Habari za Punde

Watu wenye ulemavu Pemba wasema wameonyweshwa njia na ZLSC

Na. Haji Nassor - Pemba

WATU wenye ulemavu Kisiwani Pemba, wamesema sasa wanaweza kujitetea na kujitambua pale wanapovunjiwa haki zao za binadamu, kufuatia mafunzo mbali mbali waliopatiwa na Kituo chs Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba.

Walisema kabla ya kupatiwa mafunzo hayo hawakuwa na uwelewa wa kufuatilia, kujitetea, na kupigania haki zao za binadamu pale wana[povunjiwa ingawa kwa sasa hali inaridhisha.
Wakizungumza kwenye mkutano wa tathmini juu ya mfaunzo ya haki za binadamu waliopewa na Kituo cha Hudumza za Sheria Zanzibar katika kipindi kilichopita.

Watu hao wenye ulemavu walisema, wapo baadhi yao wameshavunjiwa haki zao na baada ya kujitetea na kufuatilia katika vyombo vya kisheria wamefanikiwa kupata haki zao.
Mwenyekiti wa Jumuia ya wasioona wilaya ya Mkoani Ali Hemed Khalifa, alisema hivi karibuni alilipwa shilingi 250,000 baada ya kuchaniwa shati lake na konda wa gari ya abiria.

“Nilimwambia anishushe Mtambile akanipitisha na jeuri juu, lakini wakati anataka kuondoka nikamzuia na kisha akanichania nguo yangu, lakini nilipofuatilia kituo cha Polisi, hatimae alinipa fidia ya kima hicho cha fedha”, alisema.

Nae mjumbe wa UWZ wilaya ya Wete Katija Mbarouk Ali, alisema hata yeye hivi karibuni alidhalilishwa kimaneno na vijana, lakini kutokana na uwelewa alifika Kituo cha Polisi na kisha ufumbzi ukapatikana.

“Baada ya kusikia nataka kwenda Polisi wale vijana walinifuata eti tuyamalize nje ya kituo, lakini kutokana na uwelewa niliopewa na Kituo cha Huduma za Sheria juu ya haki za bindamu, nilikataa na kuwafikisha Polisi”, alifafnua.

Nae Salma Abdalla mwanachama wa UWZ alisema, mafunzo waliopewa yalisaidia sana kwanza kujielewa wao na kisha wajibu wao pale wanapovunjia haki zao za binadamu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWZ wilaya ya Mkoani Malik Mohamed Omar, alisema baada ya mafunzo hayo, alishafika kwa uongozi wa bandari ya Mkoani na kuwaomba kwamba watu wenye ulemavu wasikae foleni na kufanikiwa.

Katika hatua nyengine watu hao wenye ulemavu, walisema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni kukosa ushirikiano wa dhati juu ya utekelezaji wa sheria yao kwa kuotekelezwa ujenzi wa majengo ya umma kuwa marafiki.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mratibu wa ZLSC tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed alisema, yapo makundi kadhaa ndani ya jamii walishayapa mafunzo na sasa wanaangalia tathmini ikiwa mafunzo hayo yameleta tija.

“Tunafanya tathmini juu ya mfaunzo ya haki za binadamu ambayo tuliwahi kuwapa kwa muda mrefu, maana tunataka kujua iwapo njia tuliotumia ni sahihi”, alifafanua.

Nae Afisa Tathimini na ufuatiliaji kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar Mohamed Khatib Mohamed, alisema tathimini wanayoifanya itawaelekeza kwa ajili ya mafunzo mengine kujua njia sahihi zaidi.

“Tathimini ambayo tunawafanyia nyinyi, sasa itatupa taarifa mpya, wapi tulikosa, au ikiwa njia tuliotumia haikuwa nzuri, sasa leo (jana) ndio tutaelewa”, alifafanua.


Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, kinaendelea na kufanya tathimini kwa wadau wake mbali wakiwemo watu wenye VVU, wenye ulemavu baada ya kuwapa mafunzo ya haki ya binadamu katika kipindi kilichopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.