Habari za Punde

ZSTC yakabidhi vifaa vya kuendeleza vitalu vya miche ya karafuu

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar Dkt. Said Seif Mzee (kulia) akimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mliasili, Mifugo na Uvuvi Dkt. Juma Ali Shehena ya vifaa vilivyotolewa na Shirika hilo kwa ajili ya kuimarisha vitalu vya miche ya mikarafuu.
Picha na Ramadhani Ali.

Na Ramadhani Ali – Maelezo  

Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) limeikabidhi Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi  vifaa kwa ajili ya kuendeleza vitalu vya miche ya mikarafuu vyenye thamani ya shilingi milioni 26 na fedha taslimu milioni kumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZSTC Dkt. Said Seif Mzee amemkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Maliasili, Mifugo na Uvuvi Dkt. Juma Ali kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo katika hafla iliyofanyika Wizarani Maruhubi.

Dkt Said amesema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakishirikiana na Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka katika mambo yanayoongeza tija katika uzalishaji wa miche ya mikarafuu na pia katika kutoa elimu kwa wakulima wa karafuu juu ya njia bora ya kupanda kuhuisha na kuzichuma.
Mkurugenzi Mtendaji alieleza kuwa Shirika katika kuendeleza zao la karafuu litaendelea kutoa misaada ya kuimarisha taasisi za Serikali na taasisi za watu binafsi zenye nia ya kuimarisha zao hilo kubwa la kiuchumi Zanzibar.

Amekumbusha kwamba katika mwaka 2015/2016 Shirika Shirika lilitoa msaada wa wenye thamani ya shilingi milioni 70.8 kwa Idara  ya Misitu na kuvisaidia vikundi 10 vinavyootesha miche ya mikarafuu yenye thamani ya shilingi milioni mbili laki nne.

Akipokea vifaa hivyo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo alisema Wizara itaendeleza juhudi za Serikali ya kuhakikisha inazalisha zaidi ya  miche milioni  moja kwa mwaka Unguja na Pemba katika kuhakikisha zao hilo linaendelea kuimarika.
Amesema watahakikishia wanafuatilia miche mipya iliyopandwa mwaka huu ili kuona inakua vizuri na hatimae kutoa mavuno makubwa miaka michache ijayo.

Vifaa vilivyokabidhi  ni pamoja na nyavu za vitalu za kivuli na paipu za kujengea vitalu, saruji, kamba, nondo, mchanga, kokoto kwa ajili ya kuchimba visima vipya vya kumwagilia maji vitalu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.