Na
Salmin Juma , Pemba
''Tupeni miradi tunayoweza kuifanya
sisi kama wazee, kwani tunahitaji kujikwamua hasa ukizingatia wazee roho zetu
zimeshatangalia kwa Mungu hivyo hatuwezi kufanya hiyana katika miradi hiyo na
tofauti na vijana wa leo wanapopewa miradi''
Hii ni kauli yakutilisha imani na kusikitisha iliyotoka kinywani mwa Mzee Ali Omar Abdalla mwenye umri wa miaka 73
mkaazi wa vitongoji wilaya ya Chakechake mkoa wa kusini Pemba.
Kauli hii imekuja wakati alipokua
akizungumza nami juu ya hali ya kuthaminiwa, kujaliwa na kuenziwa kwa wazee wa kisiwani Pemba.
Ilikua ni katika harakati za kutafuta
habari ikiwa ndio desturi yangu maishani katika ulimwengu wa tasni ya habari,
nilikutana na wazee wengi katika maeneo tofauti ya kisiwa hiki cha Pemba ambao
kiujumla wao niliwaona wapo katika hali isiyoyakuridhisha kimavazi na hata katika
mtazamo wa kawaida wanaonekana ni wenye kuchoka kwa shida achiliambali uzee
wanaoendelea kuwavaa.
Wazee hao baada ya kuwaona, moyoni
nikajengeka hamu ya kutaka kuzungumza na baadhi yao ili kutaka kujua, jee uzee wao ndio sababu ya
wao kua katika hali kama niliyokwisha ieleza hupo juu.
Kwa lengo la kutaka kujua, safari ya
kwanza nilielekea huko Wingwi Mapofu mkoa wa kaskazini Pemba, ambapo nilikutana na wazee wengi wasiopungua
10 kike kwa kiume, nami nikaketi chini baada ya kukaribishwa na hapo ndipo ulipokuwa
mwanzo wa maongezi yetu, lengo ikiwa ni kutaka kujua ni kwa namna gani wazee
wenye umri wa kuanzia miaka 60 kwenda
juu wamekua wakijaliwa na kuthaminiwa nchini mwetu, hasa ukizingatia miongoni
mwao wamo wastaafu ambao walishajitolea nguvu zao miaka mingi kutumikia nchi
hii.
Wakati tukiendelea na mazungumzo huku
nikiwadadisi kutaka kujua wao kama wazee wana eneo maalum ambalo wanaweza
kufikisha kiliochao pindi wanapofikwa na shida , nikagundua kuwa kumbe kuna
mpango kabambe uliyotengengezwa kwa lengo la kuwasaidia nao ni ''Mabaraza ya
wazee'' katika kila shehia.
Na kati ya hao niliyokaa nao kumbe
alikuwamo M/kiti wa baraza la wazee wa shehia ya Wingwi Mapofu mzee Mzee Salum Said Ali (67), tulizungmza mengi
na ya kutosha lakini makubwa kati ya hayo alisema, nia na makusudio ya baraza
lao ni kujikwamua na hali ngumu za kimaisha wanazokumbana nazo wazee pamoja na
kuwa na chombo cha kufikisha na kushtaki kiliochao.
Alisema lengo la baraza lao ni zuri
lakini bado hawajafikia lengo kuu ambalo ni kumuona mzee anakua katika
mazingira mazuri yaliyokusudiwa ingawa wameshaanza kuona mwanga na wangali wanajipa
matumaini makubwa.
''Serikali ipo lakini sio kila kitu
tuikumbizie serikali, sisi kama wazee tunaweza kujisaidia na ndio maana tukakaa
pamoja kupanga mikakati ya kupiga hatua za kimaendeleo mbele'' alisema Mzee
Ali.
Katika hatua nyengine alisema ingawa
wana azma kubwa ya kujisaidia lakini pia inawawiya vigumu kufikia malengo
kwasababu ya upungufu wa pesa za kujiendeshea, alitolea mfano kwakusema ''
unapata semina ukashiriki mafunzo fulani mjini chakechake lakini nikijitazama
sina kitu mfukoni, naamua kufunga safari hivyo hivyo hatimae nachelewa na
nikifika hakuna kitu nilichowahi'' alisema Mzee Ali.
Mzee Ali aliendelea kunieleza kuwa, kutokana
na hali hiyo ngumu wanayokabiliana nayo kwa makusudi wakamua kuweka utaratibu
wa kuchangishana kila mwezi shilingi 1,000/= ili kujikwamua pale wanapokwama.
Hali za wazee hao kwakweli bado
zinaonekana kuwa dhaifu kiuchumi, sikusita kuwauliza , jee muna mradi wowote ambao mumeuanzisha au
munaotaka kuuanzisha ili alau mupate ahuweni katika mambo yenu? alinijibu
''Ndio tumeanzisha nasari ya minazi na mpaka muda huu tunaminazi 85 ambayo tunatarajia
kuipanda vizuri baadae tuuze nazi ili kipato kikue katika baraza letu'' alisema
Mzee Ali.
Baraza hili linaonekana kukamilika ,
lina mratibu wa shuhuli zao zote bw:
Said Yussuf Hamad, Katibu wa baraza Bi Fatma Rashid Nassor na wajumbe wake 10
ambao ni mchanganyiko wa wanawake na wanaume.
Nilichojifunza ni kwamba, wazee wamethubutu
na wameweza na ndio maana wakamua kujikusanya pamoja kuunda baraza la wazee ili
kukaa pamoja na kuzaa mbinu mbadala ya kujondoa katika hali ngumu za kimaisha, kama
waswahili wanavyosema ''UKUBWA DAWA''
Lakini juu ya kuthubutu kwao hali ya
wazee hao inaonekana kuwa ngumu kiuchumi na katika maeneo mengine muhimu ya
huduma za binaadamu.
Nimeyasema haya kwa sababu mmoja kati
ya wajumbe hao Mzee Hamad Faki Mwinyi
(80) alinieleleza kuwa ingawa wanabaraza hilo na linawasaidia katika mambo
mengine lakini bado huduma ya afya ni kikwazo '' bado kutibiwa ni tatizo, kama
huna pesa ni tatizo'' alisema Mzee Mwinyi.
Baada ya mazungumzo hayo nikafunga
tena safari moja kwa moja mpaka maeneo ya Vitongoji mkoa wa kusini Pemba nako
nikakutana na wazee kama wale wa Wingwi, walikua na baraza baraza ya wazee
shehia ya Vitongoji, na mwonekano wao pia haukupishana na wale wa kule Wingwi, walionekana
kuchoka kimwili , niliomba kuzungumza na mwenyekiti wa baraza hilo ambae ni
Mzee Ali Juma Khamis kwa heshima na taadhima walinikaribisha na kuanza
mazungumzo yetu, narudia tena hapa, lengo langu ni lile lile kutaka kujua ni
kwanamna gani wazee kisiwani Pemba wanajaliwa na kuthaminiwa?
Mzee Juma aliniambia, baada ya kuona
hali zao zimekua mbaya na hakuna wa kuwafatilia moja kwa moja wakaanzisha
baraza la wazee , waweze kujisemea shida zao pamoja na mahitaji yao yote.
Alisema kabla ya uwepo wa baraza hilo
mambo yalikua ni mashaka matupu, huduma za afya bora kwao ilikua ni kama ndoto
na hata ikitokea misaada hakuna anaowaona lakini hali hivi sasa kidogo
inaonekana kuwa nzuri kupitia baraza lao la wazee.
Hakika maneno haya yanatia moyo na
sasa unapata picha uwepo wa mabaraza haya ya wazee ni dira ya maendeleo kwao.
Akiendelea kunielezea faida
wanazonufaika nazo mwenyekiti huyo alisema kwa mambo yanavyokwenda huko baadae
wanatarajia kupata mafunzo tofauti ya kimaendeleo na yatasimamiwa na baraza
hilo hilo kuonyesha kwamba wazee wanaweza na si wakubezwa.
''Wazee tulikua tunatupya, lakini
sasa hivi tunatarajia kupitia baraza letu hili mambo yatakua safi sana'' alisema
Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake mshika fedha wa
baraza hilo Bi Jine Ali Abeid (67) alisema bado wanaiomba serikali na wadau
wengine wajitokeze kuwapatia miradi maalum ya wazee ambayo wataweza kuiendesha
wenyewe.
Alitolea mfano wa miradi hiyo kama vile
miradi ya biashara ambapo alisema, wakiekewa mradi wa duka wanaweza kuuwendesha
vizuri na malengo yakafanikiwa , pia wanahitaji kinu cha kusagishia nafaka na
kwa upande mwengine hata kuwezeshwa kukopeshana wao kwa wao.
Utafiti niliyoufanya umenionyesha
kuwa kuna mawazo mazuri yaliyowekwa kwaajili ya kuwathamini wazee lakini juhudi za kufanikisha malengo hayo bado
zingali zinasuasua ,ingawa wazee wenyewe wanatamaa ya maisha bora lakini muda
mrefu utapita.
Kabla ya kufanya hitimisho katika
jambo hili, niliwatafuta jumuiya ya wazee Zanzibar (JUWAZA) ili kuona nao
wanamtazamo gani juu ya mabaraza haya ya wazee na vipi wamepanga kuwasaidia.
Nilibahatika kukutana na mratibu wa
mabaraza ya wazee Pemba kutoka jumuiya hiyo Bi Sifuni Ali Haji alisema,wao kama
ni wadau wakubwa kwa mabaraza hayo, na wanafurahi kuwepo kwa wingi kwani ndio
kutapatina maendeleo sahihi kwa wazee hao.
Alisema JUWAZA wanawatembelea
mabaraza hayo ili tujue wanamipango gani ya kimaendeleo , badae wanaichukua
mipango hiyo na kuwatafuta wadhamini na wahisani ili wawezeshwe kufikia
malengo.
Bi Sifuni alitoa wito kwa kuwataka
masheha wote katika kisiwa cha pemba kuunda mabaraza ya wazee kwani kutasaidia pakubwa
katika kuwatatulia wazee shida zao ambao wanaonekana kuwa katika hali ngumu za kimaisha hivi sasa.
Sambamba na hayo, Bi Sifuni alitoa
wito kwa wahisani kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudu hizo ambapo na mimi
hapa ndipo ninapotaka kukazia kamba.
Wazee kisiwani Pemba wanateseka na
wanaendelea kuhilikika katika kila eneo la maisha , katika upande wa sekta ya
afya matibabu ni mtihani mkubwa kwao, hata misaada mengine ya kawaida kuipata
ni nadra.
Tukumbuke kuwa sio wazee wote
kisiwani Pemba wana uwezo wa kumudu huduma za kimaisha , wapo wasiojiweza , wanaoteseka
katika kusaka huduma hizo, kwapamoja tuungane kuwakomboa wazee wanaonekana kuwa
katika madhila makubwa.
Serikali na taasisi zake, wahisani na wadau wote wa maendeleo , pamoja
jitokezeni kudhamini mabaraza haya ya wazee, kwa lengo lile lile la kuwatatulia
shida zinazowakabili katika maish, ili nao ifike siku wajione wanathaminika
katika kisiwa hiki.
No comments:
Post a Comment