STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.08.2017
MAWAZIRI
kutoka vyama vya upinzani walioteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika serikali anayoiongoza
wameahidi kuendelea kumuunga mkono na kushirikiana nae kwani ameonesha nia
thabiti ya kuwaletea maendeleo wananchi bila ya ubaguzi kwa kutambua kuwa
maendeleo hayana upinzani.
Viongozi hao waliyasema hayo kwa nyakati tofauti
katika ziara ya Dk. Shein ya kutembelea miradi ya maendeleo sambamba na kuangalia
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 jinsi inavyotekelezwa
katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba, ziara ambayo kwa hivi sasa inaendelea katika
Mkoa wa Kusini Unguja.
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid, katika kijiji cha Mlilile
alieleza hatua ambazo Wizara anayoiongoza itazichukua katika kuhakikisha
wananchi wa kijiji hicho wanapata mafanikio sambamba na kuweza kuitumia vyema
ardhi yao ya mawe na bahari waliyonayo kwa kusogezewa miradi na Serikali ya
Mapindyuzi ya Zanzibar.
Waziri Rashid ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC)
alipongeza juhudi za Rais Dk. Shein katika kuwapelekea maendeleo wananchi wa
Zanzibar bila ya ubaguzi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwani maendeleo
hayana upinzani.
Alisisitiza kuwa huu ni wakati wa wananchi kwa
kushirikiana na viongozi wao wa Serikali kujiletea maendeleo na sio wakati wa
kudanganywa na baadhi ya wanasiasa.
Katika ziara ya Dk. Shein akiwa katika kijiji cha
Ukongoroni Waziri Rashid alimpongeza Dk. Shein kwa kufanya kazi kwa uadilifu
mkubwa na kuifanyia mambo mengi Zanzibar na kusisitiza kuwa si busara kupinga
kila kitu kinachofanywa na Serikali anayoiongoza kwani ameifanya mambo makubwa
ikiwa ni pamoja kuitoa nchi kuwa tegemezi na kubaikia asilimia saba tu kwani
sio jambo rahisi.
Aliongeza kuwa hatua hiyo, hufanywa na Rais makini
na aliyetulia kama alivyo Dk. Shein ambaye ameifikisha Zanzibar katika hatua
hiyo ambayo ameifanya vizuri huku akieleza hatua za Serikali kupitia Wizara anayoiongoza
kwa mashirikiano na Mradi wa MIVARF katika kuwasaidia wakulima wa ndimu
wakiwemo wale wa Ukongoroni.
Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum, Juma Ali Khatib
ambaye pia, ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi alieleza kuwa wao wakiwa viongozi
kutoka vyama vya upinzani wamekuwa wakishuhudia juhudi kubwa anazozifanya Dk.
Shein katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020,
Aliongeza kuwa wananchi na wanasiasa wote ni vyema
wakatambua na kuthamini juhudi kubwa anazozichukuwa Dk. Shein katika kuwaletea
maendeleo wananachi wote wa Unguja na Pemba kwa vitendo.
Waziri Khatib ambaye anatoka chama cha ‘Ada Tadea’,
alisema kuwa ahadi alizozitoa katika majukwa ya kisiasa kapmeni za uchaguzi
zilizopita, na wakati wa uchaguzi, kwa kweli anatimiza hadi zake hivyo
aliwasisitiza wananchi kumuunga mkono Dk. Shein pamoja na seetikali ayake
anayoiongoza ili kuleta maendeleo kwa wananchi wote bila ya ubaguzi na bila ya
itikadi ya kisiasa.
Aliongeza kuwa maendeleo hayo ni kwa watu wote
waliokuwa na vyama na wasiokuwa na vyama na kueleza kuwa yeye yumo ndani ya
Serikali anayoiongoza Dk. Shein na anatekeleza Ilani ya CCM na anamsaidia Dk.
Shein katika kuhakikisha Serikali inakwenda mbele pamoja na kuhakikisha Ilani
hiyo inatekelezwa.
Waziri Khatib katika maelezo yake aliwasisitiza
wananchi kuwa hivi sasa hakuna uchaguzi tena na kuwataka wasiendelee kukubali
kudanyaganywa kwani uchaguzi uliopo ni ule wa mwaka 2020.
“Nawasihi wananchi wenzagu tusiendelee kudanganywa
tukaambiwa kesho keshokutwa asubuhi, Rais wetu ni huyu hapa Dk. Shein, Rais
mpendwa watu na wala si mbaguzi maana katika serikali yake ametushirikisha vyema
vyama vya upinzani, nani angeweza kufanya mambo kama haya”,alisisitiza Waziri
Khatib.
Nae Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum, Said Soud
Said ambaye pia, ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Mwenyekiti wa Chama cha
Wakulima (AFP) Taifa, alisema kuwa tokea asubuhi alimuunga mkono Dk. Shein
baada ya kuuona uwezo wake mkubwa wa kuwaongoza Wazanzibari na kuahidi
kuendelea kumuunga mkono na kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi.
Alieleza sababu za kuunga mkono huko kunatokana na
kuwa vyama vya siasa havikuja kwa lengo la kufarakana na kugombana na watu ama kususiana
na kuwataka wananchi kuwakimbia na kuwaogopa kama UKIMWI wale viongozi wanaoongoza vyama vya siasa
wakaanzisha mambo kama hayo.
“Unapoingia katika ngoma ya beni basi ‘phisicali’
beni ni goma kubwa ambalo ni moja tu na zinazobakia zote ni ngoma ndogo ndogo,
sasa na hivi vyama vyengine vyote ni vigoma vidogo vidogo, beni ni CCM ndilo
linalopigwa na likaingia masikioni na kusisimua”, alisema Waziri Said.
Aidha, alitumia
fursa hiyo kuwaeleza vijana madhumuni ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964
ambayo yaliwafanya Wazanzibari kuamua kutekeleza mambo yao wenyewe na kuwataka
Wazanzibar kutokubali kuamuliwa mambo yao.
“….na Serikali hii anayoiongoza Dk. Shein ina
staili ya mdundiko mbele kwa mbele na
haina habari ya kurudi nyumba mmeeleza malalamiko yenu juu ya barabara
yenu ya Ukongoroni na Charawe hapa hapa mmepata majibu ”,alisisitiza Waziri
Said.
Hivyo, aliwasisitiza vijana kuheshimu Serikali yao
ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuheshimu Mapinduzi Matukufu ya Januari 12,
1964 kwa ajili ya kulinda na kujenga utu wao kama Wazanzibari.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment