Habari za Punde

Charawe Hatuchezi Ligi Two Kwa Sababu Sisi Tumepanda Ligi Kuu ya Zanzibar.

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.
Uongozi wa klabu ya Charawe Stars umefanya kikao chao kwa Wanakijiji pamoja na Mashabiki wao wa Mjini kwa kauli moja wameamua kutocheza ligi 2 na kutaka kupangiwa na ZFA kucheza ligi 1 ambayo ndio ligi kuu soka ya Zanzibar kwa vile wao wamepanda daraja kucheza ligi hiyo.

Akizungumza na Mtandao huu Ramadhan Abdallah “Sadifa” ambae ni msemaji mkuu wa timu hiyo amesema baada ya kumaliza kikao chao kwa pamoja wameamua kususia kucheza ligi 2 ambayo ndio waliyopangiwa na msimamo wao ni kucheza ligi 1 na sio ligi nyengine kwani wamepanda kucheza ligi kuu kwa nguvu zao.

“Tumefanya kikao cha pamoja wadau wote wa timu ya Charawe wa mjini na Kijijini na tumeamua kutocheza ligi 2, sisi msimamo wetu tucheze ligi 1 mana tumepanda daraja kwa nguvu zetu kisha leo tunaambiwa tucheze ligi 2, hatukubaliani na uamuzi huo”. Alisema Sadifa.

Jumamosi ya July 8, 2017 Viongozi wa vilabu 28 vya Unguja na Pemba walikutana katika ukumbi wa Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba na kuamua timu zitakazoshiriki ligi kuu soka ya kwa msimu wa mwaka 2017-2018 ambapo wameamua timu zilizomaliza nafasi ya 1-6 kwa kila kanda, yani Unguja na Pemba ndizo zitakazocheza ligi kuu wakati huo huo Bingwa atapata nafasi ya kuwakilisha Zanzibar katika Kombe la Klabu Bingwa Barani Afrika.

Timu 16 kati ya 28 zilizosalia ambazo hazijashuka daraja zitacheza ligi two ambapo Bingwa wa ligi hiyo atapata nafasi ya kuwakilisha Zanzibar kwenye kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Timu hizo 12 zilizofanikiwa kucheza ligi kuu (Ligi 1) msimu mpya wa mwaka 2017-2018 ni JKU, Jang’ombe Boys, Zimamoto, Taifa ya Jang’ombe, Polisi, KMKM kwa upande wa Unguja na Pemba ni Jamhuri, Kizimbani, Mwenge, Okapi, Chipukizi na New Stars.

Kwa upande wa timu 16 zitakazocheza ligi 2 msimu mpya wa mwaka 2017-2018 kati ya hizo 8 za Unguja na 8 za Pemba ambapo za Unguja ni Mafunzo, KVZ, Black Sailors, Chuoni, Kilimani City, Kipanga, Miembeni City na Charawe wakati za Pemba ni Dogomoro, Wawi Star, Shaba, Young Islander, FSC, Hardrock, Chuo Basra na Opek ambapo timu 4 za mwisho za ligi 1 zitashuka daraja ligi 2, na timu 4 za juu za ligi 2 zitapanda daraja la ligi 1 huku hoja yao kubwa Charawe wao pamoja na Miembeni City, Chuo Basra na Opek wamesema walistahiki kucheza ligi kuu kwa vile walipanda daraja lakini nafasi zao zikachukuliwa na Polisi,KMKM, Chipukizi na New Stars waliyomaliza nafasi ya 5 na 6 kwa kanda ya Unguja na Pemba kwenye ligi kuu msimu wa mwaka 2016-2017.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.