Habari za Punde

UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA NI KICHOCHEO CHA MAENDELEO KATA YA CHONGOLEANI

      Matumaini mapya ya maendeleo ya haraka katika Kata                                                                 
  • Wananchi wajidhatiti kutumia fursa kujiinua kiuchumi
Tarehe 05 Agosti, 2017 ni siku ya kumbukumbu isiyosahaulika kwa wananchi wa Kata ya Chongoleani, tarafa ya Chumbageni, Wilaya Tanga kufuatia kuwekwa jiwe la msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga. Katika Makala hii Mwandishi Said Ameir wa MAELEZO aliyekuwepo katika tukio hilo anaelezea...
Ni tukio la kihistoria ambalo wananchi wa Kata ya Chongoleani na mitaa minne inayounda Kata hiyo hawatalisahau na litaendelea kukumbukwa kwa miongo mingi kama si dahari. Wapo watakaokumbuka tukio hilo kwa ujio wa viongozi wakuu wa nchi za Tanzania na Uganda.
Wapo wataokumbuka na kusimulia umati mkubwa wa watu mbalimbali wakiwemo wageni mashuhuri walipofika hapo kwa ajili ya sherehe hiyo. Lakini wengi wataikumbuka siku hiyo kwa kuwa ilikuwa chanzo cha safari ndefu ya mabadiliko makubwa ya maisha wa wananchi wa Kata hiyo.
Uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo ambao ulihudhuriwa na Marais wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli na Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, wageni mashuhuri kutoka nchi zote mbili pamoja na wadau wakubwa katika mradi huo ulikuwa wa aina yake.
Mahudhurio hayakuwa ya kawaida. Wananchi tangu saa kumi na mbili walianza kumiminika katika mtaa wa Putini na kutengeneza misururu mirefu ya karibu kilomita tatu ya magari na wananchi wanaoelekea huko.
Kweli mbiu ya mgambo ililia chambilecho wahenga “asiye mwana aeleke jiwe” na kweli ilipotimu saa mbili Putini hapakuwa na pa kutia mguu eneo lote lililokuwa limeelekeana na bahari ya Hindi lilikuwa limesheheni wananchi wa rika mbali mbali wakionesha shauku kubwa ya kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Eneo la Kigomeni katika mtaa wa Putini ndipo sehemu ambapo bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Abert ambalo wenyeji huko Uganda wanaliita ziwa Mwitanzige wakimaanisha ziwa lisilopitwa/lisilovukwa na nzige litakapohitimisha safari ya kilomita 1,445.
Bomba hilo ambalo asilimia themanini yaani kilomita 1,115, litajengwa Tanzania, litapitia katika mikoa 8, wilaya 24 na vijiji 184 ambapo maeneo yote hayo yatafaidika mradi huo.
Mafuta hayo yakifika katika eneo la Putini kabla ya kupakiwa kwenye meli kusafirishwa katika masoko ya kimataifa, yatahifadhiwa katika matangi makubwa matano yatakayojengwa katika eneo hilo yenye uwezo wa kuhifadhi lita 500,000 kila moja na kufanya jumla ya lita milioni 2.5 kwa wakati mmoja.
Miaka nenda rudi vijana wa leo au “wahenga wa kesho”watawaeleza watoto wao hali ilivyokuwa. Wala haitakuwa ya hadhithi za “paukwa pakawa” wala “hadithi njoo, uongo njoo na utamu kolea” bali uhalisia wa waliyoyaona, wengine kuyatenda na kuyafaidi!
Kata ya Chongoleani imo katika tarafa ya Chumbageni, kilomita 25 mashariki ya Jiji la Tanga katika barabara kuu inayokwenda mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kwa mujibu wa Afisa Tarafa ya Chumbageni Musa Machunda, Kata ya Chongoleani ina mitaa mine ambayo ni Chongoleani, Ndaoya, Putini na Mpirani. Kabla ya Tanga kuwa jiji mwaka 2014, kata hiyo ilikuwa na vijiji vitatu ambavyo ni Chongoleani, Mpirani na Ndaoya.
Baada ya mabadiliko ya mwaka 2014 kuifanya Tanga kuwa jiji, vijiji hivyo vilivunjwa na kuanzishwa mitaa ambapo Chongoleani iligawanywa kuwa mitaa miwili wa Chongoleani na Putini. 
Musa alimweleza mwandishi wa makala hii kuwa sehemu kubwa ya eneo la mradi ambalo lina ukubwa wa hekta 200 (wastani wa ekari 500) limo katika mtaa wa Putini ambapo pia ndiko sehemu ilipofanyika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi na sehemu iliyobaki limo katika mtaa wa Chongoleani.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka 2012, Kata ya Chongoleani hivi sasa ina wakaazi wapatao 5,242 na kaya 1,115 kutoka wakaazi 4,737 na kaya 1008 mwaka 2012 ikiwa ni wastani wa ongezeko la watu la asilimia 2.6 kwa mwaka. Kati ya wakaazi hao wanaume ni 2,562 na wanawake 2,680.
Shughuli kubwa za kiuchumi za wakaazi wa Kata hiyo ni kilimo na uvuvi. Kwa mujibu wa Afisa Tarafa huyo, Mtaa wa Putini ambako ndio kwenye ardhi yenye rutuba zaidi, wakaazi wake wanalima sana mihogo, ndimu, minazi na mahindi kidogo lakini kwa wakaazi wa mtaa wa Chongoleani ambako ardhi yake ni ya kichanga kulima muhogo, korosho na minazi.
Wananchi wa kata ya Chongoleani wanauona mradi huo wa bomba la mafuta na ujenzi wa ghati hiyo kuwa tegemeo lao kubwa la kuifungua Kata yao kimaendeleo.
 “Wananchi wameupokea vyema mradi huu na kujenga matumaini makubwa kwa Kata yao kupata maendeleo zaidi kwa kuongeza huduma na kwao wenyewe kuchangamkia fursa zitakazoletwa na mradi huu”anasema Mwenyekiti wa Mtaa wa Putini Abdalla Said Kanuni ambaye ni mzaliwa wa kijiji hicho.
Anasimulia kuwa Kata hiyo ina historia nzuri ya kutembelewa na viongozi wa kitaifa na kwamba ujio wa viongozi na wageni mashuhuri ingawa walikuja kwa tukio la kihistoria na la aina yake bali haukuwashangaza sana bali wanaamini kuwa ni mwendelezo wa baraka za Mwenyezi Mungu kwa mtaa wao.
Analisimulia kuwa wakati wa uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa miaka ya sitini Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alifika huko kuanzisha kijiji cha ujamaa ambapo pia aliwakabidhi wananchi ardhi ya zaidi ya hekta 200.
Kwa mujibu wa mzee Steni Mwalimu Yusuf mwenye umri wa miaka 70, mwaka 1962 wananchi wa vijiji vya Ndaoya, Mvuuni, Mabambani, Bagamoyo, Mabokweni na Chongoleani walituma ujumbe wa wazee sita kumuona Mwalimu Nyerere kumuomba wapatiwe ardhi ya eneo hilo ambalo lilikuwa ni sehemu ya shamba la kampuni ya mkonge ya Amboni ingawa kampuni hiyo ilikuwa hailitumii.
Mzee huyo anaongeza kuwa wakati Mwalimu alipokuja kuwakabidhi ardhi hiyo mwaka 1966 aliwauliza lengo la kutaka ardhi hiyo na walimjibu kuwa walitaka kuendeleza kilimo na kuanzisha kijji cha ujamaa.
“Alitupa ardhi hii hekta 200, akatukabidhi pia boti mbili za mashine na vifaa vya uvuvi pamoja na jembe la kulimia linalokokotwa na ng’ombe”anasimulia Mzee Steni ambaye ndie aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji kwa miaka mingi.
Alibainisha kuwa kampuni hiyo ilikubali kuwapatia eneo hilo kwa masharti ya kupatiwa eneo jingine ambapo serikali ilikubali kuwapa eneo jingine huko Kualagula wilaya ya Muheza.
Mzee Steni anaeleza kuwa “ameupokea kwa mikono miwili mradi huo” na kufafanua kuwa yeye amelipwa fidia kwa mazao na shamba lililochukuliwa na mradi huo ambalo lipo sehemu ilipofanyika sherehe la kuweka jiwe la msingi.
“nimelipwa kwa mujibu wa Sheria lakini kwangu mimi fidia ya ardhi haina kikomo kwa kuwa siku hizi watu wanazidi kuongezeka hivyo kila mtu anataka ardhi”anaeleza na kusisitiza kuwa kwake yeye ameridhika kwa kuwa ardhi hiyo imechukuliwa kwa matumizi ya maendeleo ya taifa.
Kuhusu matumizi ya fedha alizolipwa fidia anasema atazitumia kubadili nyumba yake kuwa ya kisasa, kusomesha watoto, kununua mifugo na kuendeleza kilimo.
Mzee Steni ambaye hivi sasa ni kibarua kwa watalamu wa kifaransa waliopo katika mradi huo anasema amejipanga kutoa huduma kwa mradi huu kwa kujiimarisha kiuchumi kwa kuendeleza kilimo cha mboga mboga katika ardhi nyingine aliyonayo na kubainisha kuwa atatafuta mbia ili aweze kuchimba kisima kwa ajili ya umwagiliaji.
“Tunatarajia kupata huduma zaidi za jamii...tunahitaji maendeleo…shule nzuri na zahanati mpya katika mtaa wetu”haya ndio matumanini yetu mengine,anaeleza.
Kuhusu wananchi kulipwa fidia na maoni yao kuhusu fidia hizo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Putini Bwana Kanuni anaeleza kuwa kati ya hekta 200 zilizochukuliwa na mradi, karibu hekta 170 ziko katika Mtaa wake na zilizobaki zikiwa katika mtaa wa Chongoleani.
“Katika mtaa wangu ambao una kaya 215 zenye wakaazi 1050, watu 170 walihusika na kulipwa fidia za maeneo yao; wapo waliolipwa fidia kwa mashamba yao, nyumba zao na pia kwa maeneo yaliyotumiwa na barabara”anaeleza Bwana Kanuni.
Hata hivyo anasema wako baadhi ya wananchi waliokuwa hawakuridhishwa na fidia hiyo na waliwasilisha malalamiko yao katika uongozi wa Halmashauri na pia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambako yameshughulikiwa.
Kama walivyonena wahenga kuwa “usilolijua ni usiku wa kiza” na ndivyo ilivyokuwa kwa kwa baadhi ya wananchi wa kata hiyo anasema Bwana Kanuni “wengine tuliwaza mambo makubwa makubwa tukasahau kuwa fidia inazingatia Sheria na kanuni zake”.
Anasema kuwa wapo waliowaza kununua boti kubwa kubwa za uvuvi, kuanzisha mashamba makubwa ya ufugaji wa kuku na ng’ombe na mengine mengi lakini haikuwa hivyo kwani wahenga hawakukosea waliposema “mipango si matumizi”.
Baada ya kulipwa fidia zao hivi sasa wengi wao wanafikiria kuimarisha nyumba zao za kuishi na pia kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya kutoa makaazi kwa watumishi wa mradi na zaidi kujiandaa kutoa huduma mbalimbali wakati wa ujenzi na baada ya kukamilika mradi.
Bwana Kanuni alibainisha kuwa watoa huduma kama za chakula wao wanasubiri kupatiwa rasmi eneo lao la kutolea huduma mara baada ya ramani kamili ya eneo kutolewa na waendesha mradi.
Kuhusu uwezekano kwa watanzania kutoka sehemu nyingine za nchi kuvamia eneo hilo kutafuta riziki, Bwana Kanuni anasema wao watawapokea kwa moyo mkunjufu na wako tayari “kushirikina nao bega kwa bega”  
Jambo la msingi na kubwa kwa mradi huu, anasisitiza Mwenyekiti wa Mtaa wa Putini, ni imani kubwa ya wananchi wa Kata ya Chongoleani kuwa utabadili maisha yao kutoka hali waliyonayo  sasa kuwa bora zaidi.
“Dalili tumeshaanza kuziona. Baada ya kuchongwa barabara hii tayari safari za daladala zimeongezeka mara tatu huku maombi zaidi ya kutoa huduma hiyo yamewasilishwa”alieleza.
Kuhusu suala la ajira alifafanua kuwa tayari vijana wameanza kufaidika na huduma za ulinzi ambapo hadi sasa vijana 80 wamepata ajira za muda kwa nyakati tofauti katika mradi huo.
Hata hivyo ili kuhakikisha vijana wa Kata ya Chongoleani wanapata ajira za ulinzi, anaeleza kuwa hivi karibuni Mshauri wa Mgambo wa Wilaya ameshatoa taarifa ya mafunzo kwa vijana wa Kata hiyo ili kuwaandaa kushika kazi za ulinzi katika mradi.
Mwananchi mwingine wa Mtaa wa Putini bwana Mwinjuma Waziri Mwinjuma ambaye naye ni miongoni mwa wananchi waliokuwa wakimiliki eneo sehemu ya eneo lilipowekwa jiwe la msingi la mradi anaeleza kuwa wananchi wote waliostahili kupata fidia akiwemo yeye mwenyewe wamelipwa na ameridhika kwa kuwa jambo hilo limefanywa kisheria.
Akizungumzia huduma za jamii, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Milapwa anaeleza kuwa hapana shaka yeyote kuwa maeneo hayo yataongezewa huduma hizo kwani mradi huo utaongeza mahitaji ya huduma hizo.
“Hata huduma za afya tunatarajia kuzipanua. Hivi sasa tunayo zahanati lakini mpango wetu ni kujenga kituo kipya cha afya ili wananchi pamoja na hao watakaohudumia mradi waweze kupata huduma hizo karibu na eneo la mradi” alibainisha Mkuu huyo wa Wilaya.
Tukio la kuweka jiwe la msingi ni historia itakayobaki katika kumbukumbu za wengi walioshuhudia tukio hilo wakiwemo waandishi wa habari ambao walifanya kazi nzuri kuuhabarisha umma ndani na nje ya nchi.  

Hapana shaka yeyote kuwa tukio lile ni miongoni matukio makubwa yaliyowahi kupewa uzito mkubwa na vyombo vya habari nchini. Kwa mradi huu vyombo vya habari havitakuwa ndio mwisho bali mwanzo wa safari ndefu ya kuandika historia ya mradi huu mkubwa ambao umedhihirisha udugu na ukaribu wa serikali na wananchi wa Tanzania na Uganda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.