Habari za Punde

Waziri Kheri Amewataka Watendaji wa Ofisi za Mabaraza ya Mji Kuwa Waadilifu

Na Masanja Mabula -Pemba.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Mhe. Haji Omar Kheri, amebaini madudu ya ukusanyaji wa mapato yanayofanyika katika baraza la mji wete, kwa baadhi ya watendaji kutumia risiti za iliyokuwa halmashauri ya wilaya hiyo na kujipatia fedha kwa maslahi yao.

Amesema Serikali inataarifa  kamili ya ubadhirifu huo unaofanywa na baadhi ya watendaji wa baraza hilo na kuikosesha Serikali mapato ambayo yalikuwa yatumike katika kuleta maendeleo ya wananchi.

Mh.Waziri ameyasema hayo, katika mkutano wa kukumbushana majukumu na watendaji wa Serikali wakiwemo wakuu wa wilaya, Mkoa ,vikosi vya usalama, halmashauri, madiwani na masheha, katika ukumbi wa Jamuhuri, Wete Pemba.

Amesema ,Serikali haitamfumbia macho na kumuhurumia mtendaji yoyote anaejihusisha na udanganyifu wakati wa kuwapatia huduma wananchi kwa njia zisizo halali kwa maslahi binafsi.

“Vipo vyombo vyetu, vya halmashauri na baraza la mji vinatumika kukusanya mapato haramu, waache mara moja, tutafanya maamuzi mara moja na hakuna ambae hawezekani’’, alisema Waziri huyo.

Sambamba na hayo amesema Wizara yake iko tayari kuwatoa kazini wanaothubutu kufanya vitendo hivyo kwa nia ya kuondoa kasoro zilizopo na kuweka sawa utekelezaji wa majukumu yao kwa maslahi ya nchi wanayoitumikia.

“Naomba kaimu unikabidhi risiti zangu za watu wanaokwenda wakikusanya mapato haramu sasa hivi tuone tunazifanyia kazi’’, alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, amewataka watendaji wa Halmashauri na mabaraza kufanya kazi kwa uadilifu pamoja na kujua majukumu yao ili kufikia dhamira ya kuingizia mapato Serikali ambayo yatasaidia kufikia malengo waliojiwekea.

Amesema kuwa, Serikali ya Mkoa itasimamia maagizo yaliotolewa na Waziri ili kuhakikisha watendaji wa Halmashauri na Baraza la Mji kwa kila mmoja anawajibika ipasavyo.

“Kwa agizo hili Serikali ya Mkoa haitakuwa na muhali kwa mtendaji yoyote ambae atashindwa kuwajibika katika majukumu yake aliyopangiwa”,alisisitiza.

Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa huo, Mberwa Hamadi Mberwa, amewataka watendaji wa taasisi hizo kusimamia na kufatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na kuhoji wanapobaini mapungufu ya kiutendaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.