Habari za Punde

HESLB Yatangaza Majina ya Awamu ya Kwanza Waliopangiwa Mikopo Kwa 2017-2018.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Abdul-Razaq Badru akiongea na waandishi wa habari kuhusu upangaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2017/2018 leo (Jumatano, Oktoba 18, 2017) katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronica Nyahende (Picha: HESLB).

TAARIFA KWA UMMA

ORODHA YA KWANZA YA MAJINA YA WALIOPATA MIKOPO 2017-18

Jumatano, Oktoba 18, 2017

Waombaji wa Mwaka wa Kwanza
 Tunapenda kuwafahamisha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 kuwa, baada ya uchambuzi wa maombi yao, Orodha ya Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupangiwa mikopo imekamilika.

Kiasi cha Tshs 34.6 bilioni kimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196. Kwa ujumla, Tshs 108.8 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
  
Orodha hiyo ya kwanza inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz) na itatumwa kwa vyuo husika. Orodha nyingine (batches) zitafuata kadri taratibu za udahili na uchambuzi zinavyokamilika. Lengo ni kutoa majina ya wote waliofanikiwa kupata mkopo kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba, 2017.

Orodha hii ya wanafunzi 10,196 imepatikana baada ya kupokea na kuchambua Awamu ya Kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495waliopata udahili katika chuo kimoja. Itakumbukwa kuwa moja ya sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji kupata udahili katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali.

Wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mikopo, watapangiwa mikopo baada ya kuchagua na kuthibitisha chuo watakachojiunga kwa ajili ya masomo.

Tshs 318 bilioni zatengwa kwa ajili ya wanaoendelea na masomo

Wakati huohuo, tunapenda kuwafahamisha wanafunzi wa elimu ya juu wanaoendelea na masomo na umma kwa ujumla kuwa tunatarajiakuanza kutuma vyuoni fedha za mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefaulu mitihani yao kuanzia leo, Jumatano, Oktoba 18, 2017.

Kiasi cha Tshs 318.6 bilioni kitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka wa masomo 2017/2018. Tayari Serikali imeshatoa fedha hizo na lengo la Bodi ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondoloea wanafunzi usumbufu.

Hitimisho
Bodi ya Mikopo inawasihi waombaji wa mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea kukamilisha maandalizi ya orodha zinazofuata za wanafunzi waliopata mikopo. Tutaendelea kutoa taarifa kwa vyombo vya habari na tovuti ya Bodi mara kwa mara.
Mwisho.
Imetolewa na:
ABDUL-RAZAQ BADRU
MKURUGENZI MTENDAJI
JUMATANO, OKTOBA 18, 2017

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.