Habari za Punde

WANAFUNZI 2,348 WASHINDA KATIKA RUFAA ZAO ZA MIKOPO YA ELIMU YA JUU

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

WANAFUNZI 2,348 WASHINDA KATIKA RUFAA ZAO ZA MIKOPO YA ELIMU YA JUU


1.0         UTANGULIZI

Taratibu za upangaji na utoaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu,zinatoa fursa kwa waombaji ambao ama hawakupata mikopo au wamepata kiwango cha mikopo wanachoona hakikidhi mahitaji, kukata rufaa.  Kwa mujibu wa taratibu zilizopo, waombaji hupewa siku tisini (90) kuanzia mwanzo wa mwaka wa masomo kuwasilisha rufaa zao.  Rufaa hizo huwasilishwa kwa njia ya mtandao na vielelezo/viambatisho huwasilishwa kupitia madawati maalum ya mikopo vyuoni.  Katika mwaka wa masomo 2016/17, zoezi la kupokea rufaa lilianza rasmi tarehe 1 Novemba, 2016 na kuhitimishwa tarehe 31 Januari, 2017.

2.0         MATOKEO YA RUFAA

Katika kipindi cha kati ya tarehe 1 Novemba, 2016 na 31 Januari, 2017 jumla ya rufaa 20,020 ziliwasilishwa kwa njia ya mtandao. Kati ya hizo, jumla ya fomu za rufaa 17,020 zilipokelewa kutoka vyuoni zikiwa na viambatisho muhimu.  Mapitio ya rufaa zilizowasilishwa yalifanywa kwa fomu zote zilizopokelewa na matokeo ya rufaa hizo (zilizoshinda) kwa makundi ni kama ifuatavyo: Walemavu 61; Yatima 57; Wenye mzazi mmoja 570; Familia zenye kipato duni 1,169 na Waliosomeshwa na wahisani 491

3.0         HITIMISHO

Bodi ya Mikopo tayari imetuma vyuoni majina ya wanafunzi walioshinda rufaa zao na inaendelea kukamilisha malipo ya mikopo yao. Aidha, Bodi inapenda kuwataarifu waombaji na umma kwa ujumla kuwa zoezi hili limefungwa rasmi hadi hapo litakapotangazwa tena katika mwaka ujao wa masomo.


Imetolewa na:

MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
28 Februari, 2017.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.