Habari za Punde

Ahadi ya Dk Shein ya mshahara, wafanyakazi waifurahia


 Na Haji Nassor, Pemba

MACHI 24 mwaka jana, Jaji mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, kwa mamlaka aliyonayo kikatiba, alimuapisha rais mteule wa Zanzibar dk: Ali Mohamed Shein, kwenye uwanja wa Amani mjini Unguja.

Sherehe si haba zilinoga, na kubahatika kuhudhuriwa na pia na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dk: John Pombe Mgufuli, makamu wake Samia Suluh Hassa, pamoja na viongozi kadhaa samba mba na mabalozi.

Kama siokufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika awali Oktoba 25 mwaka jana, na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, Jecha Salim Jecha, basi rais ambae engeshinda, angekuwa amaeshatimiza mwaka mmoja na miezi mitano sasa, ndani ya Ikulu ya Zanzibar.

Baada ya kufutwa kwa matokeo hayo, na kuitishwa tena uchaguzi, uliopewa jina la uchaguzi mkuu wa marudio, ambao uligomewa na baadhi ya vyama kikiwemo cha kikuu cha upinzani CUF, ulimpa ushindi mnono mgombea wa CCM.

Ndio huyo dk Shein, ambae aliibuka na ushindi mpana wa asilimia 91.4 na kuwaacha masafa washindani wenzake wengine 13 ambao walikuba kushiriki uchgauzi huo.

Kuapishwa Machi 24 mwaka jana kwa rais huyo mteule, ni ishara kwamba anaingia Ikulu ya Zanzibar kwa kipindi chake cha pili na cha mwisho cha miaka mitano mengine, baada ya kubisha hodi kwa mara ya kwanza Novemba mwa 2010.

Bila shaka sasa, kazi ya kuiongoza nchi ndio inaendelea na hasa, baada ya kupanga na kupangua baraza la mawaziri ni utekelezaji wa ahadi.

Si unajua kuwa, kabla ya kuingia kwenye mchakato wa kupiga kura, alipita majimbo yote 54 ya Zanzibar na kutangaaza sera zake makini, mipango, mikakati na nini atafanya pindi akirejea Ikulu.

Pamoja na chama CCM kutawala tokea mwaka 1977, kabla ya ASP Tanzania bara na Visiwani, ilikuwa kazi rahisi ya kuwashawishi wananchi, ili wakiunge mkono, si unajua imeshafanya mengi.

Na sasa dk Shein yuko ndani ya Ikulu ya Zanzibar, akiamini kuwa kuweko huko, ni kutokana na kutangaaza vyema sera zake na kisha wananchi kuwaminia kura kwa ahadi zake.

Sasa wafanyakazi wa SMZ, wanakumbuka wakati dk Shein akiwa kisiwani Pemba, kwenye uwanja wa Gombani ya kale, kwamba aliwaahidi kupandisha mishahara juu.

Aliwaahidi wafanyakazi hao, akipata ridhaa ya kuongoza tena Serikali kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, atahakikisha ndani ya mwaka mmoja wa kwanza, anaboresha mishahara ya wafanya kazi kwa kima cha chini, kuanzia na shilingi laki tatu (300,000).

Naamini, wapo waliovutiwa na ahadi hiyo, na ndio maana leo hii, wanajisifu kwamba wameshamuweka Ikulu dk Shein, wakiamini kwa uungwana wake, atatimizi hilo ndani ya mwaka mmoja wa kwanza.

Kwa hesabu za darasa la saba, tokea rais huyo ale kiapo ‘oath’ Machi 24 mwaka jana, sasa ameshatimiza mwaka mmoja, na pengine mwezi mmoja hivi, ambapo naamini ndani ya kipindi hicho wafanyakazi watakuwa tayari wanasaini shilingi laki tatu.

Naamini dk Shein ambae anamaliza muhula wake wa pili kuiongoza Zanzibar, kilio cha wafanyakazi, wakiwemo wa Ikulu anayoiongoza kitanyamaza walau kidogo, maana sasa mwezi huu wa April ndio wanasaini kima alichokiahidi.

Dk Shein kama kiongozi wa nchi kwake ni mwiko kutoa ahadi kisha asiitekeleze, maana wapo kwa sasa wanaoshuhudia ujenzi wa miundombini ya barabara na maji safi na salama kwenye maeneo yao.

Hapa leo sitaki niwataje wazee wale waliofikia umri wa miaka 70, ambao kila mmoja kwa kituo chake, anaramba shilingi 20,000 nayo hiyo ni ahadi ya dk Shein.

Nikutajie nyengine, kupandisha bei ya zao la karafuu shilingi 14,000 ambapo sasa wakulima ile asilimia 80 inabaki kwao, na asilimia 20 ndio inayoingia serikali.

Sasa na hili la mishahara wala kwake sio jambo kubwa, maana amaeshafunua ukurasa wa mapato ya serikali, na sasa mwezi huu wa April ndio wafanyakazi watachekelea shilingi 300,000.

Umakini wake, wa chama chake na watendaji wanaomsaidia kazi ndio, leo hii amekuwa gwiji wa kuahidi na kisha kutekeleza ahadi zake taratibu.  

Mkame Haji Juma, yeye ni mfayakazi kwenye taasisi ya mifugo, anasema hajaamini sana, kwamba ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, kima cha chini cha mshahara kitakua shilingi 300,000.

“Unajua ahadi za kuongezea huwa zipo kila muda, sasa kama Dk Shein ameshaapishwa na kuingia Ikulu rasmi, twangonjea kwa hamu fedha hizo mwezi huu’’,anasema kwa furaha.

Lakini mfanyakazi wa wizara ya elimu Pemba, Maryam Haji Mohamed anasema, hakuna sababu kwa Dk: Shein kulichelewsha hilo, maana aliliahidi kwa kinywa kipana.

Hashim Mmanga Muhunzi, ambae nae kwa sasa anapokea shilingi 150,000 ambao ndio kiwango cha chini cha mashahara wa SMZ, anaamini rais hilo atalitekeleza.

Yeye anasema kwa sasa chakula kimepanda bei na kufikia wastani wa shilingi 55,000 hadi shilingi 58,000 kwa kipolo kimoja cha mchele chenye ujazo wa kilo 50.

“Ukishanuanua mchele, sabuni ambayo kilo moja ni shilingi 2000, sukari ambayo kilo ni shilingi 2000, hapo hujatokezea kuumwa katikati ya mwezi, wala hujaangalia dagaa, basi unajikuta mshahara hautoshi’’, alilalamika.

Hata bibi Asha Omar Makame wa Halmashauri, alisema wafanyakazi waliowengi, wamekosa hamasa ya kazi kutokana na maisha kupanda na kisha mshahara kuwa mdogo.

“Kama rais wetu mteule akitekeleza ahadi yake ndani ya mwezi huu kama alivyoahidi kwenye kampeni yake, basi kidogo nidhamu ya kazi itakuwepo”,anafikiria.

Ussi Salim Khamis ‘babu’, yeye anasema wakati serikali inayoongozwa na Dk Shein,  ikitaka kutimiza ahadi yake hiyo, lazima iwe karibu mno na wafanyabiashara maana wamekuwa na tabia kupandisha bei za bidhaa.

“Mwaka mmoja wakati SMZ, baada ya kuongezea asilimia 25 kwa wafayakazi, kila mfanyabiashara alipandisha bei za bidhaa na hawakuulizwa, sasa na mwaka huu, uangalifu unahitajika’’, alishauri. 

Walishasema wahenga kuwa haba na haba hujaza kibaba, na bandu bandu huusha gogo, hata kama fedha haitoshi, lakini wafanyakazi wanaamini kama kiwango kikiwa kama kilichoahidwa, kibaba kitajaa.

Wazee wa kijiji cha Micheweni Pemba, kila siku husema hakuna kupata kidogo, wala apewaye hawi sawa na arambishwaye, maana kupewa unaongeza.

Wafanyakazi wa SMZ kupitia shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar ZATUC, na Katibu Mkuu wao Khamis Mwinyi Mohamed, wamekuwa wakilalamikia kila uchao, maslahi bora kwa wafanyakazi.

Hazipiti sherehe za siku ya wafanyakazi ‘Mei day’ bila ya ZATUC kuililia serikali kutaka kuwanawirishia maslahi mazuri wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na vitendea kazi.

Kama Dk Shein atatekeleza ahadi yake hiyo, itakuwa hii ni mara ya pili katika kipindi kifupi, kwa serikali kupandisha mishahara ya wafanyakazi, ambapo awali ilipandisha kwa asilimi 25, ambapo wakati huo walikuwa wakipokea shilingi 100,000

Hapo ulifikia shilingi 125,000 na kisha kujivuta tena hadi shilingi 150,000, ambapo kama ndani ya mwezi huu dk Shein, atatekeleza tena ahadi yake, itakuwa ni kwa asilimia mia moja, na kufikia shilingi 300,000.

Marekebish yaliofanywa na SMZ ni yale mwanzoni mwa wa mwaka 2011, pia mwishoni mwa mwaka 2013 na mwanazoni mwa mwaka 2014, ambapo ilipandisha kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 125,000 hadi shilingi 150,000 sawa na asilimia ishirini (20).

Lakini SMZ imekuwa haiangalii tu kupandisha mishahara kwa wafanyakazi, bali hata kuimarisha utendaji wa kazi kwa kuwapatia vifaa vya kazi, mafunzo, afya na usalama, kutunga sera, sheria na kanuni za utumishi bora pamoja na kukuza ushirikiano na Shirikisho la Vyama huru vya wafanayakazi.

Yote kwa yote wafanyakazi wa SMZ sasa wanakaa vinywa wazi wakisubiri ahadi ya dk Shein, ya kupandisha mshahara wa shilingi 300,000  ndani ya mwezi huu kutoka shilingi 150,000 wa sasa hadi shilingi 300,000.

Wakati akitoa ahadi hiyo, alisindikiza na maneno kwamba, lazima nao uwajibikaji kwenye sehemu za kazi kwa wafanyakazi uimarike, ili wananchi wapate huduma kwa wakati wanapofika kwenye sekta za umma.   


Kiwango hicho cha fedha, ambacho atakiongeza kwenye mishahara kinawezekana ikiwa uchumi wa Zanzibar nao utakuwa na kuongezeka,  kwani Serikali anayoiongoza imepiga hatuwa katika ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 4.5 hadi kufikia asilimia 7.2 kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.