Habari za Punde

Haya majipu yaliomo kwenye familia pia yamngoja Magufuli?


Na Haji Nassor, Pemba
RASI wa awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufulia, maarufu kama mzee wa kuyatumbua, anaendelea vymea kuwaongoza watanzania kama alivyoahidi.
Kila mmoja wakati alipokuwa kwenye mikutano yake ya kampeni, kwamba akipata ridhaa na kuingia Ikulu, basi atayashughulikia mijizi kama lugha yake, ingawa wapo walioguna kwa wakati huo.
Kila mmoja sasa ni shahidi, kwamba ‘JMP’ amekuwa akiwaweka hadharani wahujumu wa uchumi, ambao wanaonekana kama walikuwa wameshaota mizizi kwenye taasisi za umma.
Kwa staili hii ya kuwaripua watendaji wanaonekana kuzitumia vibaya ofisi za umma na baadhi yao kufikishwa mahakamani, walau watanzania wanaona kuwa, utekelezaji wa ahadi hiyo upo.
Lakini ninachojuliza hata haya majipu, yaliomo kwenye familia kwa kesi za ubakaji na za vipigo kwa wanawake, yanamsubiri rais John Pombe Magufuli kuyatumbua?
Maana wapo wanaojiita wanaume, ambao wamekuwa mstari wa mbele kuendeleza vipigo kwa wanawake na ubakaji wa watoto, ambapo jamii imeshindwa kuyatumbua majipu hayo.
Ndio maana…. naja tena hewani kuiuliza jamii, basi hata huu udhalilishaji uliopo kwa makundi hayo, nayo ili yakome yanamsubiri mzee wa kuyatumbua?
Lazima jamii ikae na kutafakari kwamba, watoto waliopo leo ndio wazee na viongozi wa mwaka kesho, sasa kama watawafanyia udhalilishaji ukiwemo wa kuwabaka, ndio tutakuwa na taifa la aina gani?
Lakini hata wale wanaume wanaotoka masafa marefu kwenda kijiji hadi mtaa mmoja kuchagulia mwenzawe, na kisha baada ya siku, kumkaribisha kwa kipigo, ndio jamii imeshindwa kudhibiti?
Mimi nadhani tusimkabidhi kila jambo rais wetu mpendwa Magufuli, maana na yeye ni mwanadamu kama ulivyo wewe na mimi, sasa lazima huu udhalilishaji uliomo kwenye familia zetu, tutumbuane majipu wenyewe kwa wenyewe.
Tena ndani ya jamii ni rahisi kutumbuana, maana kama ni mbakaji tunalala nae nyumba moja kama sio chumba, lakini hata wapigaji wa wanawake na watoto, tunao, basi iwe rahisi kwa hili.
Kwa mfano…. zipo kesi mbichi za baba mzazi kumbaka mwanawe wa kumzaa, au mjomba kujitoa mshipa wa fahamu kwa mtoto wa dada yake, sasa hata hili twamngojea JPM?
Jawabu isiwe ndio, bali sisi jamii tuvae viatu vya rais wetu Magufuli, kwa kukubali kutoa ushahidi mahakamani, na wala sio kujichukulia sheria mikononi, maana sasa imekuwa kumuua mwanadamu kwa shutuma, ni kama kuchinja kuku kwa ajili ya wageni.
Mwenye macho ya kweli haambiwi tazama, sasa rais Mgufuli akiwaongoza mawaziri, wamekuwa wakiwawajibisha kila mwenye kutumia vibaya madaraka yake, tena bila ya kuangalia sura, sasa iweje mimi na wewe tumezee udhalilishaji?
Kama mwaka 2016, ulishindwa kumtumbua mjomba wako, baba yako, au mama yako na anawafanyia anaowaweza udhalilisaji, basi mwaka huu 2017 tuwatumbue.
Sasa basi, kama tunaimani ya kweli na kiongozi wetu huyu, lazima kila mmoja avae viatu vyake, kwa kukemea udhalilishaji huu tena kwa vitendo, na walio wasugu basi ni kuwatumbua.
Lakini na sisi wanajamii, lazima sasa ule muhali lazima tuuondowe, maana, kama leo amebakwa mtoto wa jirani, kesho au keshokutwa mbakaji atanyemelea mlango wako.
Mimi naamini kila jambo linawezekana, kama sio kupungua basi ni kumaliza kabisa, iwapo tutashirikiana na kufanya kazi zetu, huku tukijua kuwa rushwa na adui wa haki.

Mwanadishi anapatikana- kakahaji2016@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.