Habari za Punde

Charawe Hoi kwa Kipanga yapigwa 4-0, KMKM yawatia adabu Kilimani City, Kesho ni Sailors na Boys


Na Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Timu ya Kipanga imefanikiwa kuibuka na ushindi mnene baada ya kuichapa Charawe mabao 4-0 katika mchezo wa ligi kuu soka ya Zanzibar Kanda ya Unguja uliopigwa saa 8 za mchana katika uwanja wa Amaan.

Mabao ya Kipanga mawili yamefungwa na Nassor Ali dakika ya 9 na 47 huku mabao mengine yakiwekwa nyavuni na Talib Hamad dakika ya 30 na Daud Nyerere dakika ya 87.


Saa 10 za jioni uwanjani hapo ulipigwa mchezo mwengine ambapo Timu ya Mabaharia wa KMKM imefanikiwa kuibuka na alama tatu muhimu baada ya kuichapa Kilimani City mabao 3-0.

Mabao ya KMKM mawili yamefungwa na Nahodha wao Mudrik Muhibu katika dakika ya 4 na 6 huku Salum Akida akimalizia la tatu katika dakika ya 89.

Mzunguko wa pili wa ligi kuu soka ya Zanzibar kanda ya Unguja utafikia tamati kesho kwa kupigwa mchezo mmoja katika uwanja wa Amaan majira ya saa 10:00 za jioni kati ya Mabaharia Weusi Black Sailors watasukumana na watoto wa Jang’ombe timu ya Jang’ombe Boys.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.