STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 22.04.2017
JUMLA ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 2.8 zimekusanywa kwa ajili ya
ununuzi wa madawati kwa skuli za Msingi na Sekondari za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar huku ikiwa bado wadau wengine wanaendelea kuhamasishwa kuchangia.
Fedha hizo zimetajwa leo na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika
hafla ya Uhamasishaji na Uchangiaji
Madawati ya Skuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hafla iliyofanyika
katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, mjini Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa fedha
hizo ni Shilingi milioni mia tano (500,000,000) ambazo zimetolewa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika hafla hiyo na Tsh. Bilioni 1.8 za ahadi
zilimetolewa leo ambapo milioni 483 zilishakusanywa hadi mwishoni mwa mwezi wa
Machi mwaka huu.
Mapema Dk. Shein akitoa hotuba yake
katika uzinduzi wa hafla hiyo alisema kuwa suala la elimu ni suala lenye historia
kubwa kwa mwananadamu ambalo linagusa maendeleo yote duniani.
Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa ahadi
za ASP wakati wa kugombea uhuru ni kutoa elimu bure kwa wananchi wote wa Unguja
na Pemba pamoja na sekta nzima ya afya.
Aliongeza kuwa kutangazwa kwa Elimu bila
ya malipo ndio kulikofungua milango kwa watoto wote wa wenyewe uwezo na wasio na
uwezo kupata elimu kutokana na tangazo la mwanzo la elimu bure la tarehe 23.9.1964.
Alisema kuwa jitihada kubwa zimechukuliwa
na Serikali tokea mwaka 1964, licha ya changamoto kuwepo na ndio maana Serikali
imechukua uwamuzi wa kuwaita viongozi wake wote katika hafla hiyo ili na wao waiunge
mkono Serikali yao katika kuchangia madawati.
Alieleza imani yake kuwa hilo litawezekana
kwani hakuna wa kumuachia, kwani Serikali ni wananchi wenyewe na viongozi kazi
yao ni kusimamia tu na kusisitiza kuwa lengo la elimu bure pamoja na Sera yake
iko pake pale, na utekelezaji wake unatofautina na ule wa mwaka 1964 kwa
kutokana na mabadiliko ya mazingira.
“Hatuwezi kuongoza Serikali kwa zao la karafuu
peke yake na ndio maana tumeona haja ya kuongeza mambo mengine ya kuimarisha
uchumi wetu ... baada ya Mapinduzi Zanzibar idadi yetu tulikuwa laki tatu lakini leo tuko milioni moja na laki
nne”alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, alieleza kuwa baada ya Serikali kukwazwa
na mambo mengi ndio hapo iliwaomba wananchi wachangie na hadi kufikia mwaka
2014 katika Sherehe za Mapinduzi alitangaza tena uwamuzi ule ule wa Marehemu Mzee
Abeid Karume kuwa wazee wasichangie tena elimu na jukumu hilo litachukuliwa na
Serikali.
Aliongeza kuwa azma ya Serikali kwa hapo
baadae ni kuhakikisha kuwa Skuli za Sekondari nazo hazitokuwa na michango ya
aina yoyote na kusisitiza kuwa dhana ya Elimu bure ni kuhakikisha mambo yote
yanasimamiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kujenga skuli, vifaa, mishahara,
umeme, maji na mambo yote ya kuendesha skuli ni jukumu la Serikali.
Dk. Shein alimshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuipatia Zanzibar mgao madawati
ikiwa ni mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katikan kukabiliana na tatizo la madawati kwa
skuli za Zanzibar.
Pia, aliwapongeza Wabunge wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wa Majimbo ya Zanzibar kwa kutoa michango ya madawati na
kuyakabidhi katika skuli za majimbo yao, na kuwapongeza Wawakilishi kwa kutoa
michango yao ya fedha kwa madawati ya skuli.
Alizipongeza Wizara za Serikali, Ofisi
zote za Wakuu wa Mikoa, Ubalozi wa Japan pamoja na Mashirika yote ya Serikali na
yasiokuwa ya Serikali huku akieleza azma ya Serikali ya kuanzisha Mfuko Maalum
wa Madawati.
Dk. Shein alieleza kuwa kutoa ni moyo si
utajiri na kusisitiza kuwa umoja ni nguvu na iwapo mshikamano utakuwepo fedha
za kununulia madawati zitapatikana na kuhakikisha kuwa kabla ya Disemba ya
mwaka huu fedha za ununuzi wa madawati zimepatikana na suala hilo litakuwa historia.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kutoa shukurani kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambapo mara tu baada ya uwasilishaji wa
rasimu hiyo Katika Kikao cha Baraza la hilo walianza kutoa michango yao kwa
ajili ya ununuzi wa madawati hayo.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Riziki Pembe Juma, alisema kuwa pamoja na juhudi kubwa ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali kila mwaka na
kwa mwaka 2016/2017 imefikia asilimia 20 ya matumizi ya Serikali, kiwango
ambacho ndio kinachotakiwa kimataifa lakini bado baadhi ya changamoto zipo
ikiwemo uhaba wa madawati.
Aliongeza kuwa hivi sasa Wizara ya Elimu
inatumia Tsh. Milioni 31 kila mwezi kwa gharama za uji kwa skuli za maandalizi,
imenunua madaftari kwa ajili ya skuli za maandalizi na msingi na kueleza kuwa
wazazi hivi sasa hawapaswi kugharamika kununua madaftari kwa matumizi ya watoto
wao wakiwa pia watoto wa maandalizi na msingi wamepewa vitabu.
Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa kuna
uhaba wa madawati 41,871 kwa ajili ya skuli za msingi na viti 43,489 na meza
43,489 kwa ajili ya skuli za Sekondari za Serikali licha ya Serikali kutoa
fedha kila mwaka kupitia kodi ya Bandari lakini kiwango cha fedha
kinachokusanywa hakilingani na ongezeko kubwa la wanafunzi.
Nae Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia,
ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Haroun Ali Suleiman alimueleza Rais Dk. Shein kuwa jambo hilo ni zito
lakini kutokana na mshikamano , litafanikiwa kama yalivyofanikiwa mambo mengi
hapo siku za nyuma.
Alisema kuwa waliohudhuria katika hafla
hiyo ni kutoka Mashirika na Taasisi za
Serikali wakiwemo viongozi wa Serikali na kueleza kuwa washirika wengine na
wafanyabiashara wataalikwa kwa awamu nyengine ijayo na kuahidi kuwa tatizo hilo
watalisimamia na kuhakikisha linakuwa historia kwa skuli za Unguja na Pemba
Waziri Haroun alimpongeza Dk. Shein kwa
kuivalia njuga sekta ya elimu na kupunguza minung’uniko ya wazee kwa watoto wao
kutokana na kuondoa michango na kusema
kuwa hatua hiyo inatekelezwa kutokana na utelekezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
mwaka 2015-2020.
Nao Wakuu wa
Mikoa yote mitano ya Zanzibar walioa taarifa ya mikoa yao inayohusiana na
michango ya fedha zilizopatikanwa na zinazoendelea kupatikanwa kutoka katika
vyanzo mbali mbali vya fedha pamoja na wafanyabiashara, mashirika na taasisi
mbali mbali za Serikali na Binafsi zilizokuwemo katika Mikoa hiyo.
Viongozi hao
walitumia fursa hiyo kutoa michango yao ikiwa ni fedha taslim, ahadi za kutoa
madawati na fedha kwa ajili ya kuchangia madawati kwa skuli zote za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment