Habari za Punde

Upandaji miti maskulini kusaidia changamoto za kimazingira


Na Habiba Zarali, Pemba
OFISA Mdhamini  Wizara ya Ardhi,Maji ,Nishati  na Mazingira Pemba, Juma Bakar Alawi, amesema utamaduni ulioanzishwa na Wanafunzi wa upandaji miti  maskulini, kutasaidia kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za kimazingira zilizopo katika maeneo yao wanayojifunzia pamoja na maeneo wanayoishi.


Kauli hiyo aliitowa katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa Skuli za Sekondari ya Kangani na Skuli ya msingi Makombeni Wilaya ya Mkoani Pemba, ambazo ni miongoni mwa Skuli zilizofanya vizuri katika mradi wa mazingira maskulini “ECO SCHOOLS”inayofadhiliwa  na  Zayadesa na kutekelezwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.



Alisema mradi huo ni miongoni mwa hatuwa zinazochukuliwa katika kutekeleza kwa vitendo malengo endelevu  ya sasa ya dunia, pamoja na utekelezaji wa lengo ambalo linahusika na utowaji wa elimu stahiki ya maendeleo endelevu ya rasilimali hiyo.



Alifahamisha udumishaji wa mazingira ikiwemo kupanda miti ni hazina kubwa iliyotoka  kwa wazee ambao waliweza kuilinda na kuiendeleza hadi kufikia leo hii, sasa basi ni jukumu la vizazi vya sasa kuona umuhimu
huo ambao utasaidia matumizi endelevu ya  rasilimali hiyo, ili  vizazi vijavyo navyo viweze kufaidika.



“Wanafunzi mradi huu ni fursa kwenu  wala musione kama ni utumwa kwani  upandaji wa miti ni usafi wa mazingira ambao hata dini ya kiislamu imehimiza na kusema muislamu ni usafi”alisema.



Alifahamisha ili nusra iweze kupatikana kwa kuepusha mmong’onyoko ,maporomoko  na maji ya bahari kupanda juu ni jukumu la jamii kuwa mstari wa mbele kupanda miti kwa wingi, sambamba na kupeana elimu ambayo itasaidia kuwashajihisha wale ambao bado uwelewa wao ni mdogo.



“Nyinyi wanafunzi ambao tayari mumeshapata mafunzo ya utunzaji wa mazingira kupitia Skuli zenu, sasa mutowe elimu majumbani ili nako jamii iweze kuelewa umuhimu wa utunzaji wa mazingira “alisema.



Kwa upande wake Mwenyekiti wa ECO SCHOOLS Zanzibar , Abdul-Aziz Mohammed Iddi , akitowa taarifa kuhusu mradi huo, alisema utawapatia nchi wanachama fursa za kuitambuwa ,kuziendeleza na kuzitekeleza njia ,mbinu na dhana za kukabiliana na changamoto endelevu za kimazingira kama vile mabadiliko ya tabia nchi ,matumizi ya rasilimali ,majanga ya kimaumbile ,udhibiti wa taka na uharibifu wa matumbawe.



Alisema Skuli kupitia mradi huo zina fursa kufanya kazi kwa pamoja katika kukabiliana na matatizo yanayozikabili nchi zinazoendelea za Visiwa vidogo vidogo kwa kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kwa kupata zawadi mbalimbali.



“Kwa kuwa mradi huu ni endelevu mwelekeo wake basi ni ushiriki wa wote ambapo uhamisho au kustafu kwa mwalimu au kumaliza Skuli kwa baadhi ya wanafunzi hakuwezi kuathiri uwepo wake”, alisema.



Mapema wakisoma risala ya eco program, Skuli ya Kangani walisema baada ya kuingia katika mradi huo wamepata  mwamko mpya juu ya uhifadhi wa mazingira ,kuimarisha usafi wa Skuli pamoja na jamii zao ,kujifunza
mambo mbalimbali ya asili kama vile kupiga kumba na madawa ya asili waliokuwa wakitumia wazee wao.



Walisema hadi sasa wanahifadhi mazingira ya bahari kwa lengo la kuzuwia mmong’onyoko  wa ardhi na kuzuwia maji chumvi kuingia katika mashamba na makaazi ya watu.



Jumla ya Skuli 30 teule za Serikali na za binafsi kutoka Zanzibar zinatekelezwa na mradi huo, ambapo kwa Unguja ni 21 na Pemba ni 9, na Skuli 12 ikiwemo ya Sekondari Kangani na msingi Makombeni zimeweza kufikia viwango vya  kujipatia tunzo mbalimbali zikiwemo  Ngao za Shaba na za Dhahabu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.