Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Azungumza na Walimu wa Vyuo Vya Kiislam na Balozi wa Saud Arabia Ofisini Kwake Vuga Zanzibar.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi akizungumza na uongozi wa jumuiya ya walimu wa madrasa wanaopiga vita vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia Zanzibar afisini kwake Vuga
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Saudi Arabia Mohammed Al Malik, alipofika Ofisini kwake kwa Vuga kwa mazungumzo leo
Na.Mwandishi wa OMPR 
Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi amezitaka Jumuiya zisizo za kiserikali (NGO) nchini kufanya kazi ambazo wameruhusiwa kwa mujibu wa katiba zao.

Makamo wa pili wa rais ameyasema hayo afisini kwake Vuga alipokuwa akizungumza na uongozi wa Jumuiya ya walimu wa madrasa wanaopinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Amesema zipo baadhi ya Jumuiya zimeazishwa kwa malengo ya kijamii lakini baada ya muda mfupi jumuiya hizo hujiingiza kwenye siasa na kuacha kazi zao za msingi.

Balozi Seif ametoa onyo kwa jumuiya hizo kuacha tabia hiyo mara moja vyenginevyo Serikali itazifuta mara moja.

Akizungumza kuhusu udhalilishaji wa kijinsia nchini Balozi Seif amewapongeza wanajumuiya walimu wa madrasa wanaopinga vitendo vya udhalilishaji kwa uamuzi wao wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na vitendo vya ubakaji nchini.

Amesema ametiwa moyo wa walimu hao wa madrasa kwa kuwa mstari wa mbele kupambana na ubakaji unaofanywa na baadhi ya wenzao hapa nchini.
Balozi Seif amesema juhudi hizo za walimu wa madrasa za kupambana na ubakaji nchini zinawatia moyo wazazi na kuwaomba wanajumuiya kujenga umoja miongoni mwao katika kupambana na udhalilishaji.

Naye Mwenyekiti wa  Jumuiya ya walimu wa madrasa wanaopinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia mwalimu Shabaan Rashid Ndondole amesema Jumuiya yao imeundwa baaada ya kuona baadhi ya walimu wa madrasa wanaipaka matope kwa vitendo vyao vibaya kada hiyo ya ualimu wa madrasa.

Mwalimu Shaaban imeiomba Serikali na wahisani mbali mbali  kuisaidia Jumuiya hiyo kwa kuipatia vifaa vya afisini pamoja na usafiri kwani lengo lao ni kupambana na ubakaji nchi nzima.

Wakati huo huo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi amekutana na Balozi wa Saudi Arabia Balozi Mohammed Almalik aliyekuja kuwasilisha ujumbe wa Serikali yake.

Katika mazungumzo yao Balozi Seif ameipongeza Serikali ya Saudia kwa misaada yake ambayo inasaidia kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar.

Viongozi hao wawili pia wamezungumzia suala la kuimarisha utaratibu wa kwenda Hija kwa mwakani na kukubaliana suala hilo kulifanyia kazi zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.