Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar ashiriki ujenzi wa msikiti wa Ijtimai ya kimataifa Unguja

 Katikati Ni Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Mabodi pamoja na viongozi wengine wakipeleka  bati  kwa mafundi wanaoezeka msikiti wa ijitimahi.

 Msafara  uliofuatana na Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi” wakionyeshwa maeneo mbali mbali ya Ijitimai hiyo.

 Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi”  pamoja na viongozi wengi wakiomba dua mara baada ya kufanya shughuli za ujenzi
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini  Unguja Vuai Mwinyi Mohamed (kushoto) akimuonyesha Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi”  ramani ya msikiti na nyumba zingine zinazotakiwa kujengwa katika eneo hilo.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla  Juma  Saadala “ Mabodi” amewasihi  viongozi na waumini wa dini ya kiislamu kutumia fursa ya Ijitimai kuliombea  taifa  liendelee kudumu katika hali ya Amani na Utulivu.

Nasaha hizo amezitoa mara baada ya kushiriki katika shughuli za ujenzi wa   Msikiti wa Ijitimai ya Kimataifa huko katika kijiji cha Kidoto Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema mamia ya waumini wa dini ya kiislamu watakaoshiriki katika ijitimai hiyo watakuwa ni sehemu muhimu ya kufanya dua mbali mbali za kuimbea nchini inusurike na maafa ili wananchi waendelee na shughuli zao za kijamii.

Alieleza kwamba CCM  inaunga  mkono juhudi zinazofanywa na taasisi za kidini nchini katika kuhubiri amani na mshikamano  kwa wananchi wa visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Alisema licha ya Chama hicho kuwa ni taasisi ya kisiasa  bado kina jukumu kubwa la kushiriki  kikamilifu  katika shughuli za kidini zinazoendeshwa na wananchi wa wa itikadi tofauti  za kisiasa.

Aidha kwamba  Chama Cha Mapinduzi Zanzibar  kitatoa msaada wa kupeleka nguzo za umeme katika nyumba ya wageni pamoja na kununua vifaa vya samani za ofisi ya jumuiya inayosimamia  Ijitimai  hiyo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Akitoa taarifa juu ya maendeleo ya Ijitimai hiyo, Katibu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Mwalim Hafidh amesema bado wanaendelea kumalizia  ujenzi wa msikiti utakaochukua waumini zaidi ya 5100 kwa wakati mmoja.

Alisema bado wanakabiliwa na changamoto za upungufu wa vifaa vya ujenzi wa mabanda yatakayotumika  wakati wa Ijitimai pamoja na ujenzi wa shule , chuo cha madrasa, hospitali na maktaba  pamoja na miundombinu mingine nyingine ya kijamii.

Aidha ameupongeza uongozi wa CCM kwa ziara hiyo na kueleza kuwa taasisi nyingi za kisiasa zimekuwa hazishiriki ipasavyo katika masuala ya kidini hali inayosababisha kutokuwepo na ushirikiano mzuri kwa taasisi hizo.

Naye  Makamo Mwenyekiti wa  Jukumiya Fiysabilillah Tabligh Markaz Zanzibar, Sheikh Wakat Hassan Bakar Alisema lengo la  jumuiya hiyo ni kukifanya kijiji hicho kuwa chimbuko la uislamu  na ibada.

Naibu Katibu Mkuu huyo ameambatana na baadhi ya ujumbe kutoka       Baraza la Wazee CCM Zanzibar, Uongozi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkuu wa Mkoa huo, Vuai Mwinyi Mohamed.

Ijitimai hiyo inatarajiwa kufanyika Mai 19, mwaka huu na kuudhuriwa na wageni kutoka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda, Ethiopia na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.