Habari za Punde

Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Wahimizwa Kujiunga na Jumuiya Yao.

Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi akifungua mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni.
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud akieleza mafanikio ya Jumuiya tokea ilipoasisiwa mwaka jana katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja Ali Juma Ali akiwaeleza wananchama wa Jumuiya hiyo mikakati na mipango ya kuiendeleza ili kufikia malengo yake katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja wakifuatilia mkutano huo uliofanyika Baraza l a Wawakilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa Kaskazini Unguja Ali Juma Ali akiagana na Makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi baada ya mkutano wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ukumbi wa Baraza la wawakilishi la zamani Kikwajuni.

Picha na Makame Mshenga.
Na Miza Kona, Maelezo.
MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, ameitaka Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kuzidisha mshikamano  ili kuweza kubadilika kielimu na kuleta maendeleo mazuri mkoani humo.

Balozi Seif ameyasema hayo katika ukumbi wa  zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini Zanzibar katika mkutano wa Jumuiya hiyo.
Alisema vijana wengi wa mkoa huo wanakosa kuingia katika ushindani wa soko la ajira kutokana na kukosa sifa zinazohitajika.
Balozi Seif alisema jumuiya inaweza kuleta mafanikio makubwa  kwa kushirikana  pamoja na kuzidisha mshikamano katika dhamira ya kuibadilisha jamii ya mkoa huo kielimu.
Alifahamisha kuwa elimu ndio silaha pekee inayoweza kuwakomboa vijana na kuwawezesha kukubalika katika ajira mbalimbali na hivyo kuondokana na umasikini.
“Ni wakati sasa wa kubadilika kwa kuwekeza katika elimu ya watoto wetu ili kuwainua vijana na kuwawezesha kuhimili ushindani kwa kuwa na sifa zitakazoweza kuajiriwa au kujiajiri,” alifahamisha Balozi Seif.
Alieleza vijana wengi wa mkoa huo hawana mwamko wa kusoma, jambo linachangia mkoa wa Kaskazini kuwa nyuma kielimu na kimaendeleo ikilinganishwa na mikoa mingine nchini.
Amehimiza kuwepo ushirikiano wa pamoja baina ya viongozi na wana jumuiya katika kuishajiisha jamii ili iweze kubadilika kiuchumi na kuacha kuingiza itikadi za siasa katika suala la kuleta maendeleo.
Balozi Seif alisema jumuiya ina nia ya kuimarisha umoja na kuleta maendeleo katika mkoa huo.
Aidha Makamu wa Pili  wa Rais amewasisitiza viongozi wa majimbo na serikali katika mkoa huo kudumisha ushirikiano na kuwasaidia vijana wasio na uwezo wa kujikimu kwa kuwapa msukumo wa kimaendeleo pamoja na kuishajiisha jamii kujiunga jumuiya hiyo.
Jumuiya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja (NUDO), imeasisiwa mwezi Aprili 2016, na sasa ina zaidi ya wanachama zaidi ya 1000.
Lengo la kuanzishwa kwake ni kuendeleza, kuwezesha na kuijengea uwezo jamii ya mkoa huo katika kuinua ustawi wake kiuchumi, kijamii na mazingira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.