Habari za Punde

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Mabalozi wa Tanzania Nchi za Nje.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiagana na Mabalozi Saba Wapya wa Tanzania walioteuliwa hivi karibu na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwenda kuliwakilisha Taifa katika Nchi mbali mbali Duniani.
Balozi Seif akiwa katika Picha ya pamoja na Mabalozi wapya wanayoiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani mara baada ya kuzungumza nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kushoto ya Balozi Seif waliokaa ni Balozi Pindi Chana anayekwenda Kenya, Balozi Grace Mgwano anakwenda Uganda na upande wa Kulia ya Balozi Seif ni Balozi Matilda Masuka anakwenda Korea Kusini na Balozi Fatma Rajab anakwenda Nchini Qatar.
Waliosimama kutoka Kushoto ni Balozi Silima Kombo Haji anakwenda Nchini Sudan Balozi Joseph Sokoine anakwenda Nchini Belgium na Balozi Abdulla Kilima anakwenda Nchini Oman.
Picha  na - OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR.

Mabalozi wanayoiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mataifa Rafiki Ulimwenguni wataendelea kuwa na jukumu la kuitunza Heshima ya Tanzania katika misingi imara itakayoimarisha Uhusiano mzuri uliopo kati ya pande hizo mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga wakati akiwaaga Mabalozi Saba wapya wa Tanzania walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Nchi katika Mataifa tofauti Duniani uliofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.

Balozi Seif Ali Iddi alisema yapo mafungamano mazuri ya muda mrefu yaliyopo baina ya Tanzania na Nchi Rafiki ambazo Wanadiplomasia hao wa Tanzania  wana kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba uwajibikaji wao unaleta tija na faida kwa mafungamano hayo katika pande zote mbili.

Balozi Seif aliwaeleza Mabalozi hao kwamba Mataifa ya Qatar, Oman, Uganda, Kenya, Belgium na Korea Kusini yamekuwa mshirika mkubwa na Tanzania katika kuimarisha Sekta za Maendeleo zinazosaidia kustawisha maisha ya Wananchi.

Alisema Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inahitaji kuendelea kuungwa mkono na Mashirika na Taasisi za Mataifa hayo ambapo Mabalozi hayo watakuwa na jukumu la kufanya ushawishi utakaopelekea azma hiyo inafanikiwa vyema.

Akigusia Nchi ya Sudan   ambayo Tanzania imeamua kufungua tena Ubalozi wake baada ya kuufunga katika miaka ya 90 kutokana na hali ngumu ya uchumi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtaka Balozi atakayesimamia Ofisi hiyo kufanya juhudi katika kuhakikisha fursa za masomo zilizokuwa zikitolewa na Nchi hiyo zinarejea kama kawaida.

Alisema Sudan ni Nchi iliyokuwa ikiifadhili na kuisaidia sana Tanzania na Zanzibar kwa jumla nafasi nyingi za masomo hasa katika fani za Elimu ya Dini ya Kiislamu na Historia.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Mabalozi wenzake Balozi wa Tanzania Nchini Oman Balozi Abdulla Kilima alisema jukumu walilokabidhiwa na kukubali kulibeba watahakikisha wanalitekeleza kwa nguvu zao zote.

Balozi Kilima kwa niaba ya wenzake wamewaahidi Watanzania kwamba watazingatia kuilinda Heshima iliyopo ya Taifa lao inayoendelea kushamiri katika Nyanja za Kimataifa.

Mabalozi aliyozungumzao nao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kuwaaga ni pamoja na Balozi Pindi Chana anayekwenda Nchini Kenya, Balozi Silima Kombo Haji anayekwenda Sudan na Balozi Joseph Sokoine anayekwenda Nchini Belgium.

Wengine ni Balozi Abdulla Kilima anayeiwakilisha Tanzania Nchini Oman, Balozi Matilda Masuka atakayekwenda fungua Ubalozi Mpya Nchini Korea Kusini, Balozi Grace Mgwano anayekwenda Nchini Uganda na Balozi Fatma Rajab anayekwenda Nchini Qatar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.