STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 27.06.2017

RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein ametoa
wito kwa madereva wote hapa nchini kutoendesha vyombo vyao kwa mwendo wa kasi
ili kuepuka ajali zisizo za lazima hasa katika kipindi hichi cha Sikukuu ya
Idd- El- Fitri ambacho wananchi walio wengi hutumia huduma za usafiri wa
barabarani wakiwemo watoto.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo wakati akifanya
mahojiano na watoto wanaotayarisha kipindi cha “Watoto na Sikukuu” kutoka
Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), huko Ikulu mjini Zanzibar, ikiwa ni
miongoni mwa shamrashamra za skukuu ya Idd El Fitri.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa
uendeshaji wa vyombo vya moto kwa kasi ni hatari hali ambayo inaweza
kusababisha ajali zisizo za lazima kwani hakuna sababu ya kufanya hivyo kwa
kuepuka kuleta madhara hasa kwa watoto huku akisisitiza haja kwa askari wa barabarani
kuwa makini kwa madereva wote wanaoendesha vyombo vyao kwa kasi.
Hivyo, Alhaj Dk. Shein aliwataka madereva wa
vyombo vyote vya moto kufuata taratibu, sheria za barabarani sambamba na kuwa
makini wakati wakiendesha vyombo vyao kwani katika kipindi hichi cha Sikukuu
wananchi waliowengi wakiwemo watoto hutumia barabara kwa safari zao mbali mbali
zikiwemo za kwenda kutembeleana pamoja na kwenda katika viwanja vya skukuu.
Alhaj Dk. Shein alisisitiza kuwa Sikukuu ni furaha
hivyo kila mmoja ana nafasi na fursa ya kusherehekea lakini kwa upande wa
madereva ni vyema wakatumia furaha yao kwa kwenda mwendo mzuri pamoja na
kufuata, sheria, kanuni na taratibu za barabara ili kuepuka ajali.
“Na nyinyi watoto msije kuingia kwenye gari halafu
mkawatia pampu madereva kwa kuwapigia kelele, ili waendeshe gari zao mbio, huku
mkiema ndio babu hivyo hivyo engeza mwendo, si vizuri na mkiiona gari inakwenda
mbio basi msipande”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alieleza azma ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha michezo kwa watoto ikiwa ni pamoja
na kuutekeleza Mpango wa “Sport 55”, unaolenga kuongeza hamasa ya ushiriki wa
wanafunzi katika michezo kwa kuzipatia vifaa vya michezo skuli 55 Unguja na
Pemba kwa hatua ya awali, kutengeneza viwanja, mafunzo ya kiufundi na kiutawala
kwa walimu na viongozi wa michezo kwa kila Wilaya na Mikoa.
Pia, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa katika
kutekeleza hilo tayari jumla ya TZS milioni 300 zimeshakushanywa kwa lengo la
kutekeleza azma hiyo huku akisisitiza kuwa kila wilaya kutajengwa viwanja vya
michezo na zitaanza Wilaya tano na tayari viwanja viwili vimeshaanza kujengwa.
“Tunafanya Mpango mkubwa ili watoto wapate kucheza na wacheze katika mazingira
yalio bora na yalio mazuri”,alisema Alhaj Dk. Shein.
Akizungumzia juu ya maradhi ya kipindupindu, Dk.
Shein alitoa wito kwa wananchi wakiwemo watoto kulipa kipaumbele suala zima la
usafi kwani maradhi hayo chanzo chake kikubwa ni uchafu.
Alhaj Dk. Shein aliwaeleza watayarishaji hao
uzoefu wake wa maradhi hayo katika mwaka 1968 na mwaka 1998 pamoja na miaka ya
hivi karibuni kwa jinsi maradhi hayo yalivyoleta athari kubwa vikiwemo vifo na
kueleza umuhimu wa kuimarisha usafi ukiwemo usafi wa mtu mwenyewe, mazingira
anayoishi, katika miji na sehemu zote zilizoizunguka jamii.
Kwa upande wa vita dhidi ya dawa za kulenya, Alhaj
Dk. Shein alieleza mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kupambana na dawa hizo kwa wanaoingiza, wanaouza na hata wale wanaotumia na
hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Kutokana na hatua hiyo, Alhaj Dk. Shein alitoa
wito kwa watoto kutoiga tabia za matumizi ya dawa za kulevya na wakimbie wala
wasizikurubie kwani zinamadhara makubwa, huku akiwaeleza jinsi Serikali kwa
upande wake itakavyoendelendea kuwalinda, kuwaenzi na kuwatunza watoto wote.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa
wazazi na walezi kuchukua jitihada za kuwalea watoto vizuri na kuwafundisha
maadili mema na silka za Kizanzibari huku akisisitiza haja kwa wazazi na walezi
kuwaandalia watoto vyakula vizuri katika
kipindi hichi cha Sikukuu.
Hivi karibuni Alhaj
Dk. Shein alipofanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Tanzania (IGP)
Simon Nyakoro Sirro, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha
rasmi kwa Rais alimueleza haja ya kuwepo mashirikiano ya kutosha kwa askari wa
barabarani pamoja na taasisi husika inayotoa leseni za udereva wa vyombo vya
moto ili kuepusha ajali zisizo za lazima ambazo zimekuwa zikitokezea mara kwa
mara.
Nao watoto hao kwa niaba ya watoto wenzao wote
walitoa pongezi na shukurani kubwa kwa Rais Alhaj Dk. Shein kwa juhudi za
makusudi anazozichukua katika kuhakikisha Serikali anayoiongoza inawapenda,
inawatunza, inawajali na inawathamini watoto.
Mapema Dk. Shein alipeana salamu za Idd el Fitri
na viongozi wa dini pamoja na viongozi wa Serikali hapo Ikulu mjini Zanzibar na
baadae kutoa skukuu kwa wananchi mbali mbali waliofika katika viwanja vya Ikulu
wakiwemo watoto.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment