Habari za Punde

‘JUMWAMPE’ yagundua haya kwa wakulima

Na. Haji Nassor - Pemba.
KAMATI ya Ushawishi na Utetezi kutoka Jumuia ya mtandao wa wakulima wa matunda na mboga mboga Kisiwani Pemba JUMWAMPE, imesema imegundua changamoto kadhaa zinawazowakabili wakulima wao, ikiwa ni pamoja na kukosa elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo.
Kamati hiyo, ilipita kwa wakulima zaidi ya 100 kisiwani humo, na baada ya kuwajazisha dodoso maalum, waligundua kuwa wakulima hao, hawana elimu ya matumizi ya dawa za mimea, hali inayotishia usalama wao na walaji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Chakechake mara baada ya kumalizika kwa safari ya kuwatembelea wakulima, Katibu wa Jumuia Mtandao huo Hamad Ali Mussa, alisema wapo waliowagundua kutumia dawa ya kuulia kunguni kwa kutumia kwenye mazao.

Alisema jengine waliloligua wakati wakiwa na wakulima hao, ni kutokuwa na kipimo sahihi cha kunyunyizia dawa hizo, kwenye mboga mboga zao, ambpo hupelekea muda mfupi baada ya kutia dawa kuvunwa na kuuzwa sokoni.

Katibu huyo alieleza kuwa, hilo pia linaweza kusababisha athari ya kimwili kwao, walaji na hata wanyama wanaowapa malisho, baada ya kumalizika kwa uvunaji.

“Huu tuliofanya sio utafiti hasa, ni kama tumewatembelea na kuonana nao, lakini utafiti hasa tutaufanya baadae, ili kugundua changamoto hasa zinazowakabili wakulima wetu na wafugaji, maana wao ndio tegemeo letu kwa ajili ya chakula”,alifafanua.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Mtandao, Zainab Rajab Iddi, alisema kwenye msafara wao huo, piwa wamegundua baadhi ya wakulima hao, kutokuwa na uhakika wa matumizi ya maji, kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.

Alieleza kuwa, wapo wanaolalamiki bili kubwa ya maji au kukatiwa maji na ZAWA, jambo ambalo wamesema linawarejesha nyuma, katika sekta hiyo walioichagua.

“Wapo waliolalamikia kuwa hukatiwa maji na ZAWA hata kama ndio kwanza mazao au mboga mboga zao hazijapevuka, hali ambayo huwakosesha mwendo wa kufikia maendeleo yao”,alieleza.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo ya ushawishi na utetezi kutoka ‘JUMWAMPE’ Saada Hamad Kombo, alisema  ambalo jengine walioligundua na kuamua kuitafuta sera ya kilimo, ni kuwepo kwa maduka ya wauza pembejeo bila ya mpangilio, hali inayosababisha na wakulima nao kununua wapendavyo.

Aliongeza kuwa, hilo linawapa shida wakulima, kwanza kununua dawa wasizozijua matumizia yake sahihi wala vipimo vyake, maana muuza pembejeo yeye anachotaka ni biashara yake iende tu, na sio kuangalia usalama wa anaemuuzia”,alifafanua.

Kufuatia safari hiyo ya kuwatembelea wakulima, Mjumbe mwengine wa Kamati hiyo, Hassan Shamis Hassan, alisema sasa wanachotarajia kukifanya, ni kuipitia kwa umakini sera ya kilimo, ili kuona inasemaje hasa kwa uingiaji, uuzaji na utumiaji wa pembejeo zenye kimikali.

“Ingawa pia tulishakwenda ZAWA na kupendekeza tuwe na mikatab, au wizara ya biashara na viwanda kuahidi kuzitangaaza biashara za wakulima wetu, lakini pia lazima serikali iangalie uwezekano wa kutupia macho biashara ya pembejeo”,alieleza.

Aidha kamati hiyo, imeshauri kuwepo kwa umakini mkubwa wa uingiaji wa pembejeo kisiwani Pemba, aina ya mbegu za matunda na mboga mboga, sambamba na kuwajengea uwezo mabibi na mabwana shamba, ili wakulima wapate utaalamu na ushauri wao wakati wote”,alifafanua.

Mkulima wa mboga mboga shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake Mkubwa Ali Mkubwa, alisema kwake yeye kubwa analoliona linamrejesha nyuma ni ukosefu wa soko la uhakika.

Nae mkulima wa vitango, mchicha na tungule wa Vitongoji Mohamed Khamis Song, alisema hivi karibuni alikuwa na vitango 700 ambavyo alikosa soko la uhakika na kuviuza chini ya bei.

“Kitango kimoja nililazilimika kukiuza kwa bei ya shilingi ya 150 na shilingi 200, maana tulikosa soko la uhakika, sasa lazima serikali ituangalie sasa tumeshatekeleza agizo la kujikusanya pamoja”,alifafanua.


Jumuia Mtandao wa wakulima wa mboga mboga na matunda kisiwani Pemba ‘JUMWAMPE’ ambayo iliasisi tokea mwaka 2008 kwa kuanza mkoa wa kaskazini Pemba pekee, na sasa kuwa ya Pemba nzima, inadhamira ya kuwawezesha wakulima hao, ili wazalishe bidhaa zenye ubora na zinazokubalika sokoni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.