashika rasmi nafasi hiyo ya Urais na kuendelea kuliongoza Taifa hilo hadi hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.