Habari za Punde

Balozi Seif Amewataka Maafisa Wadhamini Kusimamia Taasisi na Wafanyakazi Kutekeleza Majukumu ya Utumishi wa Umma Kikamilifu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Viongozi wa Serikali wa Mikoa Miwili Kisiwani Pemba hapo katika Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.
Wakuu wa Wilaya zilizomo ndani ya Mikoa Miwili ya Pemba wakichukuwa kumbu kumbu wakati wa Mkutano wao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani.
Baadhi ya Maafisa Wadhamini na Viongozi wa Serikali Kiswani Pemba wakifuatilia Hotuba ya Balozi Seif  hayupo pichani kwenye kikao chao cha kawaida wakati anapofanya ziara za Kiserikali Kisiwani humo.
Makamanda wanaounda Kamati za ulinzi na usalama za Mikoa Miwili ya Pemba wakimsikiliza Balozi Seif wakati akizungumza nao kuhusu suala zima la shughuli za Uokoaji wa zao la Karafuu uchumaji wake ulioanza mapema mwezi uliopita.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi amewakumbusha Maafisa Wadhamini pamoja na Viongozi wengine wenye dhamana ya kusimamia wafanyakazi wa Taasisi za Umma kuhakikisha kwamba nidhamu katika utekelezaji wa majukumu ya Utumishi wa Umma inafuatwa kikamilifu.

Alisema Serikali isingependa kuona Watumishi wake wanashindwa kuzingatia sheria na Kanuni zilizowekwa katika Utumishi wa Umma na kuamua kufanya watakavyo.

Akizungumza na Viongozi wa Serikali wa Mikoa Miwili ya Pemba hapo katika Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake chake baada ya kumaliza ziara ya siku mbili kukagua Miradi ya Maendeleo Kisiwani Pemba Balozi Seif  Ali Iddi alionya kwamba nidhamu ya kuingia na kutoka kazini kwa watendaji wa Umma Kisiwani Pemba sio nzuri.

Balozi Seif alisema Maafisa wengi wa Taasisi za Umma Kisiwani Pemba wanashindwa kusimamia vyema nidhamu ya uingiaji kazini wa kabla ya Honi ya saa Moja na Nusu asubuhi na utokaji baada ya Honi ya saa Tisa na Nusu jioni.

Alisema kitendo hicho kinawapa fursa  na kutoa mwanya kwa baadhi ya Wafanyakazi wavivu na wale wakorofi kutumia udhaifu huo wa usimamizi mbovu wa baadhi ya Maafisa hao na matokeo yake kusababisha uwajibikaji mbovu usioleta tija yoyote ile.

Akizungumzia suala la vifaa vya Kazi Balozi Seif  aliagiza kuachwa mara moja tabia ya kutumiwa ovyo vyombo vya Serikali hasa vile vya moto baada ya saa za kazi kunakooneka kusababisha uchakavu wa haraka wa vyombo hivyo.

Alisema chombo cha Serikali iwapo hakitakuwa na dharura maalum ya msingi itakayosababisha chombo cha Umma kutembea baada ya saa za kazi ni vyema kikalazwa kwa faida ya chombo chenyewe pamoja na kupunguza gharama za matumizi ya mafuta isiyo ya lazima.

Balozi Seif alieleza kuwa Watendaji wote iwe Maafisa au Wafanyakazi wa kawaida bado wataendelea kuwa na wajibu wa kusimamia miradi ya Taifa pamoja na vifaa vyake.

Mapema akitoa Taarifa fupi ya hali ya Amani na Usalama ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambae pia ni Mkuu wa Mkoa huo Mh. Mwanajuma Majid alisema maisha ya Wananchi wa Mkoa huo yanaendelea vyema bila ya matukio yoyote ya uvunjifu wa Amani katika kipindi hichi.

Mh. Mwanajuma alisema kilichopo wakati huu ndani ya Mkoa Kusini Pemba ni suala la uhamasishaji wa uchumaji wa zao la Karafuu chini ya usimamizi wa Kamati Maalum { Task Force } iliyoundwa kusimamia kazi hiyo pamoja na kufuatilia mwenendo mzima wa zoezi hilo.

Mkuu huyo wa Mkoa Kusini Pemba alieleza kwamba changamoto iliyopo hivi sasa ni ufinyu wa bajeti za kufanyia uchunguzi wa Dawa za kulevya inaendelea kulikumba jeshi la Polisi  katika uwajibikaji wake lililopewa dhamana ya kusimamia mapambano dhidi ya dawa hizo Nchini.

Alisema fedha inazopata Jeshi hilo katika bajeti inayopangiwa hasa katika uchunguzi wa kubaini dawa za kulevya ni ndogo mno kiasi kwamba ushahidi unaotokana na tuhuma za wahusika wa vitendo hivyo unakosekana na hatimae kubebeshwa lawama askari wa Jeshi hilo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ambae pia ni Mkuu wa Mkoa huo Mh. Omar Khamis Othman alisema Mkoa huo  hivi sasa unaendelea kuwa na Siasa za wastani kiasi kwamba maisha ya Wananchi wake yanaendelea vyema bila ya vikwazo hasa ikizingatiwa matukio ya ajabu yaliyozoeleka katika vipindi vya nyuma.

Mh. Omar alisema utendaji wa Serikali bado una changamoto zinazoukumba Mkoa huo hasa Magari ya Wakuu wa Wilaya yanayoonekana kuchakaa na kuleta usumbufu kwa Watendaji hao wakati wanapofuatilia majukumu yao kwenye maeneo yao ya kazi.

Alisema baadhi ya Wakuu hao wa Wilaya hulazimika kuazimwa Gari jambo ambalo halileti sura nzuri na kuiomba Serikali Kuu kuangalia uwezekano wa kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Wakitoa michango yao  baadhi ya Viongozi hao wa Serikali wa Mikoa Miwili ya Pemba walitahadharisha ubaya wa Majungu unaoonekana kuathiri uwajibikaji kwa Taasisi za Umma kutokana na baadhi ya watendaji kukumbwa na tuhuma za kadhia za fitina.

Walisema Serikali inastahiki kuwa makini kwa kufanya uchunguzi wa kina pale inapopelekewa Taarifa za makosa yanayodhaniwa kutendwa na baadhi ya Kiongozi au Mtumishi wa Umma vyenginevyo watawavunjika moyo kufanya kazi bidii na uzalendo.

Wakizungumzia zoezi la uchumaji wa Karafuu Maafisa hao wa Serikali walisema makali ya sheria iliyowekwa ya Zao la Karafuu bado ni nyepesi kwa vile inaendelea kutoa mwanya  kwa watu wenye tabia ya kufanya magendo ya zao hilo kwa kusafirisha nje ya Nchi.

Walitolea mfano wingi wa Bandari bubu zilizopo Nchini ambazo hutumiwa na wahalifu wengi kwa kusafirisha bidhaa hiyo na kuvipa kazi kubwa vyombo vya ulinzi kudhibiti hali hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.