Habari za Punde

Akinababa Micheweni waaswa kutowatekeleza wake zao kwa kisingizio cha kutafuta Riziki

PEMBA, MARYAM SALIM.

Akinababa  katika Wilaya ya Micheweni Pemba, wameshauriwa kuacha tabia ya kuwatelekeza Wake zao na watoto kwa muda mrefu kwa  kisingizio cha kutafuta riziki kwani kuna uwezekanao wa kuzaliwa kwa matendo
yasiofurahisha katika Jamii.

Imefahamika kwamba ndani ya Wilaya hiyo kumekuwa na baadhi ya akinababa kuwatelekeza Wake zao na watoto kwa kisingizio cha kutafuta riziki (Kwenda dagoni kuvua) bila ya kuwachia matumizi ya aina yoyote ni hiyo kuwapa muda mgumu akinamama wa kuhudumia familia.

Ushauri huo ulitolewa na Sheha wa Shehia ya Chamboni Micheweni Pemba, Said Othman Kombo  ,wakati alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari hizi juu ya kuwepo wimbi la  akinamama na watoto waliotelekezwa na waume zao na kuishi katika maisha ya dhiki na watoto.

Alisema sula la udhalilishwaji kwa akinamama na Waume zao huonekana kama suala la kawaida bila kufahamu athari zake zinazoweza kujitokeza hapo baadae kwa watoto na akinamama wenyewe.

“ Wapo baadhi ya Wanaume huondoka majumbani kwao kwenda Dagoni kuvua kuanzia miezi 3 hadi mwaka  huku akiwaacha mke na watoto tena pengine Wajawazito na hakuna kitu chochote wanachoacha ama hata kuwapelekea kitu chochote cha matumizi wanapokuwa huko na hatimae mume anaporudi akiwa tayari  mtoto ameshazaliwa huku wakiwa wamekosa huduma muhimu alizofaa kuzipata wakati huo,” alisikitika Sheha huyo.

Alisema suala la  Wanawake kukimbiwa  na waume zao kwa kipindi kirefu bila ya kupata mahitaji ya lazima kutoka kwa Waume hao ni jambo ambalo limezoeleka hususan wale ambao huenda nje ya Zanzibar kwa shughuli za
uvuvi.

Sheha huyo, alieleza Wanawake hao bila ya kujali athari wanazopata baada ya kuambiwa na Wanaume zao kwa kipindi kirefu , wamekuwa wakijitegemea wenyewe wakiwa na mazingira magumu kwa kila kitu bila ya msaada wowote.

“Akinamama hao wanaotelekezwa hufika muda wakajishuhulisha na ubanjaji Kokoto , kwenda Baharini kupanda mwani kwa yule anaejiweza , kuchimba mawe ili waweze kujipatia fedha zitakazowasaidia kujikwamuwa na ugumu wa maisha huku Waume zao wakiwa hawana habari yoyote juu ya hali walioiacha huku nyuma ,” alisema Sheha huyo.

Alifahamisha kutokana na kadhia ya maisha magumu iliyowazunguka hujikuta hata watoto wao  ameshawashirikisha katika shughuli hizo pangine hata wakiwa Wanafunzi wa Skuli jambo ambalo hupelekea kukosa hali zao za msingi ikiwemo Elimu.

Alisema kutokana na tatizo hilo linalowakabili Wanawake wengi Vijijini , hupelekea kupata matatizo mbali mbali ikiwemo kushawishika na vitendo ambavyo havina maadili kwa kurubuniwa kifedha na watu wengine.

“ Kutokana na tatizo hilo kunahatari ya watoto kubakwa ama mama wenyewe na badala yake kuja wakapata maradhi ambayo sio ya kutarajiwa kama Vile Ukimwi n,k.” alieleza.

Alifahamisha athari zinazoweza kuwapata Watoto wanaojiingiza katika ajira za watoto ni nyingi kama vile kupata maafa , kutokea kwa mporomoko wa maadili , kwenda baharini kupara samaki na kukosa Elimu, jambo ambalo husababishwa na baba zao kuwatelekeza wao na mama zao kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Mwanakamati  wa maadili kutoka ndani ya Shehia ya Majenzi , Said Mbarouk Said, alisema suala la kutelekezwa kwa Wanwake na watoto lipo kwa kiwango cha juu ndani ya Wilaya ya Micheweni kwa
vile Wanaume wengi kazi zao ni Uvuvi na huku wakiwaacha wanawake na watoto bila kitu chochote ndani.

Alieleza sababu kubwa inayopelekea utelekezaji wa Wanaume na Watoto ni kutokana na baadhi ya akinababa kujifanya kutoelewa majukumu yao kwa wake zao pale wanapokuwa mbali nao na athari inayoweza kuwapata
akinamama na watoto wao pale wanapo kosa huduma muhimu za kijamii ikiwemo Chakula .

“ Wanawake wanapoachwa katika hali hiyo na watoto hubaki majumbani mwao wakijishuhulisha na kazi mbali mbali, ikiwemo upandani Mwani , ubanjaji kokoto , uchimbaji mawe kwa lengo la kujipatia fedha kidogo
zitakazo wasaidia na watoto na wakati mwengine hudiriki kusubiri misaada kutoka kwa jamaa zao ama hata kwa watu wengine,” alifahamisha
.

Akielezea hatuwa zinazochukuliwa kwa upande wa Mwanamke baada ya kukimbiwa kwa muda mrefu na mume wake bila ya mahitaji yoyote , ni kuwa na mazungumzo kati ya Famili ya mke na mume.

Alitowa ushauri kwa akinababa wenye tabia kama hizo kuacha kuacha kwani kumtelekeza Mwanamke hasa mke na Watoto bila ya kumpatia mahitaji  muhimu ni kosa kisheria za Kidunia hata kwa Mwenyeezi Mungu pia.

Nae , mama mmoja ambae hakutaka kutajwa jina lake gazetini kwa madai ya kulinda ndoa yake, alisema ni kweli suala hilo limezoeleka kwa Waume zao kuwaacha na watoto na kwenda Dagoni kuvua bila ya kuachia matumizi ama kuwapelekea pale wanapokuwa huko , lakini wamekuwa wakiishi kwa tabu tabu hadi pale watakapoamuwa kurudi.

Alieleza  ni vigumu mtu kuachiwa watoto peke yake awahudumie wakati baba hayupo , lakini hawana la kufanya ispokuwa ni kufanyakazi mbali mbali kama vile kupanda mwani , kubanja kokoto ili mradi watoto wapate
chakula na baadhi ya mahitaji na watoto wengine hukosa baadhi ya haki zao kama elimu.

“ Nikweli hali hiyo tumekuwa nayo kwa muda mkubwa hapa kijijini kwetu,lakini tunakabiliana nayo kiroho mbaya kwani mume akishaondoka itakubidi uhangaike uwapatie watoto angalau chakula cha mara moja,” alieleza .

Hivyo alisema ni vyema akinababa wanapoamuwa kwenda Dagoni kuvua kujipanga mwanzo kwa ajili ya kuwachia matumizi akinamama na watoto na kule wanapokwenda mambo yakiwa mazuri wasiwasahau kuwatumia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.