STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 14.05.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amehuzunishwa kwa kiasi kikubwa na maafa
yaliotokezea Unguja na Pemba kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na kuwaahidi
wananchi kuwa Serikali yao itahakikisha inawapa misaada inayohitajika pamoja na
kuzifanyia kazi athari zilizotokea zikiwemo uharibifu wa miundombinu ya
barabara.
Dk.
Shein aliyasema hayo leo katika ziara yake aliyoifanya katika maeneo mbali
mbali ya Unguja yaliyoathirika na mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha ambazo
zimepelekea baadhi ya wananchi kukosa makaazi baada ya nyumba zao kubomoka,
kuharibika kwa miundombinu ya barabara, madaraja pamoja na kuharibika kwa mazao.
Miongoni mwa maeneo aliyoyatembelea katika ziara yake
hiyo ni eneo linalotuama maji Mwanakwereke, kuangalia mafanikio ya ujenzi wa
mtaro mkubwa wa kupitishia maji kupitia Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP)
huko Karakana, Bumbwisudi kwa Goa, Mwera Gudini, Fuoni Kibonde Mzungu, Daraja la Mwanakwerekwe Nyumba Mbili ambapo
katika Mkoa huo wa Mjini Magharibi nyumba zilizoathirika ni 1,130.
Katika
ziara yake hiyo ambayo viongozi mbali mbali walishiriki, Dk. Shein pia, alipewa
taarifa mbali mbali kutokana na athari za mvua hizo za masika kutoka kwa
viongozi husika ambao pia, walieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa sambamba
na azma ya Serikali katika kukabiliana na maafa kama hayo katika maeneo
yaliyoathirika.
Akiwa
katika eneo linalotuama maji la Mwanakwerekwe, Dk. Shein alisisitiza haja ya
kufanywa kwa uchunguzi wa kina katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la kutuama
maji katika eneo hilo ambalo historia yake halioneshi kuwa eneo hilo linakaa
maji kama lilivyo hivi sasa.
Aliongeza
kuwa miongoni mwa hatua hizo za uchunguzi ni pamoja na kulifanyia kazi wazo la
wa maji hayo yanayotuama kuyapeleka Ziwa Maboga ama kuyatafutia njia kuyapeleka
Sebleni, kuyahifadhi maji katika eneo hilo ili yaweze kutumika kwa mahitahji
mengine huku akieleza haja ya kufanya taratibu katika kuhakikisha barabara
iliyopo katika eneo hilo iweze kupitika wakati wa msimu wa mvua.
Katika
eneo la Karakana Dk. Shein alipongeza mafanikio yaliyopatikana kutokana na
Mradi wa (ZUSP) na kuutaka uongozi wa
Jimbo la Chumbuni kwa kushirikiana na wananchi wao kuyaenzi na kuyalinda maeneo
ya wazi ambayo hapo siku za nyuma yalikuwa yakituama maji ili waweze kuyafanyia
shughuli nyengine za kijamii.
Katika
eneo hilo Mkurugenzi wa Idara ya Mipango
Miji Kazi na Ujenzi, Idara ya Manispaa Zanzibar Mzee Khamis Juma alimueleza Dk.
Shein mafanikio yaliopatikana kutokana na mradi huo na kumueleza kuwa katika
kipindi hichi hakuna mwananchi aliehama ama kupata athari za maji ya mvua
zinazoendelea na kueleza jinsi wananchi walivyofurahishwa na juhudi hizo za
Serikali.
Nao
uongozi wa Jimbo la Chumbuni ulipongeza juhudi za Serikali katika ujenzi wa
mradi huo ambao kwa maelezo ya Mbunge wa Jimbo hilo Ussi Salum Pondeza,
mafanikio makubwa yamepatikana na kuahidi kushirikiana na Serikali katika
kuyaendeleza maeneo ya wazi ambayo siku za nyuma wakati wa mvua za masika
yalikuwa yakituama maji.
Dk.
Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwapa pole wananchi wa Bumbwisudi kwa Goa kwa
kupata maafa yaliyotokana na mvua na kupelekea nyumba 66 kuharibika na nyengine
kuangua kabisa na kuwapongeza wananchi hao kwa kuonesha moyo mkubwa wa
kusaidiana na kustiriana wakati wa maafa hayo kwa wale walioathirika na mvua
hizo.
Aliwapongeza
wananchi hao kwa kustahamili,kutohadhibika na kutoilaumu serikali na badala
yake waliipokea hali hiyo na kumshukuru Mwenyezi Mungu na kueleza juhudi
zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwapelekea miradi
ya maendeleo wananchi wa Bumbwisudi ikiwemo barabara, umeme, elimu, afya na
mengineyo. “ Bumbwisudi ya leo sio ile ya zamani”,alisisitiza Dk. Shein.
Dk.
Shein aliwaeleza wananchi hao hatua za makusudi zitakazochukuliwa na serikali
katika kuhakikisha inaendeleza juhudi zake za maendeleo kwa kutoa mashirikiano
kwa wananchi wa Bumbwisudi na maeneo mengine kutokana na athari walizozipata,
ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa misingi katika barabara na makalbi yanayokidhi
haja.
Akiwa
Mwera Gudini, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya kuijenga kwa kiwango cha
lami barabara inayotoka Mwera kupitia Birikani hadi Fuoni meli saba (Kwa
Chimbeni), kutokana na umuhimu wake mkubwa.
Huko
Fuoni Kibonde Mzungu, Dk. Shein alipata maelezo juu ya hatua zitakazochukuliwa
na Serikali kupitia Wizara husika juu ya ujenzi wa daraja litakalokidhi haja
katika eneo hilo mara tu mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Mwanakwerekwe hadi
Tunguu utakavyoendelea awamu ya Pili kutoka Fuoni Polisi ulipofikia hadi
Tunguu.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein alipata maelezo juu ya ujenzi wa daraja la Mwanakwerekwe
nyumba mbili, ambalo kwa maelezo ya uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji, daraja hilo litajengwa kwa kuengezwa upana ili gari ziweze kupishana pamoja na kuzidishwa
umadhubuti zaidi.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha ziara yake hiyo, Dk. Shein
alisema kuwa Serikali imekuwa ikijipanga wakati wote katika kukabiliana na
maafa na pale yanapotokea huchukua hatua
za makusudi katika kukabiliana nayo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa
Serikali ipo na itaendelea kuwatunza na kuwasaidia wananchi wake pamoja na
kushirikiana nao katika maafa kama hayo na kuwataka wananchi kustahamili na
kutulia na kusubiri Serikali inasema nini juu ya athari hizo.
Dk.
Shein anatarajiwa kuelekea kisiwani Pemba hapo kesho kwa ziara kama hiyo katika
maeneo mbali mbali yaliyopata maafa na kuathirika na mvua za masika
zinazoendelea hapa nchini.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment