Habari za Punde

Serikali yakusudia kupiga marufuku uchimbaji wa mchanga

Na Mwajuma Juma

SERIKALI ya Zanzibar inakusudia kupiga marufuku uchimbaji wa mchanga hasa katika kisiwa cha Unguja  ili kulinda mazingira kuhifadhi vyanzo vya maji na kudhibiti maaeneo ya kilimo na makaazi ya watu.


Waziri wa Kilimo, Malisili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid amewaambia waandishi wa habari leo kuwa Zanzibar hakuna tena mchanga utakaokidhi mahitaji ya ujenzi hivyo lazima kupunguza kasi ya uchimbaji na matumizi ya mchanga ili kulinda mazingira kuhifadhi vyanzo vya maji na kudhibiti maaeneo ya kilimo na makaazi ya watu.


Aalisema kuwa indhari hiyo imetolewa baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu uwepo wa rasilimali ya mchanga katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

“lazima tuanze kufikiria matumiizi mbadala ya mchanga katika ujenzi ama mbinu za kutumia mchanga kidogo au kutumia rasilimali nyengine badala ya mchanga”alisema Hamad.

Alisema kuwa katika kukabiliana na hali hiyo ni lazima utaratibu wa kutoa vibali kwa uchimbaji na uchukuaji wa mchanga ubadilike kulingana na upungufu uliopo na haja ya kudhibiti matumizi ya rasilimali chache iliyobakia.

Alisema kuwa takwimu zilizofanywa na idara ya misitu na maliasili zisizorejesheka zinaonesha kuwa katika kipidi cha miaka 10 kuanzia 2005 hadi 2015, Unguja ilichimba tani 2,658,503 na Pemba 200,959 za mchanga kutoka katika machimbo rasmi yaliyoainishwa na Serikali.

Alisema kwamba kiwango hicho ni sawa na wastani wa tani 241,682 kwa mwaka kwa Unguja, na tani 18,269 kwa Pemba, ambazo ni sawa na uchimbaji wa wastani wa tani 20,140 kwa mwezi katika kisiwa cha Unguja na tani 1,522 katika kisiwa cha Pemba.

Alisema kuwa hizo ni takwimu halali za uchimbaji mchanga zilizofanywa katika maeneo yaliyo rasmin ambapo jumla ya hekta 522 Unguja na hekta 150 Pemba zilizchimbwa mchanga.

Alisema Zanzibar hivi sasa inaeneo dogo ambaalo ni hekta 14 ambazo hazitoshi kukidhi mahitaji ya mchanga ya miradi mikubwa iliyoidhinishwa na serikali mbali na mahitaji ya wananchi.

Alisema kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haipo tayari kuona kuwa vizazi vijavyo vinaachiwa ardhi yenye mashimo na isiyokuwa na rutuba au isiyofaa kwa matumizi mengine.

Aidha alisema kuna baadhi ya nchi zinaagiza mchanga kutoka nchi za nje ili kuendeleza miji na makaazi ya wananchi wake, hatua ambayo itafanywa pia na Serikali ya Zanzibar katika kukabiliana nayo.

“kuna baadhi ya nchi zimepiga maarufuku kabisa matumizi ya mchanga isipokuwa kwa shughuli maalum sasa wananchi wa Zanzibar imefika wakati wabadilike na waitumie maliasili haba ya mchanga kwa nidhamu ya hali ya juu na kuibakisha pia kwa ajili ya vizazi vijavyo”alisema.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni inaonesha kwamba kwa wastani Unguja inachimba hekta tatu kwa kila mwezi na Pemba inachimba nusu hekta kwa kila mwezi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.