Habari za Punde

Baraza la Mji wete kuweka taa za barabarani



NA/ ZUHURA JUMA-- PEMBA

BARAZA la Mji Wete limesema linatarajia kuweka taa za barabarani katika Mji wa Wete, jambo ambalo litasaidia kukuza fursa za kiuchumi kwa wananchi ambazo zitaweza kuwaingizia kipato.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi wa Baraza hilo Philipo Joseph Ntonda, alisema taa hizo zinatarajiwa kuwekwa mara baada ya kukamilika kwa mradi wa Soko, Ofisi na sehemu ya maegesho ya magari (stand), ambapo ziko katika kufanyiwa matengenezo.


Mtonda, alisema  uwekaji wa taa katika mji wa Wete kutasaidia kukuza fursa za kiuchumi kutokana na wananchi kupata nafasi ya kufanya biashara mpaka nyakati za usiku katika maeneo hayo, ambayo kwa sasa ni vigumu kufanya biashara nyakati hizo.


“Wananchi watajiajiri wenyewe kwa kufanya biashara hadi usiku, kwani kuna maeneo mengine ni vigumu kufanya biashara nyakati hizo, hivyo zitakapowekwa taa hizo wataweza kufaidika nazo”, alisema Ntonda.


Mkurugenzi huyo aliutaja mradi utakaoweka taa hizo kuwa ni, mradi wa kuimarisha miji Zanzibar (ZUSP) uliopo chini ya Wizara ya Fedha, ingawa bado hawajapewa gharama za mradi huo.


Alieleza   uwekaji wa taa hizo pia kutasaidia kupungua kwa uhalifu kwa sehemu za mji huo, kutokana na mwangaza utakaokuwepo.


“Mji kadiri unavyokuwa na wahalifu huongezeka na hufanya uhalifu katika maeneo yaliyokuwa yapo giza, hivyo uwepo wa taa hizi zitasaidia sana”, alieleza Mkurugenzi huyo.


 Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi kutoa  ushirikiano wakutosha utakapokuja mradi huo, kwa kuzienzi na kuzilinda, ili kuweza kuwanufaisha katika maisha yao ya kila siku.


Nao wananchi wa Mji wa Wete walisema kuwa, watafaririka sana zitakapowekwa taa katika mji huo,  kwani wataweza kunufaika na kupungua kwa uhalifu kwa baadhi ya maeneo yanayotisha kutembea usiku.


“Kuna maeneo mengine katika mji huu, ifikapo usiku unashindwa kupita kutokana na kukaa vijana wahalifu, jambo ambalo hushindwa kupita mwanamke au mtoto, lakini taa zitatusaidia wahalifu wataondoka kabisa”, walisema wananchi hao.


Aidha walisema kuwa, pia biashara zitakuwa katika mji huo kutokana na kuengezeka kwa maeneo ya kufanyia biashara, jambo ambalo ni faraja kwa wananchi.


Miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kuwekwa taa hizo ni pamoja na kuanzia Ikulu mpaka Limbani, Kizimbani mpaka Ghalani, barabara ya Bopwe, Selemu, Kifumbikai, Kifoi, Kilorodi, Kipangani na Jadida.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.