STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 01.03.2017

RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha
miradi mbali mbali ya maendeleo inayosaidia kukuza uchumi na kuimarisha ustawi
wa jamii hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Ujumbe wa
Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB wanaofanyakazi zao
ndani na nje ya Bara la Afrika, ujumbe ulioongozwa na Bi Lekhethe Mmakgoshi kutoka Afrika Kusini,
anaeiwakilisha Afrika Kusini, Swaziland na Lesotho.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ujio wa viongozi hao wakuu 12 kutoka AfDB kuja
Zanzibar umeonesha wazi jinsi Benki hiyo inavyoithamini Zanzibar na kujali
juhudi zake katika kuimarisha miradi ya maendeleo ili chini ya benki hiyo sambamba
na kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo.
Dk. Shein alisema kuwa
AfDB imeweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo hasa katika sekta ya miundombinu ya
barabara kwa upande wa Unguja na Pemba.
Akieleza juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi na kuimarisha sekta
za maendeleo, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao azma ya Serikali ya kuujenga upya
uwanja wa ndege wa Pemba ili uweze kutoa huduma sawa na uwanja wa ndege wa
Abeid Amani Karume uliopo Unguja na kuongeza kuwa tayari upembuzi yakinifu
umeshafanywa na hivi sasa mchakato katika azma hiyo unaendelea.
Dk. Shein aliongeza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi kubwa katika
kuutengeneza uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume kwa kuzipanua njia za
kurukia na kutulia ndege katika uwanja huo pamoja na ujenzi wa jengo jipya la
abiria katika kiwanja hicho ambapo kumaliza kwake kutaongeza idadi ya watalii
wanaoingia nchini.
Aidha, Dk. Shein
aliipongeza AfDB kwa azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
miradi mengine mipya ya maendeleo sambamba na kuiendeleza ile ya iliyopo hatua
ambayo alisema itazidi kuimarisha uchumi na kukuza sekta nyengine za kijamii na
kimaendeleo.
Dk. Shein aliongeza
kuwa AfDB imesaidia kwa kiasi kikubwa kusaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya juhudi ambazo zimechangia kupunguza
vifo vya akina mama na watoto.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kuueleza ujumbe huo kuwa Zanzibar ni miongoni mwa
nchi za Bara la Afrika zinazopokea watalii wengi kutokana na mazingira na
vivutio mbali mbali vilivyopo.
Hivyo, Dk. Shein
aliwakaribisha viongozi hao kuja kuitembela Zanzibar wakati wa mapumziko yao.
Nao ujumbe huo wa Wakurugenzi Watendaji wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ulimuhakikishia Dk. Shein kuwa Benki hiyo
itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na kupongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Akizungumza kwa niaba
ya ujumbe huo Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB anayeziwakilisha nchi za Afrika ya
Kusini, Lesotho na Swaziland Bi Lekhethe Mmakgoshi alieleza kuwa ujio wao
Zanzibar ni kuja kujionea juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha miradi ya
maendeleo iliyo chini ya Benki hiyo sambamba na kuchukua vipambele vilivyowekwa
katika kuendeleza miradi hiyo.
Aidha, Bi Mmakgoshi
alieleza kuwa ujumbe huo umefarajika kwa kiasi kikubwa na hatua za kuendeleza
miradi ya maendeleo ya Benki hiyo inayotekelezwa hapa Zanzibar na kuahidi azma
ya Benki hiyo ya kuanzisha miradi mengine mipya na kuedneleza ile iliyopo
ambayo inaendelea ikiwemo ile ya barabara.
Sambamba na hayo,
kiongozi huyo wa AfDB alimueleza Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikiwemo Zanzibar imekuwa na utaratibu mzuri katika utekelezaji wa miradi iliyo
chini ya Benki hiyo juhudi ambazo zinafaa kuungwa mkono.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment