Habari za Punde

Ofisi ya Afya Wilaya ya Mjini Unguja Ikishirikiana na Madaktari Bingwa Kutoka China Wakitoa Huduma Katika Siku ya Afya ya Kijiji

Daktari Bingwa kutoka Nchini Jamhuri ya Watu wa China Dk.Gao, akitowa huduma ya kumpima mmoja wa mwananchi waliojitokeza katika zoezi la huduma ya Afya ya Kijiji akimpima kifua mtoto Salma Mohammed mkaazi wa Kilimahewa Wilaya ya Mjini Unguja katika siku ya Afya ya Kijiji iliyofanyika katika madarasa ya Skuli ya Kwamtipura Wilaya ya Mjini Unguja.
Daktari bingwa wa pua na masikio kutoka China Dk. Fei Jie, akimfanyia uchunguzi wa pua Bi. Amina Himid katika siku ya Afya ya kijiji iliyofanyika Skuli ya Kwamtipura.
Afisa Afya akimpatia dawa mmoja wa wagojwa waliofika kupata huduma katika siku ya afya ya kijiji huko Skuli ya Kwamtipura Wilaya ya Mjini. 
Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mjini Unguja waliojitokeza kupima Afya zao zilizotolewa na Madaktari wa Kichini katika viwanja vya Skuli ya Kwamtipura Unguja 



Na Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar.
Mkurugenzi wa Kinga na elimu ya afya Dk. Fadhil Mohammed Abdalla, amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya zao.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kwani humuwezesha mtu kubaini mapema iwapo amepata maradhi na hivyo kutibiwa kabla athari haijwa kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo wakati wa kutolewa huduma za afya katika shehia ya Kilimahewa Bondeni kutoka kwa madaktari bingwa wa China, amesema kuwa ni vyema kunapotokea fursa ya huduma bila malipo, wananchi wazichangamkie ipasavyo.

Dk. Fadhil alisema serikali imekuwa ikichukua juhudi kubwa kuwafikishia wananchi huduma za afya karibu na maeneo yao wanakoishi.

“Huduma hii adhimu na ni muhimu kwa kujua afya yako na baada ya kupata vipimo unapata matibabu na wengine hushauriwa wafike hospitali ya Mnazi mmoja kwa kupata matibabu zaidi.” Alisema mkurugenzi huyo.

Dk. Fadhil amesema lengo la huduma hizo ni kuwashajiisha wananchi waweze kuelewa maradhi waliyonayo na kuwezesha kupatiwa matibabu.

Aidha alieleza kuwa, madaktari hao hutoa elimu ya afya kuhisiana na maradhi ya kuambukiza hasa katika kipindi hichi cha mvua.  

Nae daktari dhamana wa wilaya ya mjini Ramadhani Mikidadi Suleiman, amesema zoezi la kupima afya ni muhimu na wataalamu wa kutosha wapo hivyo wananchi wasipuuze kujitokeza.

Katika uchunguzi uliofanya kweny zoezi hilo, Dk. Mikidadi alisema wananchi wengi wamegundulika na matatizo ya macho, meno, koo, kisukari na shinikizo la damu na kupatiwa matibabu.

Amewahimiza wananchi kutodharau zoezi hilo litakalokuwa linafanyika kila baada ya miezi mitatu.

Naye sheha wa shehia ya Kwamtipura Hassan Hashir Hassan, ameeleza kufurahika kwake kutokana na wananchi wengi kuitikia wito na kujitokeza katika zoezi hilo lililofanyika bila ya malipo.

Maradhi mengine yaliyogunduliwa kutokana na uchunguzi ni tezi dume, maradhi ya mama na mtoto pamoja na kuchukuliwa vipimo vya maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Wananchi mbalimbali wameipongeza serikali kwa kuwafikishia huduma hizo katika maeneo  yao, wakisema imesaidia kuwapunguzia usumbufu na gharama za kwenda mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.