Habari za Punde

Balozi Seif awasilisha Muelekeo wa Tanzania katika uimarishaji wa Sekta ya Utaliikwenye Jukaa la dunia la uchumi


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tamasha la Uchumi la Dunia linalofanyika Mjini Amman Nchini Jordan akimuwakilisha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis OMPR.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga uwezo zaidi wa kukabiliana na vitendo vya  rushwa katika azma yake ya kujenga uchumi imara utakaostawisha Taifa kwa kuongeza Mapato kupitia Sekta ya Utalii sambamba na Ujenzi wa Viwanda vipya vya kudumu.


Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anayemuwakilisha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwenye Jukwaa la Dunia la Uchumi {World Economy Forum } wakati akiwasilisha Muelekeo wa Tanzania katika uimarishaji wa Sekta ya Utalii hapo katika Ukumbi wa Mfamle Hassan Bin Talal pembezoni mwa Bahari Nyeusi Mjini Amman Nchini Jordan.



Balozi Seif alisema zipo jitihada za ziada zilizochukuliwa katika ujenzi wa miundombinu ndani ya Sekta ya Utalii kutokana na Rasilmali nyingi zilizopo ikiwemo Mbuga za Wanyama, Ardhi yenye Rutba, Fukwe za kuvutia pamoja na Mlima wa Pili kwa urefu Duniani Kilimanjaro zilizoifanya Tanzania kujikita zaidi katika uimarishaji wa Seklta hiyo.



Alisema Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikichukuwa juhudi mbali mbali kwa kushirikiana na Sekta na Taasisi Binafsi kuendeleza Viwanda na soko la Biashara ya Utalii lenye muelekeo mkubwa wa kutoa ajira hasa kwa Vijana wanaomaliza masomo yao ya Sekondari na Vyuo Vikuu.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza washiriki wa Warsha hiyo ya mambo ya Utalii ndani ya Jukwaa la Dunia la Uchumi Mjini Amman Jordan kwamba Tanzania tayari imeimarika katika kukabiliana na matukio
ya Kigaidi ili kutoa nafasi kwa Wawekezaji wa Kimataifa kutumia fursa zilizopo Tanzania katika kuwekeza miradi yao hasa ile ya Utalii.



Alieleza kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa inaendelea kuwa kisiwa cha Amani ndani ya Mwambao wa Afrika Mashariki na Ukanda wa Kusini ya Afrika ya Jangwa la Sahara kutokana na ushiriki wake
uliojaa nidhamu katika ulinzi wa maeneo hayo.


Alisema kutoka na hali hiyo ya amani na utulivu  iliyopo Nchini Tanzania Makusanyo ya mapato kupitia  sekta ya Utalii yanakadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 1.6 licha ya kukumbwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia Nchi pamoja na kutumia Teknolojia ya Habari katika kuutangaza Utalii nje ya Nchi.



Akifafanua Sekta ya Utalii kwa upande wa Visiwa vya Zanzibar Balozi Seif  alisema Sekta hiyo ambayo kwa sasa imechukuwa nafasi ya Tatu katika Uchumi wa Dunia imekuwa tegemeo kubwa la Uchumi wa Zanzibar.


Balozi Seif alifahamisha kwamba tokea kuimarishwa kwa fursa za Uwekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar mwanzoni mwa Miaka ya 80 zipo fursa nyingi za ajira zinazokadiriwa kufikia Laki 376,000 rasmi na zile zisizo rasmi na kuleta faraja kwa Wananchi walio wengi.


Alisema Lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ni kufikia fursa za ajira zipatazo Laki 500,000 hadi ifikapo mwaka 2020.



Balozi Seif alieleza bila ya shaka kwamba Utalii kwa sasa imekuwa Sekta muhimu katika ukuaji wa Uchumi Kidunia uliopanda na kufikia kiwango cha asilimia 9% kinachokisiwa kugharimu Dola za Kimarekani Trilioni 1.3 katika bidhaa zinazosafirishwa kutokana na Sekta hiyo.



Alisema rikodi ya Bara la Afrika ya Watalii Milioni 14.8 ndani ya Mwaka 2000 imeongezeka hadi kufikia Milioni 68 kwa Mwaka 2015 ikifikia asilimia 62% ya idadi ya wageni wa nje wanaoingia Bara  hilo walioibua ajira zipatazo 25,000,000 sawa na asilimia 7.1% ya ajira zilizoibuka ndani ya Bara hilo.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliipongeza Jordan chini ya Kiongozi wake Mfalme Abdulla wa Pili kwa uamuzi wake wa kuwa mwenyeji wa Mkutano huo wa Jukwaa la Dunia la Uchumi .



Jordan imekuwa  mwenyeji wa Jukwaa la Dunia la Uchumi { World Economy Forum } kwa takriban mara Tisa sasa na 16 kwa Kanda na Mashariki ya Kati ya Kaskazini mwa Afrika Jukwaa la Uchumi la Dunia { World Economy Fforum - WCF} limeasisiwa Mwaka 1971 chini ya Muanzilishi na Mwenyekiti wake  Profesa Klaus Schwab huko Davos, Switzerland  likilenga kusaidia kuepuka vita sambamba na kupunguza wimbi la Wakimbizi katika eneo la Mashariki na
Kati na Kaskazini ya Bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.