Habari za Punde

Bendera ya CAF haipo tena Zanzibar mlingoti upo mtupu

 Bendera ya CAF ilivyokuwa ikipepea nje ya uwanja wa Amaan sehemu ya VIP
Mlingoti ulivyo mtupu baada ya bendera hiyo kushushwa baada ya Zanzibar kuvuliwa uanachama CAF.

Na: Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar.

Siku moja tangu Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kutangaza kuifutia Zanzibar uanachama wake wa kudumu wa 55 wa Shirikisho hilo, leo kwa mara ya kwanza Bendera ya CAF visiwani Zanzibar imeshindwa kupepea na kuambulia mlingoti kuwa mtupu .

Tangu Zanzibar kupata uanachama wa shirikisho hilo Bendera ya CAF ilikuwa ikipepea katika Uwanja wa Amaan sehemu ya V.I.P nje kwenye bustani ndogo, na hiyo ilikuwa ni kiashiria ya kuwa kweli Zanzibar ni mwanachama wa kudumu wa 55 wa shirikisho hilo.

Juzi Kamati ya utendaji ya CAF ilikutana mjini Rabat, Morocco na kuamua mambo kadhaa likiwemo hilo la Zanzibar kufutiwa uanachama wake ambapo Viongozi wakuu wa chama cha Soka Zanzibar (ZFA) walikuwepo katika Mkutano huo ambapo alikuwepo Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina, Katibu Mkuu wa ZFA Mohd Ali Hilali “Tedy” pamoja na kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) Hemed Suleiman “Morocco”.

Jana Rais wa Caf, Ahmad Ahmad amesema Zanzibar ilipewa nafasi hiyo kimakosa na si sahihi kwa nchi moja kuwa na wanachama wawili wa shirikisho hilo.

Zanzibar ilipewa uanachama wakati wa utawala wa Issa Hayatou ambaye alikuwa akiungwa mkono na TFF chini ya Jamal Malinzi, hata hivyo Hayatou aliangushwa na Ahmad Ahmad ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi wa CAF.

Hata hivyo, Zanzibar kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefanya kuvuliwa tena uanachama huo na kuendelea kubaki kama ilivyo.

Siku ya Alhamis Machi 16, 2017 itaendelea kukumbukwa na Wazanzibar baada ya ZFA kuingizwa rasmi kuwa Mwanachama wa 55 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF” kufuatia Kikao cha 39 cha Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo kilichofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia,uanachama ambao umedumu kwa siku 128 tu tangu siku hiyo mpaka jana July 21, 2017.

Katika kura 54 za CAF, kura 51 zimekubali Zanzibar ipatiwe uanachama wa kudumu wa Shirikisho hilo na nchi 3 zilikataa Zanzibar isipatiwe ambazo ni Madagascar, Benin na Seychelles ambapo Madagascar ndio nchi anayotoka Rais wa sasa wa CAF Ahmad Ahmad.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.