Habari za Punde

Hilika aibuka mfungaji bora Ligi Kuu ya Zanzibar


Na: Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar.

Mshambuliaji wa Zimamoto Ibrahim Hamad Hilika ameibuka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Zanzibar kwa msimu wa 2016/2017 baada ya kufunga jumla ya mabao 14 katika hatua ya 8 bora.

Hilika alianza dalili za kuwania ufungaji bora baada ya kushinda yeye pia kwenye ligi kuu ya Zanzibar kanda ya Unguja ambapo alishinda jumla ya mabao 19 katika kanda hiyo, hivyo ukipiga hesabu 19 na 14 utapata 33 ambayo ndio idadi ya mabao aliyofunga msimu huu wote tangu ligi ilipoanza kanda mpaka kufikia hatua ya 8 bora.

Nafasi pili imekamatwa na Mwalim Mohd wa Jamhuri aliyefunga mabao 10 katika ligi kuu soka ya Zanzibar hatua ya 8 bora.

Mtandao huu umepiga stori na mshambuliaji huyo na kutaka kujua amejisikiaje kufanikiwa kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo ambapo amefurahishwa mno na kusema kuwa ni lengo lake kuwa mfungaji bora na katimiza.

“Nimefurahi sana kwani niliweka lengo hilo lakini nawashukuru viongozi wangu wote pamoja na wachezaji wangu kwani bila ya ushirikiano wao siwezi kufanikiwa kwa chochote”. Alisema Hilika.

Mpaka sasa hakuna zawadi yoyote iliyotangazwa na Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) kwa mfungaji bora wala kwa bingwa wa ligi hiyo atapatiwa zawadi gani huku wadau wengi wakihimizwa kujitokeza kuwapa hamasa vijana hao ambao wanafanya makubwa na mazuri katika soka la Zanzibar.

Mfungaji bora wa msimu uliopita wa mwaka 2015-2016 ni Hakim Khamis “Men” alifunga mabao 17 na kuisaidia timu yake Zimamoto kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ambapo pia aliwahi kuwa mfungaji bora wa ligi kuu soka ya Zanzibar msimu wa mwaka 2011-2012 wakati Super Falcon ya Pemba ilitwaa ubingwa msimu huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.