Habari za Punde

Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Mwaka 2016/17 Kufanyika Dar es Salaam Mwishoni Mwa Mwezi Mei, 2017

Baadhi ya Washiriki waliohudhuria Mkutano wa Wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/17 uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bi. Sophia Mjema akizungumza hivi karibuni na  Wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/17. Kwa Dar es Salaam, utafiti huu  unatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi Mei, 2017.
 Mkurugenzi Msahauri,  Dkt. Cecilia Makafu kutoka Shirika la ICAP Tanzania akiwasilisha mada kuhusu Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/17 kwa wadau wa Utafiti huo wa Mkoa wa Dar es Salaam.












Na: Veronica Kazimoto.Dar es Salaam
05 Mei, 2017.
Wito umetolewa kwa Wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam ambao kaya zao zimechaguliwa kitaalam kwa ajili ya  Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/17 kutoa ushirikiano kwa wadadisi wataokusanya taarifa za utafiti huo utakaofanyika mwishoni mwa mwezi Mei, mwaka huu.

Akizungumza hivi karibuni katika  Mkutano wa Wadau wa Utafiti huo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bi. Sophia Mjema amesema Utafiti huu ni muhimu sana kwani husaidia kujua hali halisi ya ugonjwa wa UKIMWI na hivyo kuongeza nguvu zaidi ya kuondokana na ugonjwa huo.

"Mimi niwaeleze tu kwamba, utafiti huu ni muhimu sana katika mkoa wetu wa Dar es Salaam kwa kuwa utatusaidia kujua hali halisi ya maambukizi ya VVU na hatimaye kupata nguvu zaidi za kuondokana na ugonjwa huu, hivyo nawaagiza kusimamia zoezi hili na kuwahimiza Wananchi wote ambao kaya zao zimechaguliwa kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaofanya taarifa za utafiti huu", amesema Mjema.

Mjema amefafanua kuwa, utafiti huu ni wa kwanza kukusanya taarifa zinazohusiana na maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa watu wanaoishi na VVU na wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote pamoja na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell count).

Aidha,  utafiti huu utapima uwepo wa viashiria vya usugu wa dawa, kiwango cha maambukizi ya kaswende pamoja na homa ya ini (Hepatitis B).

Akizungumzia kiwango cha maambukizi ya VVU katika tafiti zilizopita, Mkuu wa Wilaya huyo ameeleza kuwa, maambukizi yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003 mpaka asilimia 5.1 mwaka 2011 na kuifanya Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zenye kiwango cha chini cha maambukizi ya nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo nchi nyingi za ukanda huo zina kiwango cha zaidi ya aslimia 10.

Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Grace Magembe amesema kuwa, kwa mkoa wa Dar es Salaam, utafiti huu utahusisha kaya zisizozidi 1,000  na Wananchi watakuwa na hiari ya kukubali kupima ambapo kwa wale watakaogundulika kuwa na maambukizi, watapata rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.

"Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI hauhusishi watu wote bali ni kaya chache tu ambazo zimechaguliwa kitaalam ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine na kwa hapa Dar es Salaam kaya zilizochaguliwa hazizidi 1000", amesema Dkt. Magembe.

Utafiti wa aina hii ni wa mara ya nne (4) kufanyika nchini Tanzania ambapo wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa pili mwaka 2007 na wa tatu mwaka 2011.

Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 /17 unafanyika nchini, chini ya usimamizi wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS)  na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.