Habari za Punde

Rais Dk Shein: Serikali kushirikiana na sekta binafsi kuimarisha viwanda


 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                     5.1.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekifungua kiwanda cha Maziwa  cha “Azam Dairy” na kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyokusudia kuimarisha na kuendeleza viwanda ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Sekta binafsi.

Dk. Shein aliyasema hayo, katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kukizindua rasmi kiwanda hicho kinachomilikiwa na  Bakhressa Group of Campanies” inayoongozwa na Mwenyekiti wake Said Salim Bakhressa, kilichopo Fumba Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 53 ya Mapinduzi ya matukufu ya Zanzibar.

Mapema kabla ya hotuba yake hiyo Dk. Shein alikitembelea kiwanda hicho na kupata maelezo ya kitaalamu kutoka kwa  Meneja Uzalishaji  wa Kampuni ya Azam Dairy Production Limited (ADPL) Adilson Fagundes,

Katika hotuba yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kuendeleza sekta ya viwanda kwa kutambua umuhimu wake katika maendeleo ya Zanzibar sambamba na historia yake katika sekta hiyo pamoja na sekta ya biashara.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za uandaaji wa Sera Mpya za Viwanda itakayozingatia zaidi matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini na kueleza azma ya kuunganisha viwanda na sekta ya utalii.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kueleza historia ya Zanzibar katika sekta ya biashara na viwanda kapla ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 na kueleza kuwa Zanzibar si mwanagenzi katika sekta hizo.

Adha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza azma ya Serikali katika kuanzisha kiwanda cha kusindikizia samaki hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ni visiwa vilivyozunguikwa na bahari hvyo malighafi za kiwanda hicho ni rahisi kupatikana.

Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa mji wa Fumba utafumbuka kutokana na mipango kabambe ya Serikali katika kuliimarisha eneo hilo la uwekezaji kwa upande wa Unguja na Micheweni kwa upande wa Pemba.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya “Bakhressa Group of Campanies” Said Salim Bakhressa kwa nia yake thabiti ya kujenga kiwanda hicho hapa Zanzibar na kuleta maendeleo kwa ajili ya Zanzibar na watu wake sambamba na juhudi zake za kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Sera maalum katika uwekezaji kwa kutoa nafasi kwa kila mmoja mwenye uwezo na fedha aje kuekeza haza Zanzibar huku akieleza umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi ambayo ndio mashine ya uchumi popote pale duniani.

Dk. Shein alisema kuwa kiwanda hicho ni cha kisasa na mitambo yake haipo katika nchi za nyingi za bara hili la Afrkka na hata nje ya bara hili na kusifu hatua hiyo na kusisitiza haja kwa taasisi husika kuwashajiisha wananchi kunywa mazima hapa nchini kwani imegundulika wananchi wa Zanzibar si watumiaji wazuri wa maziwa.

Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa kiwanda hicho kuweka siku moja maalum ya Kitaifa ya kunywa maziwa hatua ambayo itawashajiisha wananchi wa mbali mbali wa Zanzibar kunywa maziwa.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliahidi kutafutiwa ufumbuzi changamoto zote zinazokikabili kiwanda hicho ikiwemo  Sheria za Muungano, utumiaji mdogo wa bidhaa za maziwa kwa wananchi wa Zanzibar, upatikanaji wa malighafi ya maziwa na nyenginezo.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed  alieleza kuwa sekta ya uwekezaji ina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi na ndio maana Rais Dk. Shein amekuwa akilisimamia hilo kwa nguvu zake zote na mafanikio makubwa yanaendelea kupatikana.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Sheikh Bakhressa kwa uzalendo wake wa kuekeza kiwanda hicho kwani serikali itapata mapato kubwa kutokana na kiwanda hicho sambamba na kupanua soko la ajira.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA0 Salum Khamis Nassor alieleza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha na kuendeleza maeneo huru huku akieleza namna Mamlaka yake ilivyoshirikiana na Muwekezaji huyo katika kuanzisha kiwanda hicho.

Mapema Mwakilishi wa Kampuni hiyo Salim Aziz alieleza kuwa kiwanda hicho kina mitambo ya kisasa ya kusindika maziwa ambayo husindika maziwa kwa kuyapitisha katika mfumo maalum wa joto kwa ajili ya kuyahifadhi na kuuwa wadudu ambapo katika kiwanda hicho uwekezaji wa jumla ya Dola milioni 20 umefanyika.

Alisema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kusindika jumla ya lita Laki moja na elfu sitini kwa siku ambapo kiwanda kinaweza kutumia malighafi ya maziwa safi na maziwa ya unga na kuelez changamoto iliyopo ya upatikanaji wa maziwa safi.

Sambamba na hayo alieleza kuwa kiwanda hicho kimetoa ajira za moja kwa moja zipatazo 130 na nyengine nyingi ambazo si za moja kwa moja ambapo maziwa ya kiwanda hicho huuzwa hapa Zanzibar kwa asilimi 10 na Tanzania Bara kwa asilimia 90.

 Mwakilishi huyo pia alieleza changamoto zilizopo zikiwemo upatikanaji wa malighafi ya maziwa ambapo maziwa yanazozalishwa na wakulima wa hapa Zanzibar ni kidogo, Sheria za Muungano, Utumiaji mdogo wa bidhaa za maziwa na gharama kubwa za uendeshaji wa Boiler ambayo hutumia mafuta maalum ambayo hapa nchini hayapo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.