Habari za Punde

ZAECA Kisiwani Pemba Yamshiki Mwananchi Kwa Tuhuma za Kutowa Rusha.

Na Mwandishi Wetu Pemba.
Mohammed Said  Mohammed (46) Ngwachani anashikiliwa na  Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) Mkoa wa Kusini Pemba akituhumiwa kutoa rushwa ya shilingi laki moja ili kumshawishi mwananchi asitoe taarifa ya mashamba ya Serikali ambayo mtuhumiwa anayatumia kinyume na sheria .
Mtuhumiwa huyo amekamatwa na Mamlaka hiyo akidaiwa kutoa rushwa na shilingi laki moja kwa mwananchi (jina tunalo) ili asitoe taarifa ya mashamba ya Serikali ambayo mtuhumiwa anayamiliki kinyume na taratibu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi , Mkuu wa Mamlaka hiyo Mkoa wa Kusini Pemba Suleiman Ame amesema walipokea taarifa kwa mwananchi huyo akidai kuahidiwa kupewa fedha kiasi cha laki moja ili amsaidie mtuhumiwa kuyaficha mashamba ya Serikali .
Amesema  uwamuzi wa mtuhumiwa huyo kutaka kutoa rushwa , kumetokana na Serikali kuendesha zoezi la  uhakiki wa mashamba yake ili kuyakodisha ambapo baadhi ya mashamba ambayo yalikuwa katika zoezi la kukodishwa yanatumiwa na mtuhumiwa .
“Ni kweli tunamshikiliwa mtuhumiwa Mohammed Said Mohammed wa Ngwachani kwa tuhuma za kutoa rushwa  ya shilingi laki moja ili afiche taarifa za mashamba ya Serikali ambayo anayatumia kinyume na taratibu ”alifahamisha.
Amesema kuwa Mamlaka itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kukabiliana na wananchi wanaohujumu uchumi wa nchi ili kudhibiti mapato ya Taifa .
Aidha amewataka wananchi kushirikiana na Mamlaka katika kufanikisha udhibiti wa vitendo vya utoaji na upokeaji wa rushwa kwa maslahi ya nchi .
“Tunaomba sana wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA) ili kufanikisha udhibiti wa vitendo vya uhujumu wa uchumi ”alisisitiza.
Mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na Mamlaka na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinamkabili upelelezi utakapo kamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.