Habari za Punde

TANZIA-ZFA Yapata Pigo Yaondokewa na Mjumbe Wao. Mchezo wa Jamhuri na Taifa ya Jangombe Mchezo Huo Kuahirishwa.

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Chama cha Soka Visiwani Zanzibar kimepokea taarifa ya msiba wa mjumbe wao kamati tendaji ZFA Taifa ndugu Suleiman Khamis maarufu Kamba ya Mbuzi uliotokea jana asubuhi jijini Dar es salam.

Marehemu alipata nafasi hiyo ya ujumbe wa kamati tendaji kupitia nafasi za umoja wa Vilabu kutokea Kisiwani Pemba.

Kabla ya kushika nafasi hiyo, marehemu aliwahi kuwa muamuzi wa mpira wa miguu wakati chama cha mpira wa miguu wakati huo kikijulikana kama EFOZA, baada ya hapo alifanikiwa kupewa nafasi ya ukatibu mkuu katika timu ya Chipukizi ambayo kwasasa inashiriki ligi kuu soka ya Zanzibar.

Marehemu alikuwa ni kiongozi aliyesimamia haki ya kikanuni na katiba na alikua hayupo tayari kuona haki haitendeki kwa mujibu wa taratibu za mpira.

Taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu ni kuwa marehemu            Suleiman alikua akisumbuliwa na Pressure na Sukari na kabla ya kusafirishwa kupelekwa Hospitali ya Agakhan jijini Dar es salam, pia alilazwa Hospitali kuu ya Chake Chake Kisiwani Pemba.

Marehemu amezikwa jana saa 10:00 alaasiri huko kijijini kwao Kengeja na ambapo kutokana na msiba huo ZFA wamefuta mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar uliokuwa uchezwe jana katika uwanja wa Gombani kati ya Jamhuri dhidi ya Taifa ya Jang’ombe.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema Peponi Amiin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.