Habari za Punde

Wadau wa Elimu Wakutana Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kisomo Jijini Dar es Salaam.

Wanajopo walioshiriki mjadala huo kutoka kushoto ni Viola Julius mratibu wa tovuti ya iSwapMyBooks, Given Edward toka mtandao wa MyElimu,Kiya JK wa taasisi ya SEMA na  Irene Kiwia wa TWA network
Mmoja wa wachangiaji Bw. Yeriko Nyerere  akichangia jambo wakati wa siku hiyo
 Bw. Paschal Masalu kutoka Elimika Wikiendi akiendelea ku Tweet wakati wa Siku hiyo ya kisomo
Baadhi ya wadau mbalimbali wa Elimu wakiwa katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Kisomo

Wadau mbalimbali wa elimu wamekutana kuadhimisha siku ya kimataifa ya kisomo ambayo hufanyika Septemba 8 kila mwaka. Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya iSwapMyBooks kwa kushirikiana na SOMA pia Elimika Wikiendi ulihusisha mjadala wa namna ambavyo Tanzania inaweza kutumia faida ya uwepo wa nyenzo za kidigitali katika kusaidia watoto na watu wazima kujifunza.

Akifungua maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya SOMA Bi. Demere Kitunga alieleza namna ambavyo kwa miaka ya karibuni Tanzania imekuwa ikipiga hatua katika matumizi ya nyenzo za kiditali kutokana na usambaaji wa matumizi ya vifaa vilivyounganishwa na mtandao wa intaneti hivyo kupelekea uhitaji katika kutumia nyenzo hizi katika kuboresha namna ambavyo watoto wanaweza kujifunza masomo.

Wanajopo walioshiriki mjadala huo Irene Kiwia wa TWA network, Given Edward toka mtandao wa MyElimu, Kiya JK wa taasisi ya SEMA na Viola Julius mratibu wa tovuti ya iSwapMyBooks walielezea namna ambavyo taasisi zao zimekuwa zikitumia njia za kidigitali kuwahamasisha watoto na vijana  kujifunza kwa kubadilishana ujuzi kupitia mtandaoni.

Washiriki wengine kwa namna tofauti walionyesha wasiwasi kwa namna ambavyo utaratibu wa watu kujisomea unaendelea kutoweka na hasa kwa wazazi ambao wamekuwa hawana utaratibu wa kuwanunulia watoto vitabu badala yake kuwapa simu za mkononi ambazo wamekuwa wakizitumia kwa mambo yasiyofaa. Akijibu wasiwasi huo, Mkurugenzi wa taasisi ya SEMA ndugu Kiiya JK alisema ni wakati mitaala ya masomo ibadilike kuendana na hali halisi. “Tunalazimika kama Watanzania kutengeneza vitabu vinavyoendana na hali halisi ya maisha yetu kwa sasa, wenzetu wamegundua hilo na wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika kuchapisha vitu vinavyowafaa watoto wetu”.

Siku ya kimataifa ya kisomo ilianzishwa na shirika la UNESCO miaka 50 iliyopita ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Kisomo Katika Ulimwengu wa Kidigitali”.

1458109219454_logo_blog_za_mikoi.png

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.