Habari za Punde

Dk Mabodi atoa nasaha nzito kwa makada wa CCM


 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akifungua Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini "B"  huko Mahonda katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja uliofanyika leo.



 Baadhi ya Wajumbe wa mkutano Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini "B"  wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dk. Mabodi huko Mahonda.

-Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano huo Balozi Seif Ali Idd akipiga kura katika uchaguzi wa CCM ngazi ya Wilaya ya Kaskazini "B" uliofanyika leo huko Mahonda katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja uliofanyika leo.


Na Is-haka Omar, Zanzibar.

CHAMA cha  Mapinduzi (CCM) Zanzibar viongozi watakaochaguliwa kupitia Uchaguzi wa ngazi ya Wilaya ya Kaskazini “B” kichama Unguja kuwa mstari wa mbele kukemea vikali tabia ya makundi na safu za uongozi zenye nia ya kuhatarisha uhai wa CCM katika Wilaya hiyo.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk. Abdalla Juma Mabodi wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wilaya hiyo wa kuwachagua  viongozi wa nafasi mbali za ngazi hiyo huko Mahonda katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 Alisema matarajio ya CCM ni kuona viongozi  wanaochaguliwa katika uchaguzi huo wanachukia kwa vitendo uwepo wa baadhi ya makada wanaoendekeza  makundi, Safu na rushwa ndani ya chama hicho.

Dk.Mabodi alieleza kwamba msimamo wa CCM ni  kuhakikisha Katiba, kanuni na miongozo inasimamiwa  na kufuatwa ipasavyo ili kupata viongozi na makada wenye uwezo wa kuendeleza mafanikio ndani ya chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Aidha aliwambia viongozi watakaopata nafasi ya kuchaguliwa kupitia uchaguzi huo wahakikishe wanajenga ngome imara ya kisiasa katika wilaya hiyo sambamba na  kuwashawishi wapinzani waliomo katika Wilaya hiyo kujiunga na CCM kwani ndio chama pekee kinachojali maslahi ya wananchi wote.

“Baada ya kukamilika uchaguzi huu wa ndani ya chama chetu tuna jukumu jingine la kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2020 pamoja na kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kama tulivyoahidi kwa wananchi.”, alisisitiza  Dk. Mabodi.

Aliwasihi  makada watakaochaguliwa kuwa viongozi kushirikiana vizuri na makada wenzao ambao hawakupata fursa ya kuchaguliwa kwa lengo la kuendeleza misingi imara ya ukomavu wa kisiasa na Demokrasia  iliyotukuka.

Hata hivyo aliwapongeza wanachama hasa makada waliogombea nafasi mbali mbali kwa kutofanya kampeni za fujo, vurugu na kuchafuana hali aliyosema kuwa inaonyesha ishara njema ya kukamilika kwa uchaguzi huo bila kujitokeza mapungufu.

Aidha alisema chama hicho baada ya uchaguzi huo kinakusudia kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo  viongozi wa ngazi mbali mbali za chama hicho ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Naibu Katibu Mkuu huyo Dk. Mabodi aliwataka wanachi hasa wanachama wa chama hicho kupuuza kauli zinazotolewa na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif za kuwa ataapishwa kuwa Rais wa Zanzibar  jambo ambalo haliwezi kutokea kwani Rais halali wa Zanzibar ni Dk. Ali Mohamed Shein mpaka mwaka 2020.

Katika uchaguzi huo nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Wilaya , Katibu wa Siasa na Uenezi, nafasi ya mkutano Mkuu wa Mkoa , nafasi ya Mkutano Mkuu wa taifa pamoja na nafasi ya Halmashauri kuu ya CCM Wilaya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.