Habari za Punde

Balozi Seif atembelea Hospitali ya Abdallah Mzee, Mkoani Pemba



 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiambatana na Uongozi wa Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani kukagua shughuli za huduma za Afya zinazotolewa katika Hospitali hiyo.

Balozi Seif  akiagiza uwajibikaji uliobora kwa wafanyakazi wa Hospiali ya Abdulla Mzee alipokagua Kitengo cha X RAY.


 Balozi Seif akionyesha kufarajika kwake na huduma  za uchunguzi wa Maabara zinazotolewa na Hospitali ya Abdulla Mzee wakati alipokagua kitengo cha Maabara Hospitalini hapo
 Daktari Mkuu wa Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Dr. Haji Mwita Haji akielezea changamoto wanazopambana nazo watendaji wa Hospitali hiyo wakati wanapotoa huduma za Afya kwa Wananchi.


Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR


Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba  kuangalia huduma za Afya zinazotolewa na watendaji wa Hospitali hiyo.

Daktari Mkuu wa Hospitali ya Abdulla Mzee Dr. Haji Mwita Haji alimueleza Balozi Seif  kwamba mazingira bora ya miundombinu ya Vifaa,


Majengo na watendaji yamepelekea Wananchi wa Kisiwa cha Pemba kuwa kimbilio la kutaka kupata huduma za Afya.
Hata hivyo Dr. Haji Mwita alisema zipo changamoto zinazoikabili


Hospitali hiyo pamoja na Watendaji wake akazitaja baadhi kuwa ni pamoja na umbali wa Makaazi ya watendaji hao jambo ambalo linaleta usumbufu wakati inapoteka uchelewaji wa usafiri.


Dr. Mwita alizitaja changamoto nyengine  kuwa ni uhaba wa Dawa, huduma za umeme wa dharura, ongezeko la wagonjwa pamoja na utaalamu mdogo wa watendaji wake kwa baadhi ya amashine za Kisasa zilizomo ndani ya
Hospitali hiyo na kushairi kuandaliwa mpango maalum wa kupatiwa mafunzo.


Akizungumza na baadhi ya Madaktari na watendaji wa Hospitali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Madaktari na Wauguzi wa Hospitali hiyo wanalazimika kuwajibika ipasavyo ili hadhi ya Hospitali hiyo iendelee kubakia.


Balozi Seif  alisema mfumo huo wa uwajibikaji ulioambatana na vifaa vipya na vya kisasa unaweza kushawishi wagonjwa kutoka nje ya Visiwa vya Zanzibar kutaka kupatiwa huduma za Afya kwenye Hospitali hiyo ya
Abdulla Mzee Mkoani.


Alielezea masikitiko yake kutokana na Hospitali nyingi nchini kulalamikiwa kutokana na huduma zake hawa wakiguswa zaidi Wauguzi kutokana na kauli zao za kuwavunja moyo wagonjwa wanaokwenda kutaka kupatiwa huduma za Afya.


Akizungumzia Makaazi ya Madaktari wa Hospitali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaamua kujenga nyumba Nne za Ghorofa kwa nia ya kuondosha tatizo
hilo.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeshazungumza na Kampuni iliyojenga Hospitali hiyo kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kujenga Nyumba hizo ili kupunguza gharama za kumtafuta mkandarasi mwengine wa
ujenzi huo wakati utakapowadia.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika nasaha zake kwa watendaji hao wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba alisema Serikali isingependa kuona huduma za afya zinazotolewa kwenye Hositali hiyo zinaambatana na ushabiki wa Kisiasa.


Balozi Seif alisema Hospitali ni sehemu ya huduma inayompasa mwananchi ye yote mwenye matatizo ya kiafya anapatiwa huduma zinazostahiki bila ya ubaguzi wala itikadi za kisiasa.

Alionya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamvumilia  mtendaji ye yote wa Sekta ya Afya atakayeonekana ana tabia hiyo ya kushabikia masuala ya Kisiasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.