STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.06.2017

RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein
ametanabaisha na kusisitiza juu ya umakini mkubwa unaohitajika katika kuandaa,
kusimamia na kufuatilia Mikataba ya Mafuta na Gesi ili kuepuka ubabaishaji kwani
rasilimali hizo ni za Wazanzibari wote.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba
yake aliyoitoa katika Baraza la Idd El Fitri lililofanyika huko katika ukumbi
wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisisitiza kuwa mikataba ya Mafuta na Gesi Asilia
isitoe mwanya wa kuwanufaisha watu wachache na makampuni yao kwa njia za
kijanja, dhulma na mambo ya ubabaishaji na kutaka kujifunza kwa waliotangulia
katika biashara ya aina hiyo.
Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kuwa baada
ya kukamilika kwa kazi ya kutunga Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia, kuanzisha
Mamlaka ya Kusimamia na kuratibu shughuli za Mafuta na Gesi na kuanzisha
Kampuni ya Mafuta, hatua muhimu inayofuatana ni kuandaa Mikataba ya Mafuta na
Gesi Asilia.
Alisema kuwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira, wataalamu na Taasisi zote zinazohusika katika kuandaa
Mikataba hiyo, wafahamu kuwa rasiliamali ya Mafuta na Gesi Asilia ni ya
Wazanzibari wote.
Hivyo, alisisitiza kuwa wote hao wana dhamana na
jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake
yanalindwa na vigezo vyote muhimu vinazingatiwa.
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa juhudi
anazoendelea kuzichukua katika kukuza uchumi, ikiwemo ufufuaji na uendelezaji
wa sekta ya viwanda na uzuiaji wa usafirishaji wa mchanga wenye dhahabu nje ya
nchi pamoja na kuzilinda rasilimali za Taifa.
Aidha, alisema kuwa Watanzania wote, bila ya
kujali itikadi zao za kisiasa, hawana budi wamuunge mkono na kumpa moyo kwa
kazi nzuri anayoifanya.
Alisema kuwa juhudi anazozichukua za kupambana na
rushwa na uhujumu wa uchumi, ni katika kulitekeleza jukumu la Serikali la
kuwatumikia wananchi kama ilivyoelekeza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka
2015-2020.
Alhaj Dk. Shein pia, alieleza kuwa Serikali
anayoiongoza itaendelea kuweka usimamizi madhubuti wa matumizi ya fedha zake
kwa kuweka vipaumbele katika mambo muhimu yenye kuleta tija kwa maendeleo ya
nchi.
Aliongeza kuwa Serikali itaongeza kasi kwenye vita
vya kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi na kusimamia utekeleza wa misingi
yote ya utawala bora huku akizipongeza TRA na ZRB kwa juhudi zao zilizopelekea
kuvuka malengo ya ukusanyaji wa Mapato pamoja na kuupongeza uongozi wa Wizara
ya Fedha na Mipango kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa
matumizi.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwata viongozi
kushirikiana na wananchi kwani
wanamategemeo makubwa kwa Serikali yao katika kuwatumikia kama walivyoahidi na
kuwataka kila mmoja kutekeleza wajibu wake kwani viongozi wa dini, siasa na wa
kijamii wana wajibu wa kuzitekeleza dhamana zao. Kadhalika watumishi wa umma
nao wanapaswa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kwa misingi ya usawa.
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kutoa shukurani zake za dhati kwa Mashekh
na Waalimu wote waliofanya kazi kubwa ya kutoa darsa mbali mbali, katika Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan kwa lengo la kukumbusha juu ya maamrisho ya Mola wa viumbe
wote.
Alitoa pongezi maalum kwa wananchi na wageni ambao
hawakuwa katika funga kwa ushirikiano waliouonesha kwa ndugu zao Waislamu jambo
ambalo limeonesha kielelezo cha uhusiano mwema na kupevuka kwa utamaduni wa
kuishi kwa kustahamiliana huku akiwatakia safari njema Waislamu watakaokwenda
kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu.
Pia, aliwapongeza wananchi wote kwa kudumisha hali
ya amani na utulivu nchini wakati wote
khususan katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuvipongeza
vikosi vya ulinzi na usalama kwa kusimamia hali hiyo.
Aliwapongeza kwa dhati wafanyabiashara wote
waliolizingatia ombi lake alilolitoa kwao kwa lengo la kuwahurumia ndugu zao na
kutafuta radhi za Mola wao, pale walipoitikia wito wa Serikali wa kuwataka
kutopandisha bei ya bidhaa zao katika Mwezi wa Ramadhan ili kuwapa unafuu
wananchi.
Alhaj Dk. Shein aliwataka wananchi kuendelea
kuchukua tahadhari katika kukabiliana na maradhi ya kipindupindu kwa kutekeleza
maelekezo yote yanayotolewa na Serikali, ili ile hali iliyotokea mwaka 1978 na
mwaka 1998 isitokee tena na kueleza kuwa iwapo kanuni za afya bora, usafi wa
mazingira na vile vile ujenzi unaozingatia sheria za mipango miji na vijiji
zitazingatiwa ugonjwa huo utatokomezwa.
Alieleza kuwa Serikali inachukua hatua ya kuandaa
Mpango wa kinga dhidi ya maradhi ya kipindupindu kwa kushirikiana na Shirika la
Afya Duniani (WHO) ambapo wataalamu wa Shirika hilo wanatarajia kufika hapa
nchi ni hivi karibuni.
Katika Baraza hilo la Idd El-Fitri viongozi mbali
mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mama Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Idd, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Spika wa Baraza la
Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na wengineo.
Mapema asubuhi, Dk.
Shein aliungana na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya Idd el Fitri
iliyofanyika katika viwanja vya Maisara mjini Unguja.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment