Habari za Punde

Bandari ya Mkoani kuboreshwa kukidhi viwango vya kimataifa

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kati kati akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma kushoto yake akikagua Bandari ya Mkoani inayokusudiwa kutoa huduma za Kimataifa.
 Balozi Seif  kati kati akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba wakiangalia mandhari ya Bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba akimalizia ziara yake ya siku Tatu Kisiwani Pemba.
Balozi Seif  akitembezwa katika eneo linalotarajiwa kujengwa kwa ajili ya uwekwaji wa makontena pembezoni mwa Bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba.


Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Shirika la Bandari Zanzibar  limejipanga kuimarisha miundombinu yake katika kuona Bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba inatoa huduma zinazokidhi kiwango cha Kimataifa.

Mamlaka ya Mapato Tanzania { TRA } tayari imeshatoa idhini na kutangaza kwamba Bandari ya Mkoani  Pemba inaweza kutoa huduma za Kimataifa ikiwemo shughuli za kupokea na kusafirisha Makontena kutokana na kukuwa kwa biashara katika Kisiwa hicho.


Msaidizi Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Tawi la Pemba Nd. Hamad Salum alieleza hayo wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif alipofanya ziara ya kukagua shughuli za Bandari hiyo akimalizia ziara yake ya siku Tatu Kisiwani Pemba.


 Ndugu Hamad alisema Uongozi wa Shirika la Bandari tayari umeshaanza hatua ya kufanya maboresho ya Baboya, Umeme pamoja na huduma za Maji safi na salama yaliyokwenda sambamba na Ununuzi wa Krini na Kuteremshia Vitu vizito Bandarini.


Alisema hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa Utafiti wa Kitaalamu wa kuiangalia upya Banadari hiyo uliofanywa mwaka 2016  kwa lengo la kuunga mkono maamuzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.


Msaidizi Mkurugenzi huyo wa Shirika la Bandari Tawi la Pemba alimueleza  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Bandari ya Mkoani hivi  sasa inaendelea kupokea Meli za mizigo na Abiria kutoka Unguja na  Mombasa Nchini Kenya.

Alisema kwa sasa Bandari hiyo imeshapokea meli zenye uwezo wa kubeba Tani 200 kutoka Unguja na Makontena 300 yenye ujazo wa Tani 300 kutoka Pemba licha ya kwamba bado wapo baadhi ya Wafanyabiashara  enye kigugumizi cha kuteremsha makontena yao moja kwa moja kutoka nje ya Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma alisema kwa Vile Shirika lake tayari limeshanunua Kreni Moja ya kuteremshia Mizigo, uwezo wa kushusha makontena ya wafanyabiashara katika Bandari ya Mkoani upo na kinachohitajika kwa sasa ni Wafanyabiashara hao kuyaamini mazingira hayo.


Ndugu Abdulla alisema lengo lililowekwa na Uongozi wa Shirika lake ni kuona Mizigo ya Wafanyabiashara kutoka Nje ya Zanzibar inakwenda Pemba moja kwa moja badala ya kupitia kisiwani Unguja na Mombasa Nchini Kenya.


Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema wazo la Uongozi wa Shirika hilo la Bandari kuimarisha Bandari ya Mkoani ni jema na la msingi kwa sababu litasaidia kufungua njia zaidi za Kibiashara kati ya Visiwa vya Zanzibar na Mataifa mengine Duniani.


Balozi Seif alisema shughuli za Bandari ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali Kuu inategemea kuongeza Mapato yake sambamba na kupanuka kwa fursa za ajira zitakazowanufaisha Wananchi Wazalendo hasa Vijana.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Shirika la Bandari na washirika wake vikiwemo vyombo vya Ulinzi kuhakikisha kwamba udhibiti wa uingiaji na utokaji katika maeneo ya Bandari unaimarishwa ipasavyo.

Alisema wapo baadhi ya watu hutumia harakati za wasafiri kuingiza mambo yao ikiwemo usafirishaji wa bidhaa haramu lakini pia uingiaji wa wageni wasiozingatia sheria na utaratibu uliowekwa na Taifa wa Uhamiaji.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.