Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Ujumbe wa TMF.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na kubadilishana mawazo na Uongozi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania { TMF } hapo Ofisini kwake kwenye Majengo ya Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Media Foundation Nd. Ernest Sungura.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Media Foundation Nd. Ernest Sungura kushoto akimueleza Balozi Seif  Mikakati ya TMF katika kuwafinyanga Wanahabari kuandika Habari  na Makala yaliyofanyia Utafiti na Uchunguzi.
Ujumbe wa Viongozi wa TMF uliofanya mazungumzo na Balozi Seif wa kwanza kushoto ni Mwanakhamis Mparu Mwenyekiti wa Bodi ya Redio Iqra na Bibi Florah Boniface Magabe Mshauri wa Waandishi wa Habari wa TMF.
Balozi Seif Ali Idi Kati  kati akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania uliofika Ofisini kwake majengo ya Baraza la Wawakilishi kubadilishana mawazo.
Balozi Seif akiagana na  Uongozi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania uliofika Ofisini kwake majengo ya Baraza la Wawakilishi kwa mazungumzo.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR.
Mkurugenzi Mkuu wa  Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania { Tanzania Media Foundation – TMF } Bwana Ernest Sungura  amesema hadhi ya Sekta ya Habari Nchini itaheshimika na kuaminika zaidi endapo wanahabari wenyewe watajiwekea malengo ya kufanya kazi kwa agenda katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alisema mfumo wa agenda kwa Wanahabari ndio njia pekee itakayosaidia  kuamsha ari sambamba na kuibua changamoto zinazokwaza Jamii na kuzipa nguvu za uwajibikaji Taasisi za Umma na hata zile binafsi katika kuwahudumia kwa umakini Wananchi.

Nd. Ernest Sungura  Alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa TMF uliokuwepo Zanzibar  kwa ziara maalum ya kukagua  Maandalizi na Mikakati  ya mradi wa kuwapatia Mafunzo Wanahabari wa Zanzibar.

Alisema kupitia Mfuko wa Vyombo vya Habari zipo agenda zilizowahi kuibuliwa na Wanahabari wa Vyombo tofauti Nchini akizitolea mfano  Escro, Dawa  za Kulevya, Udhalilishaji wa Kijinsia na Ubalozi wa Usalama Bara barani ambazo zimesaidia kuleta faraja kwa Jamii na kuzipunguzia matumizi mabovu yasiyo na msingi Serikali zote mbili.

Alieleza kwamba yapo mambo mengi na mazuri ya kujivunia  kutokana na kuanzishwa kwa mfumo huo wa agenda  jambo ambalo limeziletea sifa Taasisi za Habari kwa Taifa na Wananchi jambo ambalo lilisaidia kuibua changamoto zinazokwaza Serikali na Jamii kwa ujumla.

Bwana Sungura alimueleza Balozi Seif  kwamba katika kuwajengea uwezo uliobobea Waandishi wa Habari katika utekelezaji wa kazi zao TMF mwaka huu imeshatenga  Fedha Maalum kwa ajili ya kuwapatia mafunzo Wanahabari  wasiopungua Mia 600 kutoka vyombo 120 vya Habari Nchini.

Alisema mkazo zaidi wa mafunzo hayo utawekwa kwa wale waandishi na Vyombo vya Habari visivyo na uwezo wa kufanyakazi vizuri  ili navyo viweze kupiga hatua itakayokwenda sambamba na wenzao wenye nguvu za uwezeshaji kifedha.

Naye Mshauri wa Waandishi wa Habari wa TMF Bibi Florah Boniface Magabe  alisema Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa zaidi kiuchumi kama itaamua kuzitangaza fursa za Utalii zilizopo Visiwani Unguja na Pemba.

Bibi Florah alisema michezo ya Utalii wa Uzamiaji inayopendwa sana na Watalii Duniani inaweza kufungua njia pana zaidi ya ongezeko la idadi ya watalii wanaoingia Zanzibar  na kuikaribia Nchi ya Misri inayokusanya mapato makubwa kupitia fani hiyo ya michezo ya Baharini.

Alipendekeza utangazi huo wa Utalii wa Uzamiaji unaweza kutumiwa katika Matamasha mbali mbali yanayoandaliwa Zanzibar  likiwemo lile la Sauti za Bisara, ZIFF pamoja na Tamasha la Mzanzibari yanayokusanya wageni wengi kutoka Mataifa mbali mbali Duniani.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania { TMF } kwa uamuzi wake wa kuwafinyanga Wanahabari katika misingi ya kuwajibika Kitaaluma zaidi badala ya kukurupuka katika Uandishi wao.

Balozi Seif alisema kitendo cha Taasisi hiyo cha kuwajengea uwezo wa Kitaaluma Wana Tasnia hao wa Habari kitawawezesha kuzalisha zao litakalopokewa vyema tena kwa Heshima kutoka kwa Jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.