Habari za Punde

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania JPM Ahamasisha Watanzania Kumuenzi Baba wa Taifa Kwa Kuwa Wazalendo.

Na: Genofeva Matemu – WHUSM
Tarehe: 14/10/2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewataka watanzania wote kuishi maisha aliyoishi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kuacha kuwa wabinafsi na kufanya kazi kwa maslahi ya watanzania wote.
Hayo ameyasema leo wakati wa sherehe za kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na wiki ya vijana kitaifa iliyoazimishwa katika uwanja wa Amaan Mkoani Mjini Magharibi Zanzibari.

“Watanzania wanatakiwa kujenga taifa kwa vitendo vinavyodumisha amani, upendo na mshikamano kama ambavyo Mwl. Nyerere alipambana kujenga taifa lenye uhuru wa kweli linalojitegemea na lenye watu wanaojali na kuheshimu utu wa kila mmoja”.

Akizungumzia Mwenge wa Uhuru  Mhe. Magufuli amesema kuwa mwenge wa uhuru ni alama ya uhuru na utaifa wetu ambao umekua ukiimarisha muungano wetu kwa kuwaunganisha watanzania na kuchochea maendeleo  kwa kujenga na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuzindua miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo dhana yake ni kukuza utu na ustadi wa watanzania.

Kwa upande wake Kiongozio wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2017 Bw. Amour Hamad Amour amesema kuwa Mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu zimefanya kazi kubwa ya kuwakumbusha watanzania kuimarisha mshikamano, kujenga umoja wa kitaifa na kuhamasisha ukamilishaji miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuhakisi dira ya mwelekeo wa seriakali ya awamu ya tano kwa kusisitiza uwekezaji katika viwanda ili Tanzania iweze kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na wenye ulemavu Mhe Jenista Mhagama amesema kuwa watanzania wote na hasa vijana hawana budi kulinda urithi wa mwenge wa uhuru kwani ni muhimu kwa mstakabali wa nchi ya Tanzania

Mhe. Jenista amesema kuwa mbio za mwenge wa uhuru siku zote zimekua ni kichocheo cha maendeleo ya wananchi katika kuwahamasisha, kubuni, kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku mwenge huo ukitumika kufichua na kupambana na maaduni wa maendeleo hususani adui rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa rasilimali za umma, mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi, malaria na matumizi ya dawa za kulevya hadi hapo maadui hawa watakapotokomezwa katika nchi ya Tanzania.


Mwenge wa uhuru uliohasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1964 ni tunu na alama ya uhuru na utaifa wetu, huleta amani, mshikamano, uzalendo na umoja wa taifa letu la Tanzania

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.