Habari za Punde

Wanaushirika wahitaji elimu zaidi juu ya vikundi vya Saccos

HABIBA ZARALI, PEMBA.

WANAUSHIRIKA wa vikundi mbalimbali vya Saccos Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba, wamesema katika kuhakikisha Saccos za wilaya zinafanikiwa ni vyema taasisi husika wakatowa elimu ya kutosha kwa wanavikundi na wananchi kuhusiana na uanzishwaji huo.

Walisema iwapo hatuwa ya haraka ya kutoa elimu kupitia vikundi hivo sambamba na kuvitumia vyombo vya habari kutachangia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wananchi kuelimika .

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wanasacos hao ,walisema ingawa tayari wameshanza kupata elimu lakini bado hawajafahamu lengo la la ujio wa Saccos hiyo na hawajafahamu saccos za kawaida zitakuwa katika hali gani baada ya kuja kwa saccos za Wilaya.

Katibu wa “CHOKOCHO SACCOS” Mohammed Issa Mohammed, alisema wazo la kuja kwa Saccos za Wilaya ni zuri na linaweza kuwasaidia lakini bado wanahitaji elimu zaidi ya kujuwa  saccos za kawaida zitakuwa na hali gani hasa  ukizingatia zinatoa huduma kwa wananchi wake.

“Hadi sasa wananchi hawajakataa kujiunga na Saccos ya Wilaya baada ya kuanzishwa lakini wanalohitaji ni kufahamu saccos zao za kawaida zitakuwa   katika hali gani”alisema.

Alisema iwapo itatolewa elimu kupitia vipindi mbali mbali  wananchi watajuwa masharti ya kujiunga kwa vile kuna baadhi ya Saccos zao kwenye masuala ya mikopo hakuna riba.

Mjumbe wa Saccos hiyo,  Juma Khamis Kombo, alisema uanzishwaji wa saccos za Wilaya ni vyema ukaangalia zaidi umuhimu wa saccos za kawaida kwani zinawasaidia sana na endapo zitavunjwa na kupelekwa sehemu nyengine itakuwa bado lengo lao halijafikiwa.

“Katika Saccos zetu tunajiendesha vizuri na tunajisaidia vyema kupitia mikopo na hali zetu za maisha zinaimarika”alisema.

Mshika fedha wa kikundi hicho, Fatma Chum Omar, alisema ili uanzishwaji huo uweze kufanikiwa ni lazima kuwe na umoja kati ya wanasaccos wa kawaida na taasisi husika inayoshughulikia saccos hizo .

Hivyo alisema ni vyema wanasaccos mbali mbali kutowa elimu ndani ya vikundi vyao pamoja na kwa wanajamii ili uanzishwaji huo uweze kufanikiwa kama ulivyopangwa.
                          No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.