Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Azindua Mabalozi wa Usalama wa Barabarani Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akionyesha cheti maalum baada ya kuweka saini yake cha kuthibitisha uzinduzi rasmi wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani Zanzibar { RSA } hapo Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Wa kwanza kutoka kulia ni Naibu Kamishna wa Kikosi cha Usalama Bara barani Tanzania DCP Mohamed  Mpinga, Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud, Waziri wa Ujenzi Balozi Ali Karume 
 Balozi Seif akimkabidhi cheti Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC } Bibi Nasra Mohamed kutokana  mchango mkubwa uliotolewa na vyombo vya habari vya Shirika hilo wa suala la usalama bara barani.
Balozi Seif akikabidhi cheti maalum kwa Mlezi wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani wa Kanda ya Pwani inayounganisha Tanga na Bagamoyo   Bwana Nurdin Ali kutokana na mchango mkubwa wa Taasisi hiyo uliosaidia kupunguza ajali za vyombo vya moto Bara barani Tanzania Bara.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na. Othman Khamis OMPR. 
Matukio ya uvunjifu wa sheria za usalama Barabarani bado yanaendelea kuoteza nguvu kazi  ya Taifa wakiwemo Vijana wazee na watoto huku wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu na wengi kuendelea kuwa mayatima katika maisha yao yote.

Akizindua rasmi Mtandao wa Mabalozi wa wa Usalama Bara barani Zanzibar hapo ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibarf Balozi Seif Ali Iddi alisema hali hiyo imeendelea pia kuleta hasara kwa Taifa kutokana na kuharibiwa kwa miundombinu  ya Bara bara na vifaa vyengine.

Balozi Seif alisema ajali za bara barani bado zimekuwa ni tishio kwa maisha ya wannchi kutokana na baadhi ya madereva ama kwa makusudi kutotii  sheria na taratibu zilizowekwa katika kufuata matumizi sahihi yaliyowekwa bara barani.

Alisema baadhi ya madereva hao wamekuwa na tabia ya kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo wa kasi bila ya kujali watumiaji wengine  mbali mbali kama watoto ambao nao wana haki ya matumizi ya bara  bara hizo.

Balozi Seif  alionyesha masikitiko yake kutokana na baadhi ya madereva husababisha ajali za kizembe kutokana na ustaarabu wa kisasa ulioingiza wa kuendesha chombo cha moto na huku wanazunguza na simu wakati mataifa mengine Duniani hili wanalihesabu kuwa kosa kubwa bara barani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uamuzi wa kuanzishwa kwa dhana hii ya mabalozi wa usalama Bara barani  hapa Zanzibar ni wa busara  na kuwa wakati muwafaka ambapo Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada za kukabiliana na ajali za bara barani.

Akizungumzia upande wa gari za Dala dala Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kipo kilio kikubwa cha abiria kutokana na vitendo vya madereva na makonda  vya kutowafikisha katika vituo vyao walivyopangiwa.

Alisema mambo hayo yanawasumbua abiria hasa wale wenye mahitaji maalum walemavu ambayo yanakwenda kinyume na sheria za usalama bara barani pamoja na kanuni zake.

Balozi Seif alieleza kwa kutumia utaratibu wa Mabalozi wa Usalama Bara barani wakati umefika wa kukabiliana na matukio  kwa kuwapa Taarifa kwa wakati na kuchukuliwa hatua dhidi ya watu wote wanaohusika kuvunja sheria za Nchi.

Jeshi la Polisi usalama Bara barani pamoja na mamlaka nyengine ni vyema likashirikiana kwa karibu na Mabalozi wa Usalama Bara barani kwa kusimamia vyema dhana hii kwa kutumia mikakati tofauti itakayowanasa wapinda sheria za usalama bara barani.

Alisema kupaza sauti, kukemea pamoja na kuchukuwa hatua nyengine kwa wale madereva watukutu kutasaidia kuondoa udumbufu na kero zinazotokana na tabia hiyo mbaya ndani ya Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alilinasihi jeshi la Polisi kujenga utamaduni wa  kuficha siri kwani ni dhambi kubwa iwapo taarifa za uvunjaji wa sheria bara barani zinazotolewa na Mabalozi  kwa jeshi kutolewa kwa wavunja wa sheria  hizo.

Balozi Seif alifafanua kwamba huo ni usaliti wa wazi na kamwe hautokubalika kwa sababu ni adui wa maendeleo.

Mapema akitoa Tarifa Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani Nd. Justafa Mussa  alisema Mtando huo wa Kiraia umeanzishwa kwa lengo la kulisaidia Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama bara barani kupambana na na makosa yanayotokana na bara bara.

Nd. Mustafa alisema dhana hiyo ya Mabalozi wa usalama bara barani inafaa kuungwa mkono ya washirika  mbali mbali  huku wakielewa kwamba jukumu la kulinda usalama wa raia linamuhusu na kumgusa kikla mwana Jamii.

Alisema wanajumiya hao tayari wameshaanza kutoka mafunzo kwa wanafunzi katika maskuli mbali mbali nchini sambamba na kuwataka wana jamii kutowaonea haya madereva na makonda wajeuri.

Naye Mlezi wa Mabalozi wa usalama Bara barani Msaidizi Kamishna wa Jeshi la Polisi { ACP } Mkadam  Khamis Mkadam alisema ajali nyingi zinazotokea  Bara barani kutokana na vitendo visivyotii usalama bara barani.

ACP Mkadam alisema kikosi cha usalama Bara bara kimekuwa kikibuni mbinu mbali mbali za kusimamia usalama sambamba na kupunguza ajali kwa kiwqango kikubwa kadri inavyowezekana.

Alisema ajali za bara barani zilizotokeza mwaka 2016 zilifikia mia 604 na kusababisha vifo vya watu 147 wakati mwaka 2017 uliripotiwa ajali mia 517 zilizosababisha vifo vya watu 133 kukiwa na upungufu wa vifa vya watu 14.

Uzinduzi wa Mtandao wa Mabalozi wa Usalama Bara barani Zanzibar  ulioambatana na michezo ya kuigiza yenye mnasaba na tukio hilo umeshuhudiwa na wanamtandao wa Mabalozi wa usalama Bara barani kutoka Tanzania Bara wakiongozwa na Naibu Kamishna wa Usalama Bara barani Tanzania ACP Mohamed Mhina.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.