Habari za Punde

Mamlaka za Serikali za Mitaa Zizingatie Sheria Katika Ununuzi wa Huduma Kwa Umma.


Na Ismail Ngayonga. Maelezo Dar es Salaam.
KATIKA  kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2015/16,  Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ilifanya ukaguzi wa manunuzi ya umma na uhakiki wa ukaguzi uliofanyika Mwaka wa Fedha 2014/15.

Ukaguzi huo ulilenga kuangalia iwapo mikataba ya manunuzi iliyoingiwa katika kipindi husika ilitekelezwa au inatekelezwa kwa mujibu wa vigezo na masharti yaliyoainishwa kwenye mikataba husika inalingana na thamani ya fedha za umma zilizotumika. 

Katika ukaguzi wa uhakiki wa mwaka 2014/15, jumla ya ya taasisi nunuzi 70 zilifanyiwa ukaguzi wa ukidhi uliongalia namna taasisi hizo zilivyozingatia sheria na kanuni za manunuzi pamoja na matumizi ya nyaraka za miongozo na mifumo iliyoandaliwa na PPRA. 

Taasisi zilizoguswa na ukaguzi huo uliofanyika kati ya mwezi Aprili na Septemba, 2016 ni pamoja na taasisi 15 zilizo kwenye kundi la Wizara, Idara na Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa 25; na mashirika ya umma 30.

Jumla ya mikataba 21,313 ya manunuzi yenye thamani ya Tsh Trilioni 1.05 ilifanyiwa ukaguzi huo, ambapo kati yao mikataba 118 yenye thamani ya Tsh. Bilioni 55.34 ilikaguliwa katika halmashauri za serikali za mitaa.

Aidha taarifa hiyo inaongeza kuwa katika mikataba 122 ya ukusanyaji wa mapato iliyokaguliwa katika Malmaka tisa za Serikali za Mitaa, kumebainika mapungufu kadhaa katika usimamizi wa mikataba hiyo ambapo kumesababisha halmashauri hizo kushindwa kukusanya kiasi cha shilingi 761.54 milioni.

Inaelezwa kuwa pamoja na hasara hiyo, ukaguzi unaonesha kuwa halmashauri hizo hazikuchukua hatua zozote dhidi ya wazabuni waliopewa jukumu hilo kwa mujibu wa mikataba waliyoiingia.

Katika kutekeleza sera ya ugatuaji (upelekaji) wa madaraka kwa wananchi, Serikali iliamua kuwa na programu za maboresho ya Serikali za Mitaa zinazolenga kuongeza ufanisi kwa Watendaji ili waweze kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi likiwemo suala la ununuzi wa vifaa, kandarasi za ujenzi na huduma mbalimbali.

Chini ya Sera ya Serikali ya ugatuaji wa madaraka, rasimali fedha zinaelekezwa moja kwa moja katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo sehemu kubwa ya matumizi yake huelekezwa katika masuala ya manunuzi.

Miongoni mwa Miradi inayotekelezwa kupitia programu hizo ni Mradi wa Kujengea Uwezo Serikali za Mitaa kwenye Ununuzi wa Umma (MKUSEMU) ulioanza kutekelezwa kuanzia mwezi Juni 2012 na kukamilika Desemba 2017.

Aidha mradi huo umelenga kuwajengea uwezo maafisa watendaji wa Kijiji au Mtaa kuelewa masuala muhimu yanayohusu usimamizi wa fedha kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa namba 9 ya Mwaka 1982; na Sheria ya Ununuzi Namba 21 ya Mwaka 2004 pamoja na kanuni za Ununuzi za Serikali za Mitaa za Mwaka 2007.

Wadau wakuu wa mradi huo ni Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ikishirikiana na Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kikiwemo chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo). 

Mikoa iliyopo katika mradi huo na halmashauri zake katika mabano ni pamoja na Dodoma (Kondoa na Kongwa), Iringa (Kilolo na Mufindi), Tanga (Lushoto na Muheza);, Kigoma (Kasulu na Kigoma vijijini), na Pwani (Mkuranga).

Katika utafiti wa awali uliofanyika katika miradi ya maendeleo ya mikoa hiyo na vituo vya kutolea huduma ya ununuzi (shule, ujenzi wa madarasa, hospitali) ilibainika kuwa taratibu zinatofautiana kati Halmashauri moja na nyingine, Kata moja na nyingine, hali kadhalika kati ya Kijiji kimoja na kingine.

Uanzishaji wa mradi huo umekuja kufuatia mapungufu yaliyopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweza kufanya ununuzi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.

Katika kaguzi mbalimbali zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG)  na PPRA imeonesha kiwango cha uelewa wa taratibu za ununuzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni mdogo hususan kwenye kuandaa na kutekeleza mpango wa ununuzi wa mwaka, kuendesha michakato ya zabuni, utunzaji wa kumbukumbu.

Kuwepo mradi huo, kutawezesha kuwepo ufanisi katika Ununuzi wa umma, na hivyo kuiwezesha jamii kupata taarifa za ununuzi na kuweza kuzifuatilia na kutoa taarifa ya  kuhusu utekelezaji wa mikataba, kuimarisha mfumo wa kusimamia na kuhakikisha ubora wa manunuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.