Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh.
Mmanga Mjengo Mjawiri akimkabidhi msaada wa vitabu kutoka kwa PSI Mwalimu Kaimu
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Mauwani Nd.Mussa Mohd Abass.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Mmanga Mjengo
Mjawiri akitoa nasaha zake kwa Walimu Wakuu wa Skuli zilizopatiwa msaada wa
vitabu kutoka kwa Jumuiya ya Pemba
Support Island (PSI)Pamoja na Maafisa mbali mbali wa Elimu Kisiwani
Pemba.
Walimu Wakuu wa Skuli zilizopatiwa msaada wa vitabu kutoka
kwa Jumuiya ya Pemba Support Island (PSI) pamoja na Maafisa mbali mbali wa
Elimu Kisiwani Pemba.
Na Ali Othman Ali
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh.
Mmanga Mjengo Mjawiri amekabidhi msaada wa vitabu vya Sayansi, Hesabati na
Kiingereza Uliotolewa na Jumuiya ya Pemba Support Island (PSI) kwa Skuli nne za
Sekondari ambazo ni Chasasa, Konde, Shamiani na Mauwani.
Makabidhiano hayo na Walimu Wakuu wa Skuli hizo yamefanyika
katika ukumbi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Chake Chake Pemba mbele ya
Maafisa na watendaji mbali mbali wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Kisiwani Pemba.
Akitoa nasaha zake kabla ya kukabidhi vitabu hivyo vyenye
thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni nne, Tsh 4,000,000/- Mh. Naibu waziri
amempongeza Mratibu wa Idara ya Mafunzo ya Ualimu Pemba Maalim Mkubwa Ahmed
Omar kwa juhudi zake za makusudi katika kuimarisha huduma za elimu Kisiwani
Pemba na amewataka watendaji wengine kuiga mfano wake.
Mh. Mjawiri amewataka walimu hao kuenzi na kutunza vifaa vya
zamani kwa matumizi endelevu huku akionesha kutoridhishwa na tabia ya
kuvidharau na kutokuvishughulikia vifaa vyazamani na badala yake kujikita
katika kushughulikia vifaa na majengo mapya. Ameiamuru Idara ya Ukaguzi
kuingiza kipengele cha Ukaguzi katika eneo la vifaa ili kuhakikisha kwamba
vinatumika kwa ufanisi na kwa uangalifu.
Aidha, Mh. Naibu Waziri amesisitiza haja ya waalimu kuwa na
uzalendo katika utendaji wa kazi zao. Akifafanua dhana ya uzalendo Mh. Mmanga
amesema ipo haja kwa walimu kuwa na upendo kwa jamii yao, upendo kwa kazi yao
na upendo kwa masomo wanayofundisha ambapo Mh. Naibu Waziri ameonesha wasiwasi
wake juu ya kupungua au kutokuwepo kwa moja kati ya hayo.
Kwa upande wa utoaji wa taaluma Mh. Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali amewataka walimu kutimiza wajibu wao katika kuwafundisha
wanafunzi na kuwatanabahisha kwamba wanawajibu mkubwa wakusimamia malezi ya
vijana.
“Walimu tujikumbushe kwamba tunawajibu wa kulea hivyo basi
tufanye kazi kulingana na taaluma zetu, mfanyaka kazi mwenye taalumu hasukumwi
katika kutenda majukumu yake, taaluma ndio inayomuongoza kusimamia vyema kazi
hiyo”
Mh. Mmanga amesisitiza haja ya kuwashajiisha wanafunzi wawe
na moyowakujisomea vitabu kwa wingi akitanabahisha kwamba kufanya hivyo
kutawapatia uwezo wa kujenga hoja kitaaluma.
Awali Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Pemba Mh. Salim Kitwana Sururu amemshukuru Mh. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Amali Zanzibar kwa kuwa karibu katika harakati za kukuza maendeleo ya elimu
Zanzibar.
Pemba Support Island ni Jumuiya ya misaada ambayo
ilisajiliwa rasmi mwaka 2010 ikiwa na namba usajili (CHY 19162) ambapo inatoa
misaada mbali mbali yakimaendeleo kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment