TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
|
Oktoba 06, 2017
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tamko la THBUB kulaani tukio la Bwana Nassoro Msingili
kukatwa mkono
Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kukatwa
mkono kwa mtu mwenye ualbino, Bwana Nassoro Msingili (75) wa Kijiji cha
Nyarutanga Kata ya Kisaki, Morogoro Vijijini, tukio lililotokea usiku wa
kuamkia Jumanne Oktoba 3, 2017.
Tume inalaani
vikali kitendo hicho cha kikatili. Aidha, Tume inaungana na Watanzania wengine
nchini kote kumpa pole Bwana Msingili na kumtakia apone haraka.
Tume,
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa elimu kwa Watanzania kwa
ujumla kuhusu umuhimu wa kuheshimu utu, haki na stahiki mbalimbali za watu wenye
ualbino kwa kuwa ni binadamu sawa na binadamu wengine.
Aidha,
Tume inavitaka vyombo vyote vya dola pamoja na wananchi kwa ujumla kutoa ulinzi
kwa watu wenye ualbino, ambao wako kwenye hatari ya kushambuliwa. Kinachojidhihirisha
kutokana na yaliyomkuta Bwana Msingili ni dhahiri kuwa jukumu hili
halijafanyika kikamilifu.
Tume
inapenda kuwakumbusha Watanzania wote kuhusu kuheshimu na kulinda haki za watu
wenye ualbino. Kwa hiyo Tume:
1. Inaikumbusha Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti vitendo
vya kikatili kwa watu wenye ualbino nchini na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo
hili.
2. Inawakumbusha wananchi kuwa vitendo vya ukatili, mauaji, na matendo yote
yanayokiuka Sheria yanayofanywa na raia wasio wema ni ukiukwaji wa Sheria, haki
za binadamu na misingi ya utawala wa sheira; Hivyo Tume inakemea matendo haya
na kutaka yapigwe vita.
3. Inapendekeza Kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi za Wilaya, Kata,
Vijiji na Vitongoji wakiwemo watendaji watimize wajibu wao ili kuhakikisha
usalama wa watu wenye ualbino katika maeneo yao.
4. Inalipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua za kuwakamata watuhumiwa haraka. Aidha,
inaliomba Jeshi hilo lifanye uchunguzi wa kina na kuwafikisha mbele ya vyombo
vya sheria wote watakaobainika kuwa walihusika na ukatili huo.
5. Tume na wadau wengine wataendelea kutoa elimu zaidi kwa umma kuhusu haki za
watu wenye ualbino na masuala ya haki za binadamu na wajibu, sheria, utawala
bora na uraia.
Mwisho, Tume inatoa
wito kwa wananchi wa Kijiji cha Nyarutanga na maeneo mengine kutoa ushirikiano
kwa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wote waliohusika na unyama huu
wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
MWENYEKITI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU
NA UTAWALA BORA
Oktoba 6, 2017
No comments:
Post a Comment